Steve Nyerere azidi kuwakoroga wanamuziki, uongozi wapewa saa 48

Muktasari:
- Msanii Steve Mengele maarufu Steve Nyerere, amezidi kuwagawa wanachama wa Shirikisho la Muziki Tanzania (SMT) kutokana na kuteuliwa kwake kuwa msemaji wa Shirikisho hilo.
Dar es Salaam. Msanii Steve Mengele maarufu Steve Nyerere amezidi kuwagawa wanachama wa Shirikisho la Muziki Tanzania (SMT) kutokana na kuteuliwa kwake kuwa msemaji wa Shirikisho hilo.
Mjadala wa kumkubali na kukataa uteuzi wa Steve ulianzia kwenye mitandao wiki iliyopita ikiwa ni muda mchache tu tangu uongozi wa shirikisho umtangaze.
Jambo hilo lililosababisha Shirikisho kuitisha kikao cha wanachama leo Jumatatu Machi 21, 2022 kilichoketi jijini humo kujadili muafaka wa uteuzi huo.
Katika hilo wapo wanaokubaliana na maamuzi ya bodi kuwa msemaji wao huku wengine wakimkataa na kutoa saa 48 kwa uongozi wa shirikisho hilo kumuondoa katika nafasi hiyo.
Katika utoaji wa maoni hayo, baadhi walioneka kuwa na hasira na kusema kuwa patachimbika msanii huyo asipoondolewa na wengine kusema wamedharauliwa kwa kiwango kikubwa kuwekewa mtu asiyejua namna walivyoupigania muziki wao na wala hajui changamoto wanazopitia.
Mmoja wa waliopinga ni Mbunge wa Muheza, Hamisi Mwinjuma 'Mwana FA' ambaye pia ni msanii wa muziki wa Hip Hop kwa kusema kuwa kwa katiba ya shirikisho, Steve hana sifa ya kupewa nafasi hiyo ikiwemo kutokuwa mwanamuziki.
"Katiba ya Shirikisho inamtaja Rais kama msemaji shughuli za shirikisho, hivyo kumteua Steve ni kupeleka mamlaka ya Rais kwa mtu mwingine,"
"Jingine katiba inasema Katibu wa Mahusiano wa kitaifa na kimataifa, atagombea nafasi hiyo ambapo hili halijafanyika, kuwa na uzoefu wa mahusiano ya kimataifa, kuliunganisha shirikisho na vyama vya kimataifa, bodi ya shirikisho na atakuwa msemaji na muandaaji wa matukio mbalimbali mambo ambayo Steve hakidhi sifa hizo," amesema Mwana FA.
Wakati Wambura Wasira maarufu kwa jina la Wakazi amesema endapo shirikisho hili litaendelea kumng'ang'ania Steve watawaondoa madarakani kwa kutokuwa na imani nao.
Kwa upande wake Kalapina, amesema wanatoa saa 48, Steve awe ameondolewa na kusema kama haitafayika hivyo wataondoa uongozi na kuongeza kuwa huyo wanayemuamini, kuna sehemu kibao ameshaharibu hivyo kama shirikisho hawaoni kama ana maana ya kuwa msema.
Hata hivyo wasanii wa nyimbo za injili, taarabu na dansi waliohudhuria kikao hiko akiwemo Abdul Misambano, walisema wanamkubali Steve Nyerere kutokana na kuwa na ushawishi kwenye jamii huku akitaka wasanii wa BongoFleva kama hawamtaki watafute msemaji wao.
Awali Rais wa SMT, Ado Novemba,amesema tatizo linaloonekana ni wasanii wa Bongofleva hususani Hip Hop kuwa wabinafsi na kujiona wao wana haki ya kuwasemea wengine jambo ambalo sio zuri.
"Bodi hiyo iliyomteua Steve Nyerere, leo inaonekana imekosea, lakini bodi hiyo iliyomteua Fid Q kuwa Katibu wa Shirikisho watu walikubali maamuzi yake, naomba leo niwaambie Bongofleva waache ubinafsi," amesema Novemba.
Wakati kuhusu kusigina katiba, amesema haina ukweli wowote kwa kuwa katiba inaruhusu bodi kuhuwisha baadhi ya sheria pale inapoona inafaa na kwa Steve ilikubaliana kumtafuta mtu atakewasemea na kutafuta vyanzo mbalimbali ili kulipeleka shirikisho mbele, kazi ambayo wanaamini anaiweza.
Hata hivyo amesema wamepokea maoni na wataendelea kupokea maoni kwa wanachama wengine ili kuja na muafaka wa jambo hilo huku akigomea saa 48 walizopewa wawe wamemtumbua Steve, kwa kile alichoeleza hawawezi kupangi wadau ila watafanya hivyo mara baada ya kuwasilikilza na wadau wengine.