Bi Star humwambii kitu kwa Simba na singeli

Muktasari:
- Katika harakati zake za kutoka kisanaa alianza kuigiza 1998 kwa kujitolea na ilipofika 2000 alianza kuonekana kwenye runinga kwa malipo ya Sh20,000 kwa mwaka.
Usemi wa mvumilivu hula mbivu ndiyo umemkuta mwigizaji mkongwe Shamila Ndwangila maarufu kama Bi Star ambaye hivi sasa anakula matunda ya kazi yake.
Katika harakati zake za kutoka kisanaa alianza kuigiza 1998 kwa kujitolea na ilipofika 2000 alianza kuonekana kwenye runinga kwa malipo ya Sh20,000 kwa mwaka.
Bi Star ambaye kwa sasa anavuma kwenye Tamthilia ya Kombolela inayoonyeshwa Azam Tv akitumia jina la Mwadawa anaigiza kama mtu mwenye ulemavu wa miguu anayetumia baiskeli ya miguu mitatu kutembelea na mtu mwenye asiyekuwa na heshima kwa wazazi na watu wengine.
Mwanaspoti lilifunga safari hadi Temeke Mtoni kwa Aziz Ally, Dar es Salaam ilipo kambi ya kundi la Kombolela na kupiga naye stori ndani ya Dakika Tano.

Kati ya sanaa na mume nini kilianza kwako?
"Nilianza kuwa na mume halafu sanaa ikafuata, na mume wangu ndiyo chanzo mimi kuingia kwenye sanaa maana alikuwa katibu kwenye kikundi cha sanaa cha Tandale Arts Group, mimi nilikuwa mwandishi wa majina ya watu ambao waliokuwa wanakuja kujiunga kwenye kikundi hicho."
Kuna mafaniko ya sanaa umeyapata?
"Kwanza nashukuru wWatanzania wamenipokea vizuri katika kazi zangu za sanaa na sipati changamoto zozote zile zaidi ya mashabiki wakiniona huwa wanafurahi. Hii ni moja ya mafanikio. Kitu kingine nina mashamba, nyumba, na hata mambo mengine yanakuwa rahisi kufanya au kuyapata kupitia uigizaji."
Kwenye Kombolela (unachocheza) ndio uhalisia wako?
"Hapana ule ni mwongozo wa Tamthilia ya Kombolela ambao unanitaka niwe vile, ila kiuhalisia siko vile. Mimi ni mtu mkimya sana na wala sio muongeaji, ila kwa jinsi navyoigiza kuna baadhi ya watu ukikutana nao wanakutibua wakidhani utawacharukia kama ilivyo kwenye tamthilia. Lakini wakiona upo kimya wanabakia kukushangaa tu, kumbe tunachofanya kipo kwa Watanzania ni uhalisia wa watu na vitu hivyo vipo na tunaishi navyo."

Mbali na kuigiza majanga, utata, kuna nafasi nyingine ulishawahi kucheza toka uanze sanaa?
"Nafasi ambayo sijawahi kucheza ni ya kishua, kibosibosi yaani huenda waongozaji huwa wanaona nafiti kwenye tamhilia zao wanazoandaa na natamani kucheza nafasi hiyo ili niwateke na wale wa kishua maana kila nafasi najiamini naimudu tofauti ni stori ila kazi zangu zote nacheza vizuri, Uswahilini na sehemu zingine nilizoonekana nimecheza."
Tamthilia ipi iliyokutambulisha kwa mashabiki?
"Tamthilia iliyonitoa ni Fukoto wakati niko kundi la Kaole (Sanaa) nilicheza mke mdogo wa Muhogo Mchungu na huyu ndio moja kati ya watu walionishika mkono na kuniambia nina kipaji kikubwa na alinitabiria kuwa nitafika mbali nakuwa karibu naye na kucheza nafasi za pamoja kama mke na mume. Ndipo watu walipoanza kuvumisha kuwa tuna mahusiano na alitaka kunioa, lakini sio kweli. Halafu kipindi kile watu walikuwa hawana ufahamu wa watu wanapoigiza kuwa ni maigizo, ila sasa hivi Watanzania huwezi kuwaongopea kuwa ukicheza na mtu ndio mme wako kwelikweli. Wengi wanajua ni hadithi kuwa ukicheza naye basi inaisha."

Kuna mtoto amerithi kazi yako ya sanaa?
"Mtoto wa kurithi bado hakuna, ila watoto wangu wote wameonja kamera kwa kuwa walikuwa wakitumika sana pindi wakiwa wadogo."
Wewe ni shabiki wa timu gani na unapendelea muziki upi?
"Mimi ni shabiki mkubwa sana wa Simba. Mume wangu na watoto wangu wawili ni mashabiki wa Yanga, lakini mimi naipenda Simba na ni mpenzi wa muziki wa singeli sana kuliko kitu kingine. Pia napenda sana kuimba".
Una mtoto anaimba Singeli?
"Ndio yupo ni mtoto wa mdogo wangu wa tatu wa kiume... sio wa kumzaa mimi, ila ndio mwanangu huyo."

Unaepuka vipi na skendo za mtaani?
"Skendo haziepukiki, ila unakuwa tu unafanya kwa tahadhali maana inaweza kukukuta skendo yoyote ya kweli au kusingiziwa, hivyo unapozungumzia skendo mtu anaweza kukukochoza kumbe wewe uko tofauti na kwenye tv na ukishajitambua ni koo cha jamii basi lazima ujilinde".
Unaizungumziaje sanaa ya sasa?
"Bongo movie ya sasa watu wanachapaka kazi. Tumekuwa tuna afadhali tofauti na zamani tulikuwa tunachapa kazi malipo hakuna na kipindi hicho wasanii walikuwa wakipita kwenye vikundi ambavyo vilikuwa kama shule... ukweli kuna urahisi sana kwa sasa."
Wewe ni mtoto wa ngapi kuzaliwa?
"Mimi ni mtoto wa kwanza nilizaliwa peke yangu kwa mama yangu, ila nina ndugu upande wa baba wako wawili na upande wa mama mwingine wapo watatu, hivyo kwa baba tupo watano. Niko kwenye ndoa muda mrefu nina watoto watatu wa kike na mjukuu mmoja."

Asili yako ni wapi?
"Hapa ndio watu wengi hawajui huwa wanadhani mimi ni mtu wa pwani na wengine wanadhani ni wa Tanga, ila ni Mngoni wa Ruvuma yaani baba na mama wote ni Wangoni, na kama unafahamu Wangoni tuna miiko wengi huwa wanakuwa na majina ya kinyumbani ndio maana unakuta wengine wana majina ya wanyama, ila mimi ni Fusi na napiga kilugha kama kawaida."