TUONGEE KISHKAJI: Mitandao inavyogawa koneksheni kwa upendeleo

MITANDAO ni mizuri lakini kuna muda naona inazingua kwa jinsi inavyowanyima baadhi ya watu koneksheni. Siongelei koneksheni hiyo, naongelea koneksheni koneksheni, utanielewa vizuri.

Mwaka ule, wakati Ben Pol anatoka alipata masikio ya watu wengi sana. Alikuja na wimbo wake mmoja mkali unaitwa Nikikupata, mashabiki wakaukubali balaa, walikubali mashairi, walikubali sauti ya jamaa, wakaikubali video, wakaupenda wimbo na kuanzia hapo koneksheni ya Ben Pol na mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva ikatengenezwa. Akawa kila akitoa wimbo watu wanaukubali, koneksheni hiyo.

Halafu unakumbuka ngoma yenyewe mara ya kwanza tuliisikia wapi? Ilikuwa kwenye stesheni za redio, sio Spotify, Youtube, Boomplay wala Apple Music.

Zamani kibongobongo hakuna aliyekuwa anasikiliza Bongo Fleva huko kwenye majukwaa ya kusikiliza muziki, ni TV na redio kwa kwenda mbele.

Lakini siku hizi nani bado anasikiliza muziki kwenye redio? Na sio kwamba redio hazisikilizwi, hapana, lakini ni watu wachache wanaenda kusikiliza redio kwa ajili ya kusikiliza muziki.

Kila mtu ana uwezo wa kusikiliza muziki anaotaka muda wowote mahali popote. Kuna mitandao kibao ya kuuza na kusikiliza muziki na bado kuna washikaji wa huku mtaani tunaoweka ngoma kwenye memory card na flash.

Sasa kwa nini niende nikasikilize redio ambayo DJ anaamua kunipigia wimbo anaoutaka yeye wakati naweza kuwa DJ wangu mwenyewe na nikasikiliza muziki ninaoutaka mwenyewe muda wowote?

Ndiyo kuna sehemu niliona wameendika “uvivu ni kupiga simu redioni kuomba uchezewe wimbo fulani.”

Sasa ishu iliyoletwa na mitandao, ambayo inanifanya niichukie ni, kupata nafasi ya kusikilizwa kwenye mitandao ni ngumu sana kuliko kwenye redio.

Mameneja na watu wanaosimamia wasanii wanajua vizuri kuhusu hili, msanii mpya akitoa wimbo mkali akiweka Youtube, ni ngumu kupata wasikilizaji kwa sababu watu hawamjui, watu wanasikiliza wasanii wakubwa wanaowajua. Na hiyo inatengeneza ugumu sana kwa chipukizi kutoboa.

Nakumbuka mwaka huu tu Tanzania imepata wasanii wapya wa Bongo Fleva ambao kidogo walihit wasiozidi watano. Nusu kati yao wanatoka mikononi mwa watu wale wale wenye nguvu za mitandao. Wakati zamani, enzi za redio, ndani ya mwaka mmoja mnaweza mkawa na wasanii hata 10 wapya wanaohit.

Ingawa inasemwa intaneti imesaidia kupunguza miyeyusho hapa kati, ile miyeyusho ya unapeleka ngoma redioni DJ anakuomba kitu kidogo, kwamba sasa hivi unaweza kupandisha tu wimbo wako Youtube watu wakasikiliza.

Lakini tatizo ni kupata hao watu wa kusikiliza kwa sababu wasikilizaji wote wanasikiliza wasanii wakubwa ambao tayari wana nguvu ya kimtandao. Kwa namna hii naona kama intaneti na mitandao inawanyima wasanii wachanga wenye vipaji koneksheni na mashabiki.