Wakali waliopiga kolabo na Chibu

KUTOKANA na ushawishi na ukubwa wa chapa yake katika muziki, wasanii wa ndani na nje wamekuwa wakipigana vikumbo ili kufanya kolabo na Diamond Platnumz kwa sababu kila ambaye alipata nafasi hiyo, basi wimbo wake ulifanya vizuri.
Hilo limefanya Diamond kushirikishwa na wasanii wengi hasa wale wa Bongofleva tangu mwaka 2012 hadi 2023, na hii ni orodha ya wasanii 10 waliomshirikisha Diamond kwenye nyimbo zao zaidi ya mbili.
1. SHETTA - NIDANGANYE & KEREWA
Kutoka kuwa dansa wa Misifa Camp kwa Dully Sykes hadi kuishika Bongofleva haikuwa kazi rahisi kwa Shetta, ila kolabo yake ya kwanza na Diamond, Nidanganye (2012) ikafanya vizuri sana na kumfanya kusahau misoto maana ilimpa maokoto sio ya kitoto.
Mafanikio ya wimbo huo yakapelekea Shetta kumshirikisha Diamond katika wimbo mwingine, Kerewa (2014) ambao video yake iliyofanyika Afrika Kusini kwa Director Godfather iligharimu Dola 10,000 ikiwa ni video ya kwanza kwa Shetta kutoa fedha nyingi.

2. LINEX - NITAIFICHA WAPI & SALIMA
Wengi watawakumbuka Linex na Diamond kwa kufanya kazi pamoja katika mradi wa Kigoma All Stars ulitoa wimbo maarufu, Leka Dutigite (2012) wakiwamo mastaa wengine kama Mwasiti, Banana Zorro, Ommy Dimpoz, Baba Levo, Chege, Peter Msechu n.k.
Kabla ya hapo, Linex alikuwa amemshirikisha Diamond katika wimbo wake, Nitaificha Wapi (2012), kisha ikafuata ngoma nyingine, Salima (2015) ambayo video yake ilileta mgogoro kati ya Director Adam Juma na Linex ambaye alidai haikutoka vizuri.
3. NAY WA MITEGO - MUZIKI GANI & MAPENZI AU PESA
Rapa huyo kutokea Free Nation alimshirikisha Diamond kwenye ngoma yake, Muziki Gani (2013) ambayo ilifanya vizuri sana na kumuongezea mashabiki wengi hasa wa kike na kumpatia dili kutoka moja ya kampuni za simu za mkononi.
Baadaye Nay akaona kufanya kolabo na Diamond ni bidhaa inayouzika kwa urahisi ndipo wakaachia wimbo mwingine, Mapenzi au Pesa (2016) ingawa haukuweza kufanya vizuri kama ule wa mwanzo na hata video yake hawakuitoa.
4. HARMONIZE - BADO & KWANGWARU
Staa huyo wa Konde Music Worldwide akiwa bado ndani ya WCB Wasafi, alimshirikisha Diamond katika nyimbo tatu, mbili kati ya hizo ni Bado (2016) na Kwangwaru (2018) ambao ndio wa kwanza kwa Harmonize kwa video yake kufikisha ‘views’ milioni 100 YouTube.
Haikuishia hapo, Harmonize akaja kumpa shavu Diamond na Burna Boy wa Nigeria katika wimbo wake ‘Kainama’ unaopatikana katika EP yake kwanza, Afro Bongo (2019) ambayo iliwakutanisha wasanii wengine kama Mr. Eazi, Patoranking na Yemi Alade.

5. ZUCHU - CHECHE & LITAWACHOMA
Baada ya hapo Aprili 2020 kutambulishwa WCB Wasafi akiwa ni msanii wa pili wa kike baada ya Queen Darleen, haikuchukua muda mrefu Zuchu kumshirikisha Diamond katika nyimbo zake mbili zilizotoka kwa mpigo.
Nyimbo hizo ni Cheche (2020) na Litawachoma (2020) ambazo ndizo hasa zilimtangaza zaidi kimuziki, Zuchu alikuwa msanii wa kwanza sio kwa WCB Wasafi tu, bali Bongofleva nzima kuweza kutoa nyimbo mbili na Diamond kwa wakati mmoja na zote kufanya vizuri.

6. MBOSSO - BAIKOKO & KARIBU
Kufuatia kuvunjika kundi la Yamoto Band, Mbosso alijiunga na WCB Wasafi hapo Januari 2018. Kupitia albamu yake ya kwanza, Definition Of Love (2021) alimshirikisha Diamond katika nyimbo mbili, Baikoko na Karibu.
Haikuishia hapo, katika EP yake ya kwanza, Khan (2022) iliyochaguliwa kuwania tuzo za TMA 2022, Diamond akapewa nafasi tena kupitia wimbo ‘Yataniua’ ambao ulileta utata kwa madai umefafana na ule wa Asake wa Nigeria, Peace Be Unto You (2022).

7. CHID BENZI - MPAKA KUCHE & TUNAISHI NAO
Katika historia Diamond ndiye wa kwanza kumshirikisha Chid Benzi ambaye alisikika katika wimbo wake ‘Nalia Na Mengi’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Kamwambie (2010) ambayo ndio hasa ilimtoa kimuziki.
Baada ya kupitia changamoto za kimaisha, Chid Benzi alitaka kurudi kwa kushindo ndipo akampa shavu Diamond na AY katika wimbo wake, Mpaka Kuche (2014), na baada ya takribani miaka 10 wakatoa ngoma nyingine, Tunaishi Nao (2023).
8. RAYVANNY - MWANZA & TETEMA
Hadi sasa Rayvanny na Diamond ndio wasanii Bongofleva walioshirikiana zaidi kwa kipindi cha miaka minane iliyopita.
Rayvanny amemshirikisha Mondi katika nyimbo zake saba ambazo ni Mwanza (2018), Tetema (2019), Timua Vumbi (2019), Amaboko (2020), Woza (2020), Yaya (2023) na Nitongoze (2022) ulioshinda tuzo ya TMA 2022 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana.

9. LAVA LAVA - BADO SANA & TUNA KIKAO
Mei 2017 ndipo Lava Lava alitambulishwa WCB Wasafi akiwa ni msanii watano baada ya Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016) na Rich Mavoko (2016), huyu alipanda daraja maana mwanzo alikuwa katika bendi ya Diamond.
Ilimchukua Lava Lava muda mrefu hadi kufanya kazi na Diamond sababu walianza kutoa nyimbo za lebo kwanza, Zilipendwa (2017), Jibebe (2018) na Quarantine (2020), ila baadaye akapata kolabo ya kwanza na Mondi, Bado Sana (2021), kisha Tuna Kikao (2023).

10. JUX - SUGUA & ENJOY
Tangu akiwa na kundi la Wakacha, hakuna wimbo wa Jux uliofanya vizuri kama huu wa pili kumshirikisha Diamond, Enjoy (2023) ambao video yake ndio iliongoza Tanzania kutazamwa YouTube mwaka uliopita na hadi sasa ikiwa na ‘views’ milioni 67.

Jux alishafanya kazi na Mondi, ‘Sugua’ ya kwenye The Love Album 2019.