TUONGEE KISHKAJI: Wasanii wakongwe wanawaonea wivu wapya?

BAADA tu ya makala niliyoandika wiki iliyopita kuchapishwa nikakutana na video ya Afande Sele akimuongelea Young Lunya kwa namna ya kipekee. Nikukumbushe tu kwenye makala niliyoandika wiki iliyopita nilizungumzia jinsi wasanii wa kizazi hiki wanavyopaswa kujiandaa kuchukuliwa poa kama ambavyo wakongwe kama vile Juma Nature, Afande Sele, Mr Nice na wengineo wanavyochukuliwa poa kwa sasa.

Iko hivi. Kuna video moja inamuonyesha Young Lunya akihojiwa. Katika mahojiano hayo Lunya aliulizwa swali ambalo lilimfanya ajibu “mimi huwa sirudii boksa.” Sasa kwenye video ya Afande Sele alitoa maoni yake kuhusu video ya Lunya kutokurudia boksa. Akaongea mengi lakini moja ya alichosema ilikuwa ni hivi, nanukuu: “Wa kiume, lakini anasema kwamba yeye akivaa boksa harudii mara mbili. Sasa nikasema huyu ni mtoto wa kiume kwanini harudii boksa? Kumradhi au ana bawasiri? Kama hana ana matatizo gani yanayomfanya asirudie boksa? Angekuwa binti kweli, lakini mtoto wa kiume unasema hurudii boksa wewe hip hop kweli? Sisi wenzie tunavaa boksa mwaka mzima babuuu.”

Lakini sio Afande pekee nimewahi pia kusikia wasanii wengine wakongwe wakiongelea wasanii wa kizazi hiki kwa namna fulani ambayo haisharii amani. Nimewahi kusikia Q Chief akimuongelea Diamond, Mr Nice akimuongelea Diamond, Dudu Baya akimnanga Shetta na zaidi. Mpaka inanipa wasiwasi na kunifanya nijiulize au pengine wasanii hawa wakongwe wanadhani wabaya wao ni wasanii wa kizazi hiki?

Nasema hivyo kwa sababu mtaani mimi na washkaji zangu tunaamini wasanii wa zamani walifanya muziki mkali, lakini hakukuwa na maokoto ukilinganisha na sasa hivi. Sasa hivi msanii anaweza kuja siku mbili tatu akazoa maokoto kama yote.

Sasa ukiangalia hali za kifedha za wasanii wakongwe pengine wanaona kama wasanii wapya wanafaidika kwa kutumia barabara ambazo wakongwe walizichonga. Pengine kwa sababu hiyo wanaanza kuwamaindi madogo. Naomba nikumbushe kwamba sijasema kama wasanii wakongwe wana wivu, nimesema pengine wana wivu. Ninaweza kuwa sahihi au naweza kuwa nakosea. Lakini mwisho wa yote, jambo ambalo nataka kuwakumbusha wasanii wa aina zote mbili- wa kisasa na wakongwe ni kwamba wasipigane wenyewe kwa wenyewe, wasitengeneze uadui kati yao. Wasanii wakongwe hawapaswi kuona wasanii wa kizazi hiki kama wabaya wao na  wa kizazi hiki pia wasione wakongwe kama wabaya wao.

Wabaya wao ni mashabiki kama nilivyozungumza kwenye makala ya wiki iliyopita. Mashabiki ndio wanaosababisha wanawadharau wasanii wakongwe na kuwafanya wajione kama vile mchango walioutoa kwenye tasnia hauthaminiwi. Mashabiki ndiyo wanafanya wasanii wakongwe wajione si lolote, si chochote matokeo yake wanaanza kuwarushia madongo wasanii wa kisasa wakidhani ndiyo maadui zao.