Si mchezo... Rihanna mjamzito tena, sikia alichokisema!

Muktasari:
- Rihanna aliyefunika na kibao chake, Umbrella (2007), katika tamasha la kifahari la Met Gala 2025 hapo juzi, ndipo alionyesha ujauzito huo zikiwa ni siku chache kabla ya mtoto wake wa kwanza kutimiza umri wa miaka mitatu.
MKALI wa Pop na RnB Marekani, Rihanna, 37, anagonga vichwa vya habari duniani baada ya kuweka wazi anatarajia kupata mtoto wa tatu pamoja na mpenzi wake wa kitambo rapa Asap Rocky, 36, kutokea nyumbani kwao Barbados.
Rihanna aliyefunika na kibao chake, Umbrella (2007), katika tamasha la kifahari la Met Gala 2025 hapo juzi, ndipo alionyesha ujauzito huo zikiwa ni siku chache kabla ya mtoto wake wa kwanza kutimiza umri wa miaka mitatu.
Mpiga picha wake, Miles Diggs ndiye alikuwa wa kwanza kufichua habari hizo kupitia Instagram akichapisha picha za mwanamuziki huyo akiwa amevalia sketi na blauzi huku ujauzito wake ukionekana vizuri kabla ya kuibuka katika zulia jekundu.
Asap Rocky ambaye ni mwenyekiti mwenza wa Met Gala mwaka huu, aliwaambia waandishi wa habari kwenye zulia jekundu kuwa anajisikika vizuri kutarajia mtoto mwingine na Rihanna, mwanamuziki aliyeuza rekodi zaidi ya milioni 250 duniani.
"Ni wakati wa kuwaonyesha watu kile tulichokuwa tukiandaa. Na nina furahi kila mtu ana furaha kwa ajili yetu kwa sababu tunafurahi, nadhani unaelewa," alisema Asap Rocky, mwanachama wa kundi la Hip Hop la Asap Mob liloanzishwa mwaka 2006.

Ikumbukwe ukaribu wao ulianza kuonekana hadharani walipotumbuza remix ya wimbo, Love It (2011) katika tuzo za MTV VMAs 2012, na baadaye Asap Rocky akaonekana katika video ya wimbo wa Rihanna, Fashion Killa (2013).
Mnamo Desemba 2019 wakapita pamoja juu ya zulia jekundi la tuzo za British Fashion na kufika Novemba 2020 wakathibitisha wao ni wapenzi na kwenda mapumzikoni katika visiwa vya Barbados na wote wamezaliwa huko.
Mtoto wao wa kwanza RZA alizaliwa Mei 13, 2022, mwaka uliofuatia Rihanna akajifungua mtoto wa pili, Riot hapo Agosti 1, 2023, na sasa ikiwa ni baada ya mwaka mmoja ana ujauzito mwingine, kwa kifupi hapoi wala haboi!.
Chanzo kimoja cha karibu na familia hiyo yenye utajiri wa zaidi ya Dola1.4 bilioni, kimeuambia mtandao wa People, Rihanna na Asap Rocky wanataka watoto wao wakue kwa pamoja na ndiyo sababu ya uzazi huu wa karibu karibu.
"Rihanna amekuwa akitaka kuwa na familia kubwa siku zote, kwa hiyo bado hajatosheka, wana furaha kukuza familia yao na wana shauku kubwa kuwapatia wavulana wao mdogo wao," chanzo hicho kilieleza na kuongeza.
"Walitaka watoto wao wafuatane kiumri ili wakue pamoja na kushirikiana vizuri, kama familia wanajisikia kubarikiwa na wanashukuru sana kwa baraka hii kubwa inayokuja katika maisha yao. Ni wakati wa kipekee sana kwao," ilielezwa.

Aprili 2024 katika mahojiano yake na Interview Magazine, Rihanna alifunguka mambo mengi kuhusu malezi na familia, huku akigusia kiu yake ya kupata mtoto wa kike baada ya kujaliwa wavula hao wawili.
"Sijui Mungu anataka nini, lakini ningependa kuwa na watoto zaidi ya wawili. Nijaribu kupata msichana wangu, lakini bila shaka akiwa ni mvulana mwingine, basi ni mvulana wangu mwingine," alisema Rihanna.
Rihanna alipoulizwa na mwanamitindo Mel Ottenberg kuwa anataka kuwa na watoto wangapi maishani mwake, alijibu kadiri Mungu anavyotaka awe nao huku akigusia uhusiano wake na Asap Rocky ulivyo na nguvu katika malezi.
"Mtu anapokuona na kukuamini na kufikiria unastahili kuwa mama wa watoto wake, ni hisia nzuri. Nilihisi hivyo hivyo kumhusu, nilijua angekuwa baba bora," alisema staa hiyo wa kibao, Diamonds (2012).
Kauli ya Rihanna ilikuja baada ya hapo awali Asap Rocky kuulizwa iwapo kuna wimbo wa ushirikiano kati yake na mama watoto wake watakuja kuutoa na kusema ushirikiano pekee watakaofanya ni kuleta watoto duniani na siyo kwenye muziki.
"Nadhani tunafanya kazi nzuri sana katika kushirikiana, kuzaa watoto. Nadhani huo ndiyo ubunifu wetu bora hadi sasa. Hakuna kitu bora kuliko hicho huko nje," alisema Asap Rocky aliyetamba na wimbo wake, Praise The Lord (2018).
Kufikia Oktoba 2024 wawili hao wakazungumza na Jarida la W, Asap Rocky, mshindi wa tuzo mbili za BET, alifunguka kuhusu malezi ya watoto wao wawili wa kiume, RZA, 2 na Riot, 1.

"Nadhani RZA atabaki kama alivyo kwa sababu ni lango (mzaliwa wa kwanza), Riot ni mtu asiyejali, yeye ni kama mama yake. RZA ni zaidi ya baba yake, ni kama mimi tu, ni pacha wangu," alisema Asap Rocky na kuongeza.
"RZA amerithi komwe la mama yake lakini vitu vingine vyote alipata kutoka kwangu. Ninapenda komwe la kijana wangu kama ambavyo nilimpenda sana mama yake," alisema rapa huyo wa kibao, LSD (2015).
Kwa upande wake Rihanna, mwanamuziki mwenye albamu tisa, alisema Asap Rocky ni baba mzuri ambaye anashiriki vilivyo katika malezi na watoto wao wamekuwa wakimpenda kutokana na kujitoa kwake.
"Nilimpenda kabla ya kuwa baba, hii ni kubwa kuliko, ilikuwa kama mshangao ni kiongozi gani huyu, mvumilivu na mwenye upendo na hata watoto wangu wanavutiwa naye," alisema Rihanna na kuongeza.
"Katika yote mimi ni historia tu, ni ziada. Ndiyo!, inatokea, haijalishi ikiwa ni wasichana au wavulana; wanampenda baba yao kwa njia tofauti, na mimi hupenda kuwaona hivyo," alisema mwanzilishi wa chapa ya vipodozi, Fenty Beauty.
Hata hivyo, hatua hii ya Rihanna kutarajia mtoto mwingine mwaka huu, inazidi kuondoa uwezo wa ujio wa albamu yake ya tisa ambayo imesubiriwa kwa muda mrefu tangu alipotoa, ANTI (2016), miaka tisa iliyopita, hivyo ni wazi ameamua kujenga familia kwa sasa.
Ikumbukwe kabla ya kuwa na Asap Rocky, Rihanna alihusishwa kutoka na Drake baada ya kuwa na ukaribu wa kikazi lakini mrembo huyo akiongea na Vanity Fair mwaka 2015 alikana hilo na kudai mpenzi wake wa mwisho alikuwa ni Chris Brown.
Drake kupitia wimbo 'Fear of Heights' kutoka katika albamu yake ya nane, For All the Dogs (2023), anasikika akimchana mwanamke ambaye anadai penzi lao kipindi cha nyuma lilikuwa la kawaida sana, kwa kifupi hakuwa na maajabu.
Kauli hiyo ilimchefua Asap Rocky, akaamua kujibu kupitia wimbo aliyoshirikishwa na Kid Cudi 'Wow' kutoka katika albamu ya Insano (2024) iliyokutanisha wakali wengine kama Travis Scott na Lil Yachty.
Katika wimbo huo wa dakika nne, Asap Rocky alitoa maneno makali kwa Drake na kudai hamsumbui na kutaka athibitishe kama ni kweli alitoka na Rihanna, huku akidai ana dawa ya tumbo baada ya hapo awali Drake kueleza kusumbuliwa na tumbo.