TUONGEE KISHKAJI: Kuupotezea mnanda, mchiriku ni kujinyima fursa

KWENYE Tamasha la Filamu la Kimataifa la Zanzibar (ZIFF) 2023, muziki ulikuwa ni sehemu ya burudani zilizokuwa zikitolewa. Kulikuwa na wasanii kadhaa waliokuwa wakitumbuiza kabla ya filamu kuanza na wengi walilitendea haki jukwaa.

Lakini nikiwa pale, bendi moja ya muziki iliuteka zaidi moyo wangu, bendi hiyo inaitwa Tanzania Dar Music Group na wenyewe wanaimba muziki wa mnanda. Jamaa walikuwa kila wanapogonga ngoma, hadhira inaamka, inashangilia, inaimba na kucheza nao.

Baada ya kuwasikiliza sana Tanzania Dar Music Group, nilipotoka kwenye tamasha, ilikuwa kila ninapopata nafasi ya kusikiliza muziki, nasikiliza muziki wa mnanda.

Na nilifanya hivyo kwa siku zaidi ya tatu mfululizo, kila nilipokuwa nafanya hivyo, wazo moja lilikuwa linakuja kichwani mwangu kwa kujirudia. Nilikuwa nakumbuka mchakato wa kutengeneza mdundo wa taifa, kisha nikakumbuka jinsi ambavyo wasanii wa muziki wa Bongofleva wanadaiwa kuacha kufanya muziki wenye vionjo vya kitanzania na kukimbilia aina nyingine ya mziki kama vile Afrobeats ya Wanaijeria na Amapiano ya Afrika Kusini.

Pia, nikawaza jinsi ambavyo sehemu nyingi zinazocheza muziki Tanzania, kwa maana ya redio na TV zisivyo na kawaida ya kucheza muziki wa mnanda.

Lakini zaidi nikawaza jinsi ambavyo mnanda unavyofanana na baadhi ya ngoma za makabila ya Tanzania na hiyo ikanifanya nigundue, kwenye mnanda, ni kama vile wanamuziki wa Tanzania walijikosesha fursa kubwa sana ya kuwa na muziki ambao una ladha za kitanzania kwa asilimia kubwa.

Najua tunaipenda Bongofleva na tunasema ndiyo muziki wetu watanzania, lakini kiukweli Bongofleva ni ngumu kuelezeka. Ukimuuliza mtu unaposikiliza muziki, ikipigiwa ngoma ya Bongofleva mbali na lugha ya kiswahili inayotumika kuimbia, kitu gani kingine kitakufanya ugundue kuwa hii ni Bongofleva?

Hutopata jibu lililonyooka, huyu atasema lile, yule atasema hili. Ana shida hii ipo hata kwa waanzilishi wa Bongofleva wenyewe. Mmoja anaweza kukwambia, Bongofleva ni mchanganyiko wa muziki wa taarabu na vionjo vya kitanzania, mwingine akakwambia Bongofleva ni muziki wa kimagharibi kama vile R&B na Pop iliyochanganywa vionjo vya kitanzania na kuimbwa kwa lugha ya kiswahili. Kwanza vionjo vya kitanzania ndiyo vipi?

Maswali kama hayo yanafanya muda mwingine Bongofleva ionekane kama vile pia sio muziki wetu. Na ndiyo maana nashindwa kujizuia kusema pengine kuinyima fursa muziki kama mnanda, mchiriku, singeli na miziki mingine ya aina hiyo ni kama vile tulijinyima fursa ya kuwa na muziki ambao unafanana na sisi kwa kiasi kikubwa, muziki ambao ungetuwakilisha vizuri.

Na uzuri ni kwamba, muziki kama mnanda na mchiriku unaweza kuchanganywa na usasa wa aina yoyote na bado ukawa muziki mzuri. Nakukumbusha kipindi ambacho Young D alikuwa anarap kwenye biti za mchiriku. Pengine tukijaribu kuipa nafasi miziki hii tunaweza kuwa na muziki ambao tunasema kusimama mbele kwa kujiamini na kusema huu ni muziki wetu.