Harmonize atoa tamko ishu ya Sh1 bilioni na Ibraah

Muktasari:
- Harmonize ameiambia Mwanaspoti kuwa anamuacha Ibraah aongee lakini mwisho wa yote anapaswa atambue kuwa "hii ni biashara iliyowekezwa na yalifanyika makubaliano na wala sio vita" hasa ikizingatiwa hajafukuzwa kwenye Lebo ya Konde Gang.
Sakata linaloendelea la msanii Ibraah kushindwa kujindoa katika lebo ya Konde Gang baada ya kuambiwa kwanza alipe Sh1 bilioni na hivyo kufikia hatua ya kuomba msaada wa michango kwa watu ili aweze kulipa pesa hiyo, mmiliki wa lebo hiyo Harmonize ameongea mazito.
Harmonize ameiambia Mwanaspoti kuwa anamuacha Ibraah aongee lakini mwisho wa yote anapaswa atambue kuwa "hii ni biashara iliyowekezwa na yalifanyika makubaliano na wala sio vita" hasa ikizingatiwa hajafukuzwa kwenye Lebo ya Konde Gang.
"Nilisema sitaongelea hili suala la Ibraah kwani makubaliano yote yaliyofanyika anayajua na ukiangalia hajafukuzwa Konde Gang bali ametaka yeye kuondoka, mwisho wa siku atambue hii ni biashara iliyofanyika makubaliano na wala sio vita," alisema nyota huyo wa ngoma ya 'You Better Go'.
"Ila ikifika muda wa mimi kutakiwa kuzungumza nitazungumza tu, lakini kwasasa sina zaidi ya hayo, na najua nini nafanya mimi," amesema Haramonize.
Ibraah ambaye mwaka 2020 alitambulishwa rasmi kuwa msanii wa lebo ya muziki ya Konde Gang, aliandika ujumbe kupitia ukurasa huo akiomba msaada kwa Watanzania wamchangie Sh1 bilioni ili aachane na Konde Gang.
"Daah hili mimi limenishinda narudi kwenu Watanzania, mzee Konde anataka nimlipe Sh1 bilioni, mimi tangu nianze muziki sijawahi hata kuingiza hata robo ya Sh1 bilioni, kwa itakayempendeza hata ukiwa na jero, buku nisaidie wangu...mimi sitaki kupishana na Mzee Konde, ila hili suala la kulipia Sh1 bilioni linaninyima usingizi, hofu yangu pia kipaji changu kupotea na sina kazi nyingine. Kwa yeyote atakayejaaliwa chochote.
"Sio mbaya kukubali kuwa mimi ni kijana niliyetokea kwenye familia ya kimasikini na hili limenikuta sina budi kulileta kwenu maana pia ninachoamini nisingefika hapa bila ninyi mashabiki wangu na wadau mbalimbali katika sanaa na nje ya tasnia. Naomba msaada kwa yeyote anayeona anaweza kunisaidia."
Ibraah tangu alipotambulishwa katika Lebo hiyo ameachia nyimbo kali kadhaa ikiwamo; Dharau, Nitachelewa, Sawa, Wandoto, Jipinde, Rara na amefanya vizuri pia katika kolabo ambazo ameshirikishwa kama Mdomo ya Harmonize, Mateso ya Mabantu na nyimbo za singeli kama Do Let Me Go ya Kinata MC na Wivu ya JayCombat.