Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasanii 10 Bongo wenye wafuasi wengi Instagram 2024

Kwa miaka zaidi ya 10 sasa Instagram umekuwa mtandao maarufu duniani kote ukiwa na watumiaji zaidi ya bilioni 2.4, ni jukwaa linalotumika na wasanii wengi wa muziki kutangaza kazi zao kwa mamilioni ya wafuasi wao. 

Wasanii wa Bongo Fleva wamejikusanyia mashabiki wengi kwenye mtandao huo ulioanzishwa Oktoba, 2010 na kuwafanya kuongoza sio Tanzania tu, bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki. 

Utakumbuka Selena Gomez ndiye mwanamuziki mwenye wafuasi wengi Instagram duniani akiwa nao milioni 429, huku Influencer Marketing Hub wakimtaja kulipwa Dola 2.5 milioni, wastani wa Sh6.2 bilioni ili kuchapisha tangazo moja katika ukurasa wake.

Hii ni orodha ya wasanii 10 wa Bongo Fleva ambao wana wafuasi wengi Instagram hadi kufikia Januari 2024, huku watatu pekee wakiwa ndio wenye wafuasi zaidi milioni 10.


1. Diamond Platnumz - milioni 17.1

Sio Tanzania tu, bali Afrika Mashariki yote inamtambua Diamond Platnumz ndiye msanii namba moja kwa wafuasi wengi Instagram akiwa nao milioni 17.1, kwa Afrika ni Davido wa Nigeria ndiye anaongoza, Diamond yupo ndani ya 10 bora.

Hadi Desemba 2015 Diamond alikuwa ndiye msanii mwenye wafuasi wengi Instagram barani Afrika akiwa nao milioni 1.5, ila kufikia Septemba 2016 akashushwa na Davido aliyefikisha wafuasi milioni 2.9 kwa wakati huo na sasa ana milioni 28.6.


2. Hamisa Mobetto - milioni 10.8

Aliingia rasmi kwenye muziki mwaka 2018 na baadaye kuachia EP yake, Yours Truly (2022), muziki na kazi yake ya awali ya mitindo zimempatia Hamisa wafuasi milioni 10.8 Instagram akiwa ni mwanamke wa nne Afrika Mashariki kuwa na namba za juu. 

Hamisa alivuma baada ya kutwaa taji la Miss XXL, After School Bash 2010, kuibuka mshindi wa pili Miss Dar Indian Ocean 2011, mshindi wa pili Miss Kinondoni na kuingia nusu fainali ya Miss Tanzania 2011, huku akiingia 10 bora ya Miss University Africa 2012.


3. Shilole - milioni 10.3

Wengi wanajiuliza ilikuwaje ghafla Shilole akapata wafuasi wengi Instagram. Hadi sasa ana milioni 10.3, ukiachana na muziki na biashara zake, usheshi wake katika mitandao, mahojiano na vyombo vya habari na matukio mengine vimempa mashabiki wengi.

Kwa Afrika Mashariki Shilole ni mwanamke wa tano kuwa na wafuasi wengi Instagram baada ya Zari The Bosslady (Uganda) - milioni 11.8, Wema Sepetu (Tanzania) - milioni 11.2, Lupita Nyong'o (Kenya) - milioni 11, na Hamisa Mobetto (Tanzania) - milioni 10.8.


4. Harmonize - milioni 9.9

Mwimbaji huyo wa Konde Music Worldwide kwa jumla anatarajiwa kuwa staa wa sita Bongo kufikisha wafuasi zaidi ya milioni 10 Instagram baada ya Diamond Platnumz, Millard Ayo, Wema Sepetu, Hamisa Mobetto na Shilole.

Harmonize ambaye sasa ana wafuasi milioni 9.9 Instagram, ni hivi karibuni tu amefikisha 'views' zaidi ya bilioni 1 YouTube akiwa msanii wa tatu Afrika Mashariki kufikia mafanikio hayo baada ya Diamond na Rayvanny.


5. Rayvanny - milioni 9.8

Kuanzia WCB Wasafi hadi Next Level Music (NLM), Rayvanny ametengeneza nyimbo maarufu ndani na nje na kumpatia mamilioni ya mashabiki ambao ndio sehemu ya wafuasi yake Instagram wanaofikia milioni 9.8.

Rayvanny anashiriki tuzo za Grammy zitakazotolewa Februari 5, 2024, ni baada ya wimbo 'Mama Tetema' aliyoshirikishwa na Maluma kujumuishwa katika albamu ya Maluma, Don Juan (2023) anayowania kipengele cha 'Best Latin Pop Album' 2024. 


6. Alikiba - milioni 9.6

Tangu alipochukua usikivu wa wengi na kibao chake, Cinderella (2007) kilichobeba jina la albamu yake ya kwanza chini ya G Records, Alikiba amefanikiwa kuishikilia nafasi yake katika tasnia na hadi sasa ana wafuasi milioni 9.6 Instagram.

Hadi sasa ameshinda tuzo za kimatifa kama All Africa Music Awards (AFRIMA) 2017 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana Afrika (Aje) ft. M.I (Mr. Incredible) na MTV Europe Music Awards (MTV EMA) 2016 kama Msanii Bora Afrika.


7. Nandy - milioni 9.2

Kitendo cha kutoa albamu moja, The African Princess (2018) na EP tatu, Taste (2021), Wanibariki (2021) na Maturity (2022), ni moja ya mambo yaliyopelekea Nandy kuwa msanii mkubwa na kujizolea mashabiki wengi ambao milioni 9.2 wanamfuata Instagram.

Nandy aliyetoka kimuziki chini ya Tanzania House Talent (THT) na wimbo wake, Nagusagusa (2016), ni msanii wa pili wa kike Tanzania kufikisha 'views' milioni 100 YouTube na 'streams' milioni 100 Boomplay Music akiwa ametanguliwa na Zuchu.


8. Vanessa Mdee - Milioni 8.7

Kwa sasa anaishi huko Georgia, Marekani na mchumba wake Rotimi na watoto wao wawili, Seven (2021) na Imani (2023), familia hii inafuatiliwa sana kwenye mitandao ya kijamii ikiwa ni moja ya mambo yaliyompatia Vanessa Mdee wafuasi milioni 8.7 Instagram.

Hadi anatangaza kuachana na muziki, Vanessa alikuwa ameshatoa albamu moja, Money Mondays (2018), ameshinda tuzo za TMA, AFRIMA, AFRIMMA n.k, huku akianzisha lebo yake, Mdee Music iliyowasaini Mimi Mars na Brian Simba.


9. Ommy Dimpoz - milioni 7.7

Kuanzia Top Band, Unity Entertainment, Poz Kwa Poz (PKP) hadi RockStar Africa na Sony Music alipotoa albamu yake ya kwanza, Dedication (2022), Ommy Dimpoz amejipambanua kama mwimbaji bora na sasa mashabiki milioni 7.7 wanamfuta Instagram.

Huyu ndiye msanii wa kwanza kushinda tuzo za TMA mara mbili mfululizo kwenye kipengele cha Wimbo Bora wa Kushirikiana, alishinda mwaka 2012 na 2013 kupitia nyimbo zake, 'Nai Nai' na 'Me and You' alizoshirikiana na Alikiba na Vanessa Mdee.


10. Linah - milioni 6.8

Ukiachana na muziki wake mzuri, hakuna ubishi Linah amepata wafuasi wengi Instagram hasa kutokana na aina ya maudhui anayoweka kwenye ukurasa wake, picha zake kali za kuvutia tayari zimempatia wafuasi milioni 6.8.

Ni Linah huyu ambaye ndiye msanii wa kwanza wa kike Tanzania kufanya kazi na Director wa Afrika Kusini, Godfather ambaye aliongoza video ya wimbo wake, Ole Themba (2014) iliyogharimu Dola 30,000, wastani wa Sh75.4 milioni kwa sasa.