Ni zamu ya Afande Sele Bongo Flava Honors

Muktasari:
- Afande Sele atatumbuiza Agosti Mosi, 2025 kwenye ukumbi wa The Cask, Kawe Beach, Dar es Salaam.
MWANAMUZIKI Seleman Msindi 'Afande Sele' ametambulishwa kutumbuiza katika msimu wa tatu wa Bongo Flava Honors.
Afande Sele atatumbuiza Agosti Mosi, 2025 kwenye ukumbi wa The Cask, Kawe Beach, Dar es Salaam.
Meneja wa tamasha hilo, Kibacha Singo 'KSingo' amesema huo ni muendelezo wa kuwaheshimisha na kuwapa maua yao wakongwe wa Bongo Flava kupitia tamasha hilo linaloandaliwa na nguli wa muziki, Joseph Mbilinyi 'Sugu'.
Amesema mkongwe huyo kutoka Morogoro, historia na rekodi yake iliyotikisa katika Bongo Flava miaka mingi inakwenda kujirudia Agosti Mosi.
Akizungumzia namna alivyojiandaa na tamasha hilo, Afande Sele alisema historia inakwenda kujirudia.
"Nimekuwa mfalme wa Rhymes (mkali wa mashairi) ambaye sijapata mbadala, ile heshima na hadhi niliyoipata inakwenda kujirudia na kujidhihirisha dhahiri katika Bongo Flava Honors.
"Nimeipokea kwa dhati heshima hii niliyopewa na kaka yangu Sugu aliyenilea kwenye muziki, ninachoweza kuwambia mashabiki wangu na wale wa Bongo Flava kwamba Agosti Mosi, nitaliongoza vema jahazi hili," amesema Afande Sele.
Mwanamuziki huyo amesema siku hiyo atafanya shoo na wanamuziki mbalimbali aliowahi kufanya nao kazi kwenye kundi la Watu Pori ambalo yeye ndiye mwanzilishi na wale aliwahi kuimba nao nyimbo mbalinbali nje ya kundi hilo.
Akimzungumzia Afande Sele, Sebo Maganga alisema akitajwa yeye anamkumbuka kwa ngoma kali ikiwamo ya Mimi ni Msanii, kioo cha jamii.
"Ni wakati wa kuusikia na kuona muziki mzuri wa Afande Sele laivu kwenye Bongo Flava Honors, na kuwapa wasanii wetu wakongwe wa Bongo Flava maua yao wakiwa hai ma kutukumbusha wapi muziki huu umetoka," amesema.