TUONGEE KISHKAJI: Wakenya wapewe namba ya Coy Mzungu, wakachekeshe
Muktasari:
- Hata hivyo, stori yenyewe ina sura mbili, sura ya kwanza tunaipata kutoka kwa Willy Paul na katika shoo hiyo walikuwepo wasanii wengi kwenye listi ya kuperform akiwemo Diamond na Willy Paul.
MWANZONI mwa wiki hii, stori iliyotrend ilikuwa ni msanii Willy Paul a.k.a Willy Pozze wa Kenya kudaiwa kugombana na Diamond Platnumz katika shoo iliyofanyika huko Kenya.
Hata hivyo, stori yenyewe ina sura mbili, sura ya kwanza tunaipata kutoka kwa Willy Paul na katika shoo hiyo walikuwepo wasanii wengi kwenye listi ya kuperform akiwemo Diamond na Willy Paul.
Lakini ilipofika zamu yake alishangaa kuona Diamond na timu yake wanamzuia kupanda jukwaani, eti wanataka Diamond atangulie kabla yake. Hapo ndipo ugomvi ulipotokea.
Wakati kwa mujibu wa Diamond, anasema alichokisema Willy ni uongo. Yeye hakushuka hata kwenye gari lake. Alikuwa anasubiri muda ufike, aitwe akatumbuize. Willy Paul alikuwa anagombana na watu wengine lakini aliamua kugeuza stori ili kutumia kama kiki.
Baadae mchekeshaji wa Kenya, Erick Omondi akaandika barua ndefu katika Instagram yake akilaani kilichomtokea WIlly Paul huku aking’aka anataka wasanii Wakenya wapewe heshima sawa na wasanii wa nje. Kwani wa nje wakienda Kenya wanathaminiwa sana, huku wale wa Kenya wakidharauliwa.
Omondi alitaja vitu kama vile wasanii wa nje kupewa masofa meupe backstage, kupewa pombe na vinywaji wanavyotaka na kadhalika. Mwisho akawa anapush agenda ya, inabidi kwa Kenya sanaa ya Wakenya ipewe upendeleo zaidi, kama ni muziki, basi asilimia 75 ya ngoma zinazochezwa klabu na katika vyombo vya habari ziwe ni za kikenya.
Kusema ukweli naelewa anachokisema Omondi na kiu yake ya kuona wasanii wa Kenya wanapewa thamani. Lakini kutamani kuona sanaa yao inapewa kipaumbele kabla ya sanaa za wasanii wageni. Hata hapa Bongo, wasanii wengi wamekuwa wakilalamikia michezo ya kituruki inawapoteza na kuwanyima fursa ya michezo yao kuonyeshwa.
Hata hivyo, uwasilishaji wa Omondi umekaa kidalali sana na unaonyesha wazi anachokitaka sio anachokisema.
Inaonyesha pengine Omondi anachikitaka sio wasanii wa Kenya wapewe kipaumbele, bali anataka historia imkumbuke kama mtu aliyepambania sanaa ya Kenya kupewa kipaumbele.
Kwa sababu huwezi kutaka msanii kama Diamond, aje nchini kwako halafu apewe thamani moja na wasanii wa kawaida kama Willy Paul.
Kama kweli Omondi angetaka hilo liwezekane, asingeanza kwenye kuomba masofa ya kukaa, masofa kitu gani bwana, angeanza kuomba Willy Paul alipwe sawa na Diamond.
Kwa sababu kama mwenye shoo tu anamlipa Willy Paul chini ya kiasi anachomlipa Diamond, hiyo inatosha kuonyesha wazi ni msanii gani ana thamani zaidi.
Anachokisema Omondi ni kama vile uende pale Al Nassr, halafu utake kila mchezaji alipwe sawa na Cristano Ronaldo kwa sababu tu mpira ni mchezo wa timu eti kwa sababu timu ikipata ushindi ni jitihada za timu nzima.
Haiwezi kuwa hivyo kamwe, Ronaldo ana thamani zaidi ya wachezaji wengine na atalipwa zaidi na kifurushi chake kitakuwa tofauti kwenye nyanja zote.
Kwa kifupi hakuna njia fupi ya mafanikio. Kama Willy Paul na msanii yeyote anataka kulipwa zaidi ya wasanii Watanzania, inabidi apambane awe sawa au juu zaidi ya wasanii wa Tanzania. Mbali na hapo, haki anayopambania ni kama kuchekesha watu.