Richie: Wabongo wavivu kufikiri na kubuni

RICHIE
Muktasari:
Richie alisema watayarishaji wengi ni mahiri katika kunakiri na kukarabati sinema kutoka nje kama vile Nigeria na India.
SINGLE Mtambalike ‘Richie Richie’ amefunguka kuwa wasanii na watayarishaji wa filamu wa Tanzania ni wavivu wa kufikiri na kubuni katika uandishi wa filamu na uandaaji.
Richie alisema watayarishaji wengi ni mahiri katika kunakiri na kukarabati sinema kutoka nje kama vile Nigeria na India.
“Niseme ukweli, sisi ni wavivu na si wabunifu bali ni mahiri katika kukopi tu, hatujui kitu, ndio jambo ambalo linatufanya tushindwe kusonga mbele kwani kazi zetu ni zilezile hakuna kitu kipya.
“Angalia ilitoka filamu ya Kigodoro sasa hivi zimetoka aina hiyo kibao,” alisema Richie.
Msanii huyo alifafanua kuwa hata rafiki yake, Jacob Steven ‘JB’ naye aliingia katika mkumbo huo kwani naye ametengeneza Filamu ya Chausiku yenye mlengo kama huo.
Richie anawashauri watayarishaji wa kuwa wabunifu na kutumia wataalamu kwani sinema ni kazi inayotengeneza ajira si kuuza sura kama zamani.