TUONGEE KISHKAJI: Maharamia walivyoubeba muziki Afrika

New Content Item (1)

NATAZAMA mahojiano ya Ruger, msanii wa Nigeria aliyeimba wimbo wa Asiwaju na nyingine nyingi kali. Mtangazaji anamuuliza unafahamu kwamba Kenya kuna mtu anafanana nawe kimuonekano, hivyo hupanda jukwaani akiwa amevaa kificha jicho kama wewe, amepaka rangi nywele zake kama wewe na huimba ngoma zako akijifanya ni wewe, na watu hulipa pesa kumtazama wakidhani ni Ruger? Ruger anajibu, “Ndio, nafahamu.”

Swali lililofuata la mtangazaji ni “Unafanyaje? Unamchukulia hatua!”

Ruger anasema; “Hatua? Hatua za nini? Nafurahia kila anachokifanya. Anapambana kutafuta mkate wake, kwanini nimchukulie hatua? Naamini kwamba, watu wanaolipa pesa kumtazama wanatambua kwamba yeye sio Ruger halisi, ni mtu ambaye ametokea kufanana na Ruger, hivyo ameigeuza kama fursa ya kupata chakula, hivyo muache braza atafute chakula.”

“Anachokifanya hakinipungizii chochote kwa sababu pengine sehemu anazotumbuiza ni sehemu ambazo sitawahi kufika. Hivyo kwa yeye kuwa huko ni kama vile timu yangu ya matangazo imeweka bango langu huko. Kwa sababu anapopanda jukwaani huimba nyimbo za nani? Za kwangu. Kwa hiyo watu watasikia ngoma zangu kutoka kwake, watanipenda nami nitaendelea kutengeneza mashabiki hata sehemu siwezi kufika.”

Anachokisema Ruger ndiyo ‘mentality’ iliyosaidia kiwanda cha muziki sehemu nyingi duniani hususani nchi za Afrika. Kuna kipindi vitendo vya uharamia wa kazi sana hususani muziki ulikuwa mkubwa sana. Wasanii walikuwa wanateseka sana kupata faida kupitia kazi zao, kwa sababu msanii anaachia albamu leo, kesho anakuta albamu feki iko mitaani, watu wananua bei nusu ya ile orijino. Matokeo yake wasanii hawaambulii cha maana.

Mambo yamekwenda hivyo hadi teknolojia ilipokuwa, majukwaa ya kusikiliza na kutazama muziki kama vile Youtube, Dizzer, Boomplay na mengine yalipoanza kuwa mengi na rahisi kufika. Ndipo wasanii wakagundua njia nyingine ya kuuza kazi zao ambayo kwa kiasi kikubwa iliondoa uhitaji wa watu kununua kazi feki.

Kwenye majukwaa ya kusikiliza muziki unasikiliza muziki bure kabisa. Sasa kwanini mtu ahangaike na kwenda kununa CD feki? Na ili kukomesha wasanii walikuwa wanagawa kazi zao bure kiasi kwamba leo hii imekuwa kawaida kuona Nandy anaachia albamu yake wazi Youtube kila mtu anasikiliza muda wowote, wakati wowote bila kulipia hata senti moja.

Msanii anafanya hivyo kwa sababu anajua, watu watasikiliza naye msanii atatengeneza mashabiki wengi kisha atachukua hiyo idadi kubwa ya mashabiki na kwenda kuitumia kama mtaji kwenye kupata madili ya vitu vingine kama matamasha, matangazo ya biashara na kadhalika. Kwa sababu licha ya kwamba wasanii wanapata pesa kupitia majukwaa ya kusikiliza muziki lakini ukweli ni kwamba sio pesa kubwa.

Kwahiyo ukitazama jinsi uharamia ulivyokuza biashara ya muziki unaweza ukasema muda mwingine, changamoto huwa ndiyo chachu ya maendeleo.