TUONGEE KISHKAJI: Ya wasanii wa zamani, yatawakuta wapya

LICHA ya kwamba Lamata Leah Mwendamseke unafanya kazi kubwa ya kuhakikisha Bongo Movie bado inaongelewa kupitia tamthiliya yako ya Jua Kali lakini na wewe jiandae kukutwa na yaliyomkuta Vincent Kigosi ‘Ray’.

Na sio yeye tu, na hata wewe Amil Shivji jiandae, licha ya kwamba unatengeneza filamu zinazowakilisha Tanzania kimataifa, mfano, filamu ya kwanza ya Tanzania kuonyeshwa kwenye tamasha la filamu la kimataifa la Tiff ni filamu yako ya Vuta N’vute lakini na wewe jiandae, yatakukuta kama yanayowakuta waliokutangulia.

Diamond ndiyo kabisa, ujipange kwa sababu naona kabisa ipo siku utapitia anayopitia Mr. Nice licha ya kwamba umetumia zaidi ya miaka saba kuwa bendera ya muziki wa Bongofleva nje ya Tanzania.

Young Lunya utapitishwa kwenye mateso anayopitia Fid Q subiri siku yako inakuja.

Na nasema hivi sio kwamba nawatisha, hapana. Nasema hivi kwa sababu nawafahamu vizuri mashabiki wa Kitanzania hawana heshima hata kidogo kwa watu waliofanya makubwa kwenye kiwanda cha burudani katika taifa hili.

Tungekuwa tunaheshima leo tusingeshuhudia watu wanamtukana Khadija Kopa kwa sababu yoyote ile kwa sababu wanatafuta umaarufu, iwe kwa sababu ni maarufu na wanataka kuendelea kuwa maarufu kwa kutukana watu. Iwe kwa sababu mtoto wa Khadija anafanya ‘dhambi’ sana au kwa sababu yoyote ile.

Mtu unaanzaje kumtusi Khadija Kopa mmoja wa wasanii ambao siogopi kusema ni msingi wa muziki huu wa kizazi kipya. Niambie bila Khadija na Nasma Khamis Kidogo kukinukisha kipindi kile tungewapata wapi kina Isha Mashauzi? Tungeipata wapi Jahazi Morden Taarab?

Na bila kina Isha Mashauzi na Jahazi Modern Taarab ya Mzee Yusufu tungepata wapata wapi watia ladha kina Msaga Sumu, watu ambao walikuwa wanaimba kwenye shughuli za mtaani kwa kutumia midundo ya taarabu.

Na bila watia ladha tungewapata wapi kina Dula Makabila, Mzee wa Bwax na muziki wao wa singeli ambao kila siku unazidi kukua na kukua. Ukizingatia yote haya unaanzaje kumkosea heshima Khadija Kopa.

Au tuseme ukijua uzito wa Juma Nature Kiroboto kwenye hii gemu unaanzaje kumtukana akisema amekataa kutumbuiza kwenye shoo ya Wasafi Festival? Sawa, labda ni kweli sasa hivi hana mashiko sana, lakini mwenyewe haamini hivyo. Haamini kwamba amekosa mashiko kiasi kwamba anaweza kupiga shoo kwa kiasi flani kidogo cha fedha, kwanini umtukane?

Yule mzee amefanya mambo mengi makubwa ya kihistoria kwenye hiki kiwanda cha burudani hapa Tanzania. Kiroboto ame-inspire madogo wengi sana Tanzani. Bila Juma Nature tusingekuwa na TMK Wanaume, TMK Halisi wala TMK yoyote ile.

Bila TMK tusingewapata Mkubwa na Wanawe wala Yamoto Band na hapo bado hatujataja wasanii wengine nje ya Temeke ambao Juma Nature kwao ni kama ‘godfather.’

Mashabiki wa Tanzania hatuna staha, hatujui namna ya kuwaheshimisha watu waliofanya makubwa na kujenga msingi wa hiki kiwanda. Na tunafanya dharau hizi tukiongozwa na watu maarufu kwenye mitandao ya kijamii wanaofanya dharau kwa kigezo cha kuita content.