Unajua Rayvanny ni mjanja mjanja sana!

Muktasari:
- Rayvanny alishinda kupitia wimbo wake, Kitu Kizito (2023) akimshirikisha DJ Misso Misondo, ni wimbo uliorekodi muda mfupi tu baada ya DJ Misso Misondo na Wazee wa Makoti kuanza kuvuma.
STAA wa Bongo Fleva kutoka Next Level Music (NLM), Rayvanny ameshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023 katika kipengele cha Wimbo Bora wa Singeli ikiwa ni matokeo ya ujanja ujanja wake katika muziki.
Rayvanny alishinda kupitia wimbo wake, Kitu Kizito (2023) akimshirikisha DJ Misso Misondo, ni wimbo uliorekodi muda mfupi tu baada ya DJ Misso Misondo na Wazee wa Makoti kuanza kuvuma.
Huo ulikuwa mwendelezo wa Rayvanny kupita na matukio yanayovuma, mfano kipindi Dudu Baya anateka mazungumzo mitandaoni na harakati zake, Rayvanny mara moja akafanya naye wimbo, Konki (2018).
Utakumbuka mapema mwaka huu Rayvanny aliwekwa kitimoto na idadi kubwa ya mashabiki mtandaoni waliodai amekuwa mwepesi wa kudandia nyimbo za wasanii wenzake zinazofanya vizuri kuliko kuwekeza ubunifu katika kazi zake.

Kelele hizo zilizidi baada ya kuachia remix ya wimbo wa Dayoo, Huu Mwaka (2024) ambao ulikuwa ufanya vizuri, wengi wanaamini Rayvanny anatembelea nyota za wasanii wenzake maana kila wimbo au tukio linaloibuka na kubamba basi atapita nalo.
Anachofanya staa huyo ni anaposikia wimbo wa msanii fulani unafanya vizuri basi atamuomba afanye remix na ikibidi washirikiane, hadi sasa mbinu hiyo imempa Rayvanny kolabo zaidi ya 10 za ndani na nje.
Mpango huo upo kibiashara zaidi maana ndiye anagharimikia kila kitu ila kazi husika lazima iwepo kwenye majukwaa yake ya kidigitali hasa YouTube na hapo ndipo wakosoaji wake wanaona Rayvanny hana mpango wa kusaidia kama anavyodai.
Mavokali & Rayvanny
Muda mfupi baada ya Mavokali kuachia wimbo wake, Mapopo Remix (2022) ulifanya vizuri sana kimataifa na hata kuzizidi nyimbo nyingi za wasanii wakubwa Bongo na punde tu Rayvanny akafanya remix yake.

Kama ni upepo au kutembelea nyota basi hapa Rayvanny alifanikiwa kwa asilimia 100, ila Mavokali akawa majanja kwa kuweka remix ya wimbo huo katika chaneli yake ya YouTube tofauti na wasanii wenzake na tayari ina ‘views’ milioni 16.
Rosa Ree & Rayvanny
Rapa Rosa Reee alipoachia wimbo wake, Sukuma Ndinga (2020) na kuanza kufanya vizuri, moja kwa moja Rayvanny alimuomba remix, Rosa alikubali na hadi sasa video ya wimbo huo ambayo ipo YouTube kwenye chaneli ya Rayvanny ina ‘views’ milioni 2.3.
Rosa Ree ambaye ni mshindi wa tuzo tano katika vipengele vya Hip Hop alisema hatua hiyo ni makubaliano ya menejimenti yake na ile ya Rayvanny na kuwa kazi hiyo inazinufaisha pande zote mbili.
Lil Jay Bingerack & Rayvanny
Tunaenda hadi Afrika Magharibi na kukutana na Lil Jay Bingerack kutokea Ivory Coast ambaye mwaka uliopita aliachia wimbo wake, Hi Hi Hi (2023) na kufanya vizuri baadhi ya maeneo Afrika.

Basi Rayvanny akaona hiyo ni nafasi ya yeye kupenya nchini Ivory Coast na Afrika Magharibi kwa jumla, basi yeye na Lil Jay Bingerack wakatoa remix ya wimbo huo ambao video yake hadi sasa ina ‘views’ zaidi ya milioni 1.3 YouTube.
Chino Kidd & Rayvanny - Kibela Remix
Kati ya wasanii Bongo ambao nyota zao ziling’aa mwaka uliopita, basi ni Chino Kidd, kila ngoma aliyotoa ilipata mapokezi mazuri, hakuna ubishi wimbo wake, Kibela (2023) akiwashirikisha S2kizzy na Mfana Kah Gogo ilipendwa na wengi.
Kama kawaida Rayvanny akaona hiyo ni fursa kwake, ni kingine zaidi ya kufanya remix ya wimbo na kuwapa shavu wote waliokuwepo mwanzo, huku video akiiweka katika chaneli yake na hadi sasa ina ‘views’ 2.3 milioni huko YouTube.

Guchi & Rayvanny
Staa wa Nigeria, Guchi tayari alikuwa imeishika Afrika na wimbo wake, Jennifer (2021), Rayvanny alipousikika akavutiwa nao, basi akamgharimia kila kitu Guchi akaja nchini na kurekodi remix yake pamoja na kushuti video.
Video yake tayari ina ‘views’ milioni 24 ikiwa ni video ya 12 kwa Rayvanny kutazamwa zaidi YouTube kwa muda wote, huku ikiwa kolabo yake ya pili ya kimataifa iliyofanya vizuri baada ya ‘Teamo’ (2020) akimshirikisha Messias Maricoa kutokea Ureno.