Video kama ya Roma,Stamina yachaguliwa Grammy

Video kama ya Roma,Stamina yachaguliwa Grammy

Video ya wimbo wa Life is Good wa wasanii wa Marekani, Drake na Future imechaguliwa kuingia kwenye kipengele cha Video Bora ya mwaka katika tuzo za Grammy 2021 zilizotangazwa usiku wa kuamkia leo Novemba 25.

Sasa utamu zaidi ni kwamba, video hiyo inafanana kinoma na video ya wimbo wa Kijiwe Nongwa ya kundi la Rostam linaloundwa na wasanii,Roma Mkatoliki na Stamina kutoka Bongo, na zaidi ni kwamba video ya Rostam ndio iliyotangulia kutoka.

Katika video hiyo, Roma na Stamina wameigiza kama wazoa takataka wakiwa kwenye gari la kubebea taka huku wakipiga stori kwa kuimba. Wakati kwenye video ya Drake na Future pia wameigiza wakifanya kazi mbalimbali ikiwemo ya kuzoa taka, huku aina ya upigwaji picha za video hizo pia unarandana.

Video ya Life is Good ilipotoka Januari 9 mwaka huu, msanii Roma aliandika kupitia akaunti yake ya Twitter kwamba laiti kama video ya Future na Drake ingetangulia kutoka kabla ya Rostam, ni wazi kwamba mashabiki wa Tanzania wangewashambulia kwamba wameiga.

Majina ya Washiriki wa tuzo hizo yalitajwa usiku wa Novemba 24, huku kwa Afrika ikiwakilishwa na msanii mmoja tu, Burna Boy ambaye ameingia kipengele cha Albamu Bora ya Mwaka (Nje ya Marekani) kupitia albamu yake ya Twice As Tall iliyotoka Agosti mwaka huu.

Aidha katika tuzo hizo, msanii Beyonce ametajwa kushiriki kwenye vipengele vingi zaidi akiwa anawania tuzo katika vipengele tisa.

By KELVIN KAGAMBO