Rihanna amnyima usingizi Alikiba

HIVI karibuni mwimbaji kutokea Marekani, Rihanna ameachia wimbo wake mpya, Lift Me Up, ambao amekatisha ukimya wake uliodumu kwa zaidi ya miaka sita tangu alipoachia albamu yake, ANTI, chini ya Roc Nation.
Wimbo huo ambao staa kutokea Nigeria, Tems ameshiriki kwenye uandishi utatumika katika filamu ya Black Panther2: Wakanda Forever itakayotoka Novemba 11 mwaka huu.
Rihanna alikuwa kimya tangu alipoachia albamu yake ya nane, ANTI ambayo ilitoka Januari 28, 2016 baada ya kumaliza mkataba wake na lebo ya Def Jam Recordings ambayo ilikuwa imesimamia albamu zake tangu mwaka 2005.
Kati ya albamu za Rihanna zilizosimamiwa na Def Jam Recordings ni ‘A Girl Like Me’ iliyotoka Aprili 10, 2006 ikiwa ni ya pili kwa msanii huyo, huku ndani yake ikiwa na nyimbo zenye miondoko ya Pop, Reggae na RnB.
Baadhi ya nyimbo zinazopatikana katika albamu hiyo, A Girl like Me, ni ‘Unfaithful’ uliotoka Mei 2, 2006 ambao ilikuwa wa pili kuachiwa baada ya SOS uliotoka Februari 14 mwaka huo.
Ndani ya wimbo, Unfaithful, Rihanna amezungumzia uhusiano ulivyovunjika na kuonyesha ni jinsi gani ambavyo si mwaminifu kwa mpenzi wake hadi kumsaliti na anajutia lakini huyo jamaa yake alikuwa anafahamu hilo.
Rihanna anajua kuwa ni moja ya mambo mabaya sana ambayo yanaweza kumtokea mwanaume, anaweza kumuona akifa polepole lakini hataki kuwa muuaji ila nafsi yake inateswa na usaliti.
Mwanzo kabisa anaeleza amekuwa akifanya mambo mabaya maishani mwake, anatafuta jambo sahihi la kufanya lakini inaonekana kutofua dafu anaishia kufanya vitu vibaya tu na kumuacha na hatia.
Kutokana na hilo, anajawa na huzuni kwani anafahamu anachofanya ni kibaya kabisa na hakikubaliki, hata hivyo inaonekana yeye hawezi kuipinga hali hiyo ambayo inamtesa staa wa Bongofleva kutokea Kings Music, Alikiba.
Kwa mujibu wa RIAA (Recording Industry Association of America) wimbo huo ulifikia mauzo ya Platnum mara tatu, na kuingia katika orodha ya nyimbo tano bora za dunia katika nchi nyingi, huku ukishika nafasi ya sita kwenye chati za Billboard Hot 100.
Baada ya usaliti huo wa Rihanna, Alikiba alichoka na kuamua kueleza machungu yake katika wimbo wake, Infidele iliyotoka Januari 18, 2021 na baadaye alikuja kuujumuisha katika albamu yake ya tatu, Only One King iliyotoka Oktoba 4, 2021.
‘Infidele’ ni neno la Kifaransa ambalo ukilileta kwenye lugha ya Kiingereza litambulika kama ‘Unfaithful’, kwa lugha rahisi ya Kiswahili maneno hayo yanamaanisha ni hali ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mchepuko, yaani kutokuwa mwaminifu au usaliti.
Ndani ya wimbo huu Alikiba ni mwaminifu ila mpenzi wake, Rihanna ndiye amekuwa na tatizo la kumsalitiwa hadi anaona bora waachane kutokana Rihanna ni muongo na anataka auliwe na mabwana zake.
“Kumbe ni liar (muongo) unaweza niacha mi niuliwe na mabwana zako,” anaimba Alikiba katika wimbo huo iliotengeneza na Prodyuza Yogo Beats.
Hii inamaanisha akiendelea kusalia ndani ya penzi hilo atauliwa ndio maana mbele anasema; “Bora nikuache we uende, nami niende, tushiishe kizembe”.
Kauli hiyo haina tofauti na pale Rihanna anapojifananisha na muuaji kutokana na usaliti wake hali ambayo haipendi, hivyo anajutia na anataka kuondoka na kusema, “I don’t wanna be a murderer” (sitaki kuwa muuaji).
Ikumbukwe Infidele sio wimbo wa kwanza wa Alikiba kutumia lugha ya Kifaransa, alifanya hivyo katika ngoma yake, Aje, iliyotoka Mei 2016 chini ya RockStar Africa na kufanya vizuri hadi Sony Music Africa aliyokuwa akifanya nayo kazi wakati huo kumpatia tuzo na wimbo huo ulimuwezesha kushinda tuzo ya MTV EMMA 2016 kama Best African Act.