Ukubwa wa Nahreel nje ya Navy Kenzo

NDANI ya Kundi la Navy Kenzo akiwa na mwenzake Aika, Nahreel anasimama kama mwimbaji, akiwa studio kwake The Industry anasimama kama Prodyuza ambaye ametengeneza nyimbo nyingi kali za wasanii wengi wa Bongo Fleva.
Ameshiriki kwa kiasi kikubwa kutengeneza nyimbo kibao za albamu tatu za Navy Kenzo, AIM (Above Inna Minute) (2016), Story Of The African Mob (2020) na Most People Want This (2023). Huyu ndiye Nahreel.
1. Mwaka 2003 alipewa jina la ‘Nah Lily’ na rafiki yake, Bowaz baada ya kuonyesha uwezo wa kupiga kinanda alichonunuliwa na baba yake ambaye alitaka awe mpiga kinanda kanisani, baadaye aliboresha jina hilo na kuitwa, Nahreel.
2.Kama Kawaa Records ndio studio ya kwanza kwa Nahreel kufanya kazi na nafasi hiyo alipewa na Prodyuza Yudi, ila Prodyuza G Solo ndiye alimsimamia zaidi na kumkutanisha na wasanii kama, Joh Makini kwa mara ya kwanza.
3. Mwaka 2010 ndipo wimbo wa kwanza aliotengeneza Nahreel ulishinda tuzo ya muziki Tanzania (TMA), huu ni wimbo wa Joh Makini, Stimu Zimelipiwa (2009) alioutengeneza akiwa Chuo India na ulishinda KTMA kama Wimbo Bora wa Hip Hop.
Hadi sasa akiwa kama Prodyuza, Nahreel amefanya kazi na wasanii kama Roma, Vanessa Mdee, Joh Makini, Diamond Platnumz, Weusi, Mwana FA, Nikki wa Pili, AY, Izzo Biznes, G Nako n.k.

4.Kabla ya kufungua studio yake binafsi, The Industry, Nahreel alifanya kazi katika studio mbalimbali Zikiwemo Kama Kawa Records, Home Time Records na Switch Studio ya Quick Rocka.
5.Baada ya Nahreel kuondoka Switch, nafasi yake ikachukuliwa na Luffa, naye alipohamia Wanene Studio, nafasi yake ikachukuliwa na S2kizzy, naye alipoondoka na kwenda kufungua studio yake, Pluto Repulic, nafasi yake ikachukuliwa na Ammy Wave.
6.Nahreel katika studio yake ya The Industry alitumia dakika 10 tu kutengeneza mdondo wa wimbo wa Joh Makini, Don’t Bother (2015) akimshirikisha AKA wa Afrika Kusini ambaye alifariki dunia baada ya kupigwa risasi Februari mwaka jana.

7.Hivi wajua Nahreel ni miongoni mwa maprodyuza watatu walioshiriki kutengeneza mdundo wa wimbo wa AY, Zigo (2016)? Wengine ni Marco Chali kutoka MJ Records na Hermy B wa B’Hits.
Hiyo ni sawa na wimbo wa staa wa Next Level Music (NLM), Rayvanny, Chombo (2018) ambao hadi kukamilika kwake umepita kwenye mikono ya watayarishaji watatu, S2kizzy, Rash Don na Laizer.
8.Nahreel ndiye ametengeneza wimbo wa Diamond Platnumz, Nana (2015) akimshirikisha Mr. Flavour wa Nigeria ingawa utambulisho wake (sign tune) kama Prodyuza mwanzoni mwa wimbo huo unadaiwa kuondolewa na WCB Wasafi.
9.Huyu ndiye Prodyuza wa kwanza Afrika kuingiza nyimbo tano katika chati ya African Chart ya MTV, miongoni mwa nyimbo alizotengeneza Nahreel ambazo ziliingia katika chati hizo ni Looking For You (2015) ft. Joh Makini.
10.Nahreel ana shahada ya Computer Science aliyoipata katika Chuo cha Punjab College, India, hii ni taaluma ambayo wasanii kama Roma na Jux ambao wamewahi kufanya nao kazi pia wanayo kutoka vyuo vya UDSM na Guangdong China.