TUONGEE KISHKAJI: Faida ya majina mazuri kwa mastaa

JINA lina faida kubwa kwenye biashara yoeyote. Kimsingi kuna wataalamu wa biashara wanasema sehemu kuu muhimu zinazokuunganisha mfanyabiashara na wateja wako ni mbili. Kwanza ni huduma au bidhaa unazouza na pili ni jina lako.

Kwa mfano, tuseme wewe una biashara ya kuuza vifaa vya muziki. Na vifaa vyako ni vya kipekee sana na halisi (OG) kabisa na bei pia ni rahisi lakini jina la duka lako ni tusi ambalo hatuwezi hata kuliandika hapa, unadhani jina hilo linaweza kuathiri mauzo yako kwa kiasi gani?

Je, watu wataendelea kununua bila kujali au wataacha? Unadhani wateja watakuwa wanalizungumzia vipi duka lako? Kwamba mtu akiulizwa hiyo spika umenunua wapi ataje jina la duka lako ambalo halitamkiki mbele za watu au itamlazimu aseme “duka moja lipo hivi lipo mtaa fulani”.

Sasa kwa sababu sanaa pia ni biashara, hebu leo tuangalie majina ya wasanii yanavyoweza kuwa na madhara chanya na hasi kwa wasanii na kazi zao.


JINA LINAUMBA

Hayati Ruge Mutahaba mmoja wa watu waliochangia kuukuza muziki wa Bongofleva alikuwa  muumini mkubwa wa majina mazuri yanayoeleza ukuu unaotaka kuufikia. Amewahi kutolea mfano kuhusu kampuni aliyokuwa akiifanyia kazi ya Clouds, kwamba jina hilo lilikuja kwa sababu mawinguni, juu, angani kabisa ndipo walipotaka kufikia na aliamini ukijinenea mema - mema yatatokea na yanaweza kuanzia kwenye jina.

Mfano wa majina ya kutabiri mambo mazuri ni kama Diamond Platinumz, Baraka Da Prince, Joh Makini huku majina kama P Mawenge, Nikki Mbishi, Nay wa Mitego yakiwa ni kinyume cha majina mazuri.


LINAOKOA NA MASHAMBULIZI

Unapokuwa msanii kushambuliwa ama na mashabiki au wasanii wenzako ni jambo la kawaida, lakini mambo huwa mabaya zaidi unapokuwa na jina linalotoa fursa ya kushambuliwa kwa urahisi. Jina kama Ney wa Mitego.

Nyota huyu wa muziki kipindi alipokuwa na bifu na Nikki Mbishi, na Nikki akatoa ‘diss track’ inayooitwa Neema wa Mitego ambayo humo ndani amemuongelea msichana anayeitwa Neema ambaye amejaa mitego na tabia za kudanga.  Jina likawa limetoa urahisi sana kwa Ney kushambuliwa.


NI BRAND MUHIMU

Fikiria gazeti la Mwanaspoti lingekuwa linaitwa gazeti la kuongelea michezo, wanamichezo, sanaa, wasanii na burudani Tanzania, Afrika na duniani ni watu wangapi wangekumbuka hilo jina?

Iko hivyo pia kwa wasanii majina mafupi na ya kukumbukwa husaidia msanii kuwa wa kisasa muda wote na kukumbukwa. Jina kama Zuchu, Alikiba, Harmonize, Nandy na kadhalika tunayakumbuka sio kwa sababu wao ni maarufu, bali pia kwa sababu ni majina rahisi kukumbukwa.

Na hii huenda mbali hata kwenye majina ya kazi za wasanii. Ni rahisi kukumbuka wimbo unaoitwa Maokoto kuliko pesa inatafutwa kirahisi.