Wasanii Bongo wanashindwa kuitumia Basata vizuri

Muktasari:
- Kinachonishangaza ni kwa nini wasanii hawawapi Basata kazi ya kufanya kiasi kwamba baraza hilo linaonekana kama lina kazi moja tu; kufungia kazi za sanaa zinazokiuka maadili.
KARIBU kila msanii maarufu Tanzania ana kibali cha usanii kutoka Baraza la Sanaa Tanzania (Basata). Ili kupata kibali msanii anapaswa kusajiliwa na ili asajiliwe ni lazima alipe ada ya uanachama.
Kinachonishangaza ni kwa nini wasanii hawawapi Basata kazi ya kufanya kiasi kwamba baraza hilo linaonekana kama lina kazi moja tu; kufungia kazi za sanaa zinazokiuka maadili.
Sio mara moja, bali mara nyingi tumeona wasanii wakilalamikia mikataba mibovu na ya kinyonyaji wanayopewa na lebo, wadau, kampuni na washirika wengine wa kazi za sanaa.
Mfano wa karibuni ni sakata lililomhusisha Billnass ambaye aliandika kuhusu bosi wa mmoja wa kampuni ya usambazaji wa kazi za sanaa akidai kudhulumiwa mapato ya ngoma yake ya Puuh aliyomshirikisha Jay Melody. Unajua Billnass aliandika hayo wapi? Instagram.
Mwanasheria wa aliyeshutumiwa kwa dhuluma alijibu kwamba Billnass hakudhulumiwa, bali kilichotokea ilikuwa ni sehemu ya makubaliano ya kimkataba aliouingia mwenyewe. Kwa msingi huo aliyetajwa kama mdhulumaji anadai fidia kwa kuchafuliwa jina.

Sakata la Billnass ni mfano tu, lakini yapo matukio mengi kama hilo. Na kila mara jambo kama hilo linapotokea huwa nina maswali mawili kichwani kwanza, kwanini msanii aliingia kwenye mkataba mbovu? Pili kwa nini anakimbilia kulalamika kwenye mitandao ya kijamii?
Swali la kwanza linahitaji kutulia kidogo kulielewa kwa sababu katika maisha ya kawaida karibu kila mtu anaweza kuingia kwenye mkataba mbovu siku moja, hasa kwa sababu wengi wetu hatuna uelewa wa mambo ya kisheri. Pia wengi hatuna uwezo wa kumlipa wakili au mtaalamu wa sheria.
Lakini kwa msanii aliyesajiliwa Basata, hiyo haipaswi kuwa kikwazo maana msanii anaweza akatimba pale Basata na kuomba msaada wa kupitia mkataba.
Basata wanaweza kumpa mtaalamu bure au kwa gharama nafuu na msanii akawa amejiepusha na matatizo makubwa mbele ya safari. Sasa kwa nini wasanii hawafanyi hivyo?

Swali la pili, la kukimbilia Instagram kulalamika. Linahitaji mahesabu kidogo. Kupeleka mambo Instagram inasaidia nini? Kwa nini asiende Basata - baraza linalosimamia sanaa na wasanii wote nchini? Kwa nini msanii asiende Basata ili aliyempa mkataba mbovu aitwe wakae mezani, wasikilizwe na kusaidiwa kupata suluhu? Badala yake majina ya watu yanatajwa mtandaoni, biashara zinachafuliwa na mwisho wake msanii anakumbana na kesi ya kudaiwa fidia kwa kuchafua jina.
Wasanii wakumbuke wale wazee pale Basata wanalipwa kwa fedha za walipakodi wa Tanzania pengine na ada zao za uanachama pia. Wapo pale kwa ajili ya kuwasaidia wasanii na kukuza sanaa ya Tanzania.
Inawezekana wale wazee kila kukicha wana kazi ya kufungia ngoma za wasanii kwa sababu wanakaa ofisini bila kazi, wanaboreka. Wasanii pelekeni matatizo yenu Basata wazee wapate kazi. Watawasikiliza, watawasaidia.