Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waimbaji 20 Bongo waliobadili majina yao

New Content Item (1)
New Content Item (1)

KUNA wasanii wengi wa Bongofleva waliobadili majina yao na wengine kuyafanyia marekebisho kidogo kwa lengo la kukuza chapa zao zaidi, hawa ni miongoni mwa wengi waliofanya hivyo.


1. Rapcha > Joh Makini

Kuanzia River Camp Soldiers, Good Music Family (GMF), Weusi hadi Viburi Flow, wengi walimfahamu kama ‘Joh Makini’ ila mwanzo alitumia jina la ‘Rapcha’ kama alivyoeleza katika wimbo wake, Bye Bye (2011) chini ya B’Hits.


2. Double Jay > Bwana Misosi

Alianza kwa kutumia jina la ‘Double Jay’, ni kabla ya wimbo wake, Nitoke Vipi (2003), ni kipindi akiwa msaidizi wa Professor Jay jukwaani ila baadaye akabadilisha na kuwa ‘Bwana Misosi’ hadi sasa.


3. Lil K > Young Killer

Kabla ya kukutana na Deey Classic, Duke Tachez wala Fid Q katika Fidstyle Friday na kabla kuibuka mshindi wa Fiesta Super Nyota (2012), alitambulika kama ‘Lil K’ lakini akabadili ikawa ‘Young Killer’ hadi leo.


4. Nikki Jay > Nikki Mbishi

Kabla hujamfahamu kupitia wimbo ‘Play Boy’ kutoka katika albamu yake, Sauti ya Jogoo (2011), alifahamika kama ‘Nikki Jay’ ila ukuaji wake kimuziki ukazaa jina la ‘Nikki Mbishi’ linalotumika sasa. 


5. Ney > Nay wa Mitego

Akirekodi Marimba Studio (1998) na Bongo Records (2001) alitumia jina la ‘Ney’ ila baada ya kuachia wimbo, Wamitego (2005) na kufanya vizuri ndipo zikazaliwa jina la ‘Ney wa Mitego’ liloboreshwa na kuwa Nay wa Mitego.


6. Chifu Rumanyika > Soggy Doggy

Tangu Bantu Pound Gangsters, kabla ya kukutana na Misanya Bingi wala DJ Boniluv, alijiita ‘Chifu Rumanyika’, jina alilolipambania hadi kutoa albamu, Niite Chifu Rumanyika (2005) ila la ‘Soggy Doggy’ likapendwa na wengi.


7. Dogo Baraka > Barakah The Prince

Kabla hajafahamiana na Kid Bwoy pale Tetemesha Records au Seven Mosha pale RockStar Africa, alitumia jina la ‘Dogo Baraka’ na baadaye ikawa ‘Barakah Da Prince’ ambalo aliliboresha tena na kuwa Barakah The Prince.


8. One > One The Incredible

Kuanzia Illmatix, Lunduno hadi Tamaduni Muzik alijiita ‘One’ ila baada ya kuachia ngoma ‘The Incredible’ iliyojumuishwa katika albamu yake, Soga za Mzawa (2012), ndipo likazaliwa jina la ‘One The Incredible’ linalotumika hadi leo. 


9. Sarah > Shaa

Hadi anashinda Coca-Cola Popstar (2004) na kuunda kundi laWakilisha alikuwa akitumia jina la ‘Sarah’ alilopewa na wazazi wake ila baadaye alikutana na Ngwea aliyempa jina la ‘Shaa’ ambalo yupo nalo.


10. Maromboso > Mbosso

Akiwa Yamoto Band alijulikana kama ‘Maromboso’ ila baada ya kusainiwa na WCB Wasafi (2018) akabadilishwa jina na kuwa ‘Mbosso’ kwa kile ilichoelezwa ni kuunda chapa yake upya.


11. Nigga Jay > Professa Jay

Hadi anajiunga na Hard Blasters Crew (HBC) na kukutana na Professor Ludigo alikuwa akijiita ‘Nigga Jay’ ila alipokutana na John Dilinga ‘DJ JD’ ndiye akampa jina la ‘Professor Jay’ ambalo limedumu hadi leo.


12. Saraphina > Phina

Hadi anashinda Bongo Star Search (BSS) 2018 na tuzo mbili za mwanzo za muziki Tanzania (TMA) 2021 alijulikana kama ‘Saraphina’ jina alilopewa na wazazi ila baadaye akalifupisha na kuwa ‘Phina’ hadi sasa.


13. Dogo Hamidu > Nyandu Tozzy

Akiwa na Dar Skendo chini ya Dudu Baya alijulikana kama ‘Dogo Hamidu’ ila baada ya kukua akabadili jina na kuwa ‘Nyandu Tozzy’ analotamba nalo hadi sasa nchini ya chapa yake, 26 Life.


14. 2Proud > Sugu

Rafiki yake kutoka Marekani alimpa jina la ‘2Proud’ kisha likafuata jina la ‘Mr. II’, jina la Sugu lilikuja kuanzia kwenye albamu yake nne, Nje ya Bongo (1999) na ya tano, Millennium (2000), ni baada ya watu kuona anazidi kukomaa na muziki.


15. Abby > Abigail Chams

Bongofleva ilimpokea akitumia jina la ‘Abby Chams’ ila kufuatia kusainiwa RockStar Africa na Sony Music Africa akafanya mabadiliko madogo katika jina lake na kuwa ‘Abigail Chams’ hadi leo.


16. Nikki Makini > Nikki wa Pili

Mwanzo alijiita ‘Nikki Makini’ akifuata nyayo za kaka yake, Joh Makini ila baadaye akaja kubadilisha na kuwa ‘Nikki wa Pili’, ni kitu alichohoji Nikki Mbishi katika ngoma yake, Punch Line (2011).


17. Akili > 20 Percent 

Alianza muziki akitumia jina la ‘Akili’ ikiwa ni ufupisho wa majina yake ya kuzaliwa (Abbas Kinzasa Lipakale), lakini baadaye akalibadilisha na kuja na ‘20 Percent’ analotumia sasa.


18. P The MC > P Mawenge

Tangu Tamaduni Muzik, Miraba Minne, Sisi Sio Kundi (SSK) na hadi anatoa albamu yake, Mwingi wa Habari (2013) alikuwa akitumia jina la ‘P The MC’ ila akabadilisha na kuwa ‘P Mawenge’ ambalo yupo nalo.


19. AT > BEY

Hadi anavuma na kundi la Offside Trick alitumia jina la ‘AT’ lakini mwaka uliopita alibadili jina hilo na kuwa ‘BEY’ kwa madai anataka kufika kimataifa na jina la AT limefafana na msanii mwingine wa nje hivyo itakuwa kikwazo. 


20. Lil Sama > Mr. Blue

Aliingia katika Bongofleva na jina la Lil Sama ila baada ya kuachia wimbo, Blue (2003) na kupata mapokezi makubwa kwa mashabiki ndipo wakampa jina la ‘Mr. Blue’ ambalo alilipokea kwa mikono miwili, huku likipambwa na a.k.a ya Byser.