Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TUONGEE KISHKAJI: Hivi bado tunahitaji haya katika video?

Muktasari:

  • Video ya wimbo wa Dizasta aliouachia hivi majuzi akimshirikisha G Nako unaitwa Utaliimba Jina Langu. Ni wimbo kuhusu mtu ambaye ambaye amefariki dunia na sasa anatusimulia ‘experience’ hiyo huku akituambia jinsi atakavyokumbuka na kutuuliza jinsi  tutakavyomkumbuka.

NATAMANI wasanii wangekuwa wanatengeneza video za ngoma zao au angalau baadhi ya video za ngoma kama Dizasta Vina. Simpo, lakini imejaa maana kubwa.

Video ya wimbo wa Dizasta aliouachia hivi majuzi akimshirikisha G Nako unaitwa Utaliimba Jina Langu. Ni wimbo kuhusu mtu ambaye ambaye amefariki dunia na sasa anatusimulia ‘experience’ hiyo huku akituambia jinsi atakavyokumbuka na kutuuliza jinsi  tutakavyomkumbuka. Pia akitukumbusha kwamba hakuna atakayedumu duniani.

Video inaanza na picha ya jiwe la kaburi, kisha baada Dizasta kuanza kuimba tunaanza kuona picha za watu maarufu waliofariki dunia zikipita moja baada ya nyingine. Ruge, Amina Chifupa, Sajuki, Kanumba, Manji, Nasma Hamis, Mkapa, Godzila na wengine. Na hii ni mwanzo mpaka mwisho wa ngoma.

Yaani ukiangalia video hiyo unajikuta unashtuka kugundua kifo kimeondoka na watu wangapi maarufu, matajiri na wenye nguvu na kufanya ujumbe wa wimbo ukufikie kiulaini kwamba duniani tunapita tu, hakuna chenye umaana hapa zaidi ya utu.

Sisemi video zote ziwe zinaonyesha picha za waliofariki dunia, hapana. Nachosema ni video za muziki ni sanaa ya kujitegemea. Ni sanaa ambayo ina nguvu muda mwingine kuliko hata wimbo wenyewe ikitumika vizuri. Wimbo kama This is America ambao umejikita kwenye kuelezea kadhia wanazopitia raia wa Marekani pengine ulikuwa ni wimbo wa kawaida sana mpaka video ilipotoka. Ilikuwa ni video iliyofikisha ujumbe kibunifu na mpaka ilifanyiwa ‘challenge’  kurudiwa na wasanii tofauti nchi zingine.

Mtu kama Whozu aliirudia na hivyo ndivyo alivyopata umaarufu wake kama msanii wa muziki. Kwa Tanzania tumejikita kwenye video zenye magari mazuri. Wanawake wanaocheza nusu uchi. Lokesheni au seti ambazo zimerembwa tena sanasana kurembwa na masofa na kuta za rangirangi bila kusahahu madansa wakicheza wakiwa wamevaa nguo za kufanana. Ni kitu kizuri, lakini kuna baadhi ya ngoma unaona kabisa hii video imelazimishwa kuonekana hivi, haiendani, wimbo kama huu ulitakuwa kuwa na kitu simpo chenye maana.

Na madairekta wanafanya hivi kwa kuiga bila kujua kwamba huko wanapoiga wenzao hufanya kwa maana na hufanya kwa kufikisha ujumbe. Ukiona sofa lipo katikati ya chumba kipana chenye kuta za rangi huwa na maana inayoendana na ujumbe wa wimbo sio tu kwa sababu inaonekana vizuri. Kuna video moja ya Diamond ina watu wamevaa nguo zenye logo ya chama cha Nazi ambacho kilikuwa chini ya Adolph Hitler aliyefanya mauaji ya maelfu ya raia wa Kiyahudi. Kwanza logo hiyo inakwepwa kama ukoma kwenye kazi za sanaa labda ambazo zinaongelea ishu za Unazi. Lakini kwenye video ya Diamond, madansa wamevaa na wanacheza kabisa kwa furaha.

Amini kwamba, siku Diamond akienda kimataifa ile ya kuitwa kwenye intavyuu kwenye mashoo makubwa ya TV za sehemu kama Marekani lazima atatakiwa kuielezea kwanini madansa wake walivaa hivyo huku wakicheza kwa furaha. Je na yeye ni Mnazi? Na ukiwa mnazi kwenye ulimwengu wa kimataifa shughuli yako imeisha hakuna mtu atataka hata kukaa na wewe. Kwa hiyo nadhani wasanii na madairekta wawe wanajadiliana kuona ni jinsi gani nyimbo zinaweza kuwakilisha wanachoimba. Na mara nyingine unaweza ukakuta kujadiliana kunapunguza hata gharama ya uandaaji wa video hizo. Kwa sababu nina uhakika video inayoonyesha picha za watu maarufu waliofariki dunia inatengenezeka kwa gharama rahisi kuliko video yenye magari ya kifahari.