Jux: Sijafilisika bado nadunda

Muktasari:
- Jux ameliambia Mwanaspoti, madai ya kwamba amefulia, hayana ukweli kwani yeye yuko imara kifedha na bado anaendesha biashara zake chini ya chapa yake ya African Boy kama kawaida.
MWIMBAJI wa Bongo Fleva, Jux amekanusha madai ya kufilisika hadi kufunga duka lake la African Boy baada ya kufanya sherehe ya kifahari ya harusi yake mkewe Priscilla Ajoke Ojo.
Jux ameliambia Mwanaspoti, madai ya kwamba amefulia, hayana ukweli kwani yeye yuko imara kifedha na bado anaendesha biashara zake chini ya chapa yake ya African Boy kama kawaida.
“Nasikia maneno mengi sana baada ya sherehe yangu ya harusi mimi na mke wangu Priscilla, mara nilichukua mkopo unaofikia kiasi cha Sh1 Bilioni ili kufanikisha sherehe yangu ya harusi iliyofanyika sehemu mbili tofauti Nigeria na Tanzania,” alisema Jux na kuongeza; “Eti sasa mkopo huo umenifilisi dukani na sehemu nyingine za biashara daah, mie naomba watu waache maneno maneno mengi ya kuongea vitu vya uongo. Duka langu lipo na litaendelea kuwepo na sidhani kama sherehe imetumika hiyo pesa wanayosema maana, sikufuatilia jumla ya matumizi, nilichokuwa nakiangalia ni furaha ya maisha mapya.”
Jux alifunga ndoa na Priscyla Februari 7, 2025, jijini Dar es Salaam, Aprili 2025, wanandoa hao walisafiri hadi Nigeria kwa ajili ya sherehe ya kitamaduni mjini Lagos Aprili 17, iliyofuatiwa na harusi ya kanisani Aprili 19.
Walihitimisha sherehe hizo kwa tafrija kubwa iliyofanyika Tanzania Mei 28 na kuwa mitandaoni.