Prime
Sheikh Walid ajitenga na ndoa ya Diamond, Zuchu

Ikiwa saa chache zimepita tangu msanii Diamond Platnumz kuchapisha video na picha zikimuonesha akifunga ndoa na Zuchu. Hatimaye Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Walid Kawambwa aliyeonekana akifungisha ndoa hiyo ametoa neno.

Baada ya Mwananchi kumtafuta na kutaka kujua ukweli wa jambo hilo, lililojawa na mitazamo mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii Walid ameonekana kujitenga na suala hilo huku akikataa kutoa taarifa zozote.
"Mimi siyo mzungumzaji wa vitu hivyo. Kwanini mnaniuliza juu ya ukweli wa hilo, wakati yule mtu kaposti vitu vyake yeye mwenyewe. Hamuwezi kumpata Diamond,"amesema.
Kutafutwa kwa Shekhe huyo kulikuja baada ya sintofahamu kutoka kwa watu wakitaka kufahamu ni kweli ndoa hiyo imefungwa au nikiki.
Utakumbuka jana Juni 1,2025, Diamond kwenye ukurasa wake wa Instagram alichapisha picha na video zikionesha akifunga ndoa akizisindikiza na ujumbe uliosomeka.

"Miongoni mwa vitu ambavyo nimejifunza ni ukomavu wa kukaa kimya. Ukomavu huu unataka uvumilivu wa hali ya juu, inataka uwe na moyo wa subra na hasa kukaza roho pindi mtu au watu wanapokuwa wanakupakazia ubaya fulani kwenye jamii halafu wewe una ukweli wake lakini unatakiwa ukae tu kimya usijibu ilhali ukweli unao ndani.
"Kwakweli si jambo jepesi linataka ustahimilivu wa hali ya juu sana na siwezi kusema eti nauweza sana, lakini namshukuru mwenyezi Mungu amenijaalia hekima hiyo kwa kiwango chake na nimekuwa nikiishi hivyo kwa muda mrefu kukaa kimya pindi yoyote akijaribu kusema lolote zaidi yangu na ndio maana hata interview nimekua naepuka kufanya siku hizi.

"Japo si jambo jepesi lakini faida yake nimeiona na ni kubwa maana vita yako inakuwa unapambaniwa na mwenyezi Mungu na inakufanya uwe mshindi kila siku. Anyways najua kila mmoja wenu ana picha tofauti kabisa kuhusu Diamond Platnumz na kuoa. lla tu nataka leo niwaambie kuwa huyu Diamond Platnumz alishawahi kuoa na kuna siku nitawaambia ikawaje,"amesema.
Licha ya ujumbe huo katika moja ya video aliyochapisha alisikika akimfuatisha Sheikh Walid kwa kutamka maneno haya, "Nimekubali kumuoa Zuhura Othaman kwa mahari yake tuliyokubaliana."