Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sio Witness tu, hata Beyonce kapitia kwa Dolly Parton!

Muktasari:

  • Witness, mwanachama wa zamani wa kundi la Wakilisha, kwake jina la Kibonge Mwepesi lilikuja kutokana na namna anavyotumbuiza jukwaani. Licha ya kuwa mnene bado anavunja sana, ndipo mashabiki wakampatia jina hilo na hadi sasa anasonga nalo. Fahamu zaidi.

RAPA Witness a.k.a Kibonge Mwepesi ni miongoni mwa wanawake waliofanya vizuri sana katika muziki wa hip hop Bongo. Alikuwa mshindi wa Coca-Cola Popstar 2004 na alishinda tuzo ya Channel O kupitia wimbo wake, Zero (2008).

Witness, mwanachama wa zamani wa kundi la Wakilisha, kwake jina la Kibonge Mwepesi lilikuja kutokana na namna anavyotumbuiza jukwaani. Licha ya kuwa mnene bado anavunja sana, ndipo mashabiki wakampatia jina hilo na hadi sasa anasonga nalo. Fahamu zaidi.


1. Witness alianza kuchana mwaka 1997 akitumia zaidi lugha ya Kiingereza. Ni kipindi ambacho Lady Jaydee naye anachana nyimbo za Mc Lyte na Witness katika wimbo wake, Zero (2008) uliotayarishwa na Eryne na kumshirikisha Fid Q, amegusia hilo pia.


2. Kwa muda alipambana sana kutoka na kundi lake la Dream Team akiwa na Dataz na yeye ndiye alimpa jina hilo. Walikutana katika mashindano na shoo na wenzao kipindi hicho kama Hotpot Family (Soggy Doggy), GWM (KR), Bad Gangsters (TID) na kadhalika.


3. Mtangazaji Taji Liundi ambaye ni mwanzilishi wa kipindi cha kwanza kucheza Bongofleva redioni 1994, yaani DJ Show ya Radio One, hakuona tabu kuvua tisheti yake na kumpatia Witness kama zawadi baada ya kuonyesha uwezo mkubwa kimuziki. 


4. Kiu ya Witness kimuziki iliiva baada ya kupata nafasi ya kujiunga na Sekondari ya Jitegemee Dar, hiyo ni kufuatia kufanya vizuri katika mashindano ya muziki ambayo alipenda kushiriki kila aliposikia kuna sehemu yameandaliwa.

Hata hivyo, awali Witness alikuwa anasoma Oysterbay, rafiki yake, Rashida Wanjara ambaye alikuja kuwa Miss Mara na kuingia tano bora ya Miss Tanzania 2002, ndiye alimueleza kuwa Jitegemee kuna mashindano aende akajaribu bahati yake.

Na akiwa Sekondari ya Jitegemee, Witness na wanafunzi wenzake waliwahi kuimba kwenye moja ya hafla za aliyekuwa Hayati Rais Benjamin Mkapa na walifanya vizuri.


5. Witness ni miongoni mwa watu waliokuwa wanampa nafasi Dully Sykes kuingia katika shoo. Wakati huo Dully alikuwa anatoka kwao na kwenda Club Bilicanas na kumuomba Witness amuingize ndani na hata kumtafutia nafasi ya kutumbuiza.


Na upendo huo ndio ulimfanya Dully kutoa wimbo wake, Ladies Free (2004), kwa ajili ya Club Bilicanas ambayo kila Alhamisi wanawake walikuwa wanaingia bure ingawa katika wimbo huo kaitaja siku ya Ijumaa (Friday) ili kupata vina tu.


6. Unaambiwa Witness hakuwa na mpango wa kushiriki shindano la Coca-Cola Popstar East Africa 2004, bali  alienda tu ili kumuona msanii wa Afrika Kusini, Zwai Bala ambaye alikuwa sehemu ya Majaji.

Ikumbukwe Zwai Bala alifanya vizuri na ngoma, Shibobo (1998) kutoka katika kundi lake, TKZee, hivyo umaarufu wake hasa ndio uliomvutia Witness kujongea eneo la tukio.


7. Hata hivyo, Seven Mosha alipomsikia Witness akiimba wimbo wa Gwiji wa Country Music, Dolly Parton, Jolene (1973), akamshauri kushiriki shindano hilo ila kama rapa na sio mwimbaji, na hiyo ni baada ya kuvutiwa na uwezo wake.


8. Basi Witness alipojaribu bahati yake akashinda na baadaye akaungana na washindi wenzake ambao ni Shaa na Langa kisha kuunda kundi la 'Wakilisha' ambalo jina hilo ni muunganiko wa majina yao ya mwanzao.

Wakilisha ndio walikuwa washindi wa Coca-Cola Popstar 2004 upande wa Tanzania, huku Kenya likiwa ni kundi la Sema na Uganda, Blu 3, kundi lililovuma na kibao cha Where You Are (2009) wakiwashirikisha Radio & Weasel (Goodlyfe Crew).


9. Hivyo wimbo huo wa Dolly Parton (Jolene) ulimpa Witness tobo. Ni kama ambavyo Beyonce aliurudia na kuuweka katika albamu yake ya nane, Cowboy Carter (2024) ambayo ilikuja kushinda tuzo ya Albamu Bora Grammy (2025) ikiwa ni mara yake ya kwanza.


10. Wimbo wa kwanza wa Wakilisha 'Hoi' ulirekodiwa Afrika Kusini na hata video yake ilifanyika huko. Kwa ujumla walirekodi nyimbo nne chini ya MJ Records wakiwa huko. Na walitakiwa kufanya albamu watakaporejea Bongo ila ikashindikana hasa baada ya Shaa kujitoa katika kundi.