Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rayvanny, Mondi ni kama Xavi na Iniesta!

PETER AKARO


IKIWA ni mwaka mmoja tangu Rayvanny aachane na WCB Wasafi, hilo halijaondoa ule muunganiko wake wa kikazi na Diamond Platnumz ambao umekuwa akitoa burudani ya uhakika kwa mashabiki kama walivyofanya Xavi na Iniesta.

Utakumbuka Rayvanny aliyejiunga na WCB Wasafi mwaka 2015 akiwa ni msanii wa pili, baada ya miaka sita ya kufanya kazi pamoja aliachana na lebo hiyo ya Diamond akiwa tayari amefungua yake, Next Level Music (NLM).

Chini ya WCB Wasafi alishinda Tuzo ya BET (2017), kutoa albamu moja, Sound From Africa (2021), EP tatu; Flowers (2020), New Chui (2022) na Flowers II (2022), huku akiwa msanii wa kwanza Afrika kutumbuiza katika Tuzo za MTV EMA 2021.

Miaka sita ndani ya WCB Wasafi, Rayvanny na Diamond wakawa mapacha wa kikazi kama ilivyokuwa kwa Xavi Hernandez na Andres Iniesta pale FC Bacelona, ulipigwa mwingi sana pale katikati.

Wakati klabu za Ulaya zikiiogopa Real Madrid, ila Madrid yenyewe ilipata tabu sana kwa ile Bacelona ya Xavi na Iniesta ambao wanatajwa kuwa miongoni mwa viungo bora kuwahi kutokea katika chama hilo la Catalunya.

Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Diamond na Rayvanny ndio wasanii pekee walioshirikiana zaidi na kutengeneza ngoma kubwa na kali ambazo zimetokea kupendwa na wengi na hata kupata namba kubwa katika majukwaa ya kidigitali.

Ni hivi karibuni tu Rayvanny kaachia wimbo wake mpya, ‘Yaya’ akiwashirikisha Diamond na Jux, hiyo ni baada ya kufanya vizuri na wimbo, Nitongoze (2022) ulioshinda Tuzo ya Muziki Tanzania (TMA) 2022 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana.

Wimbo huu (Yaya) ni wa pili kwa Rayvanny kumshirikisha Diamond akiwa nje ya WCB Wasafi baada ya ‘Nitongoze’, lakini ni wimbo wa tisa kufanya wao wawili tangu mwaka 2016 walipotoa wimbo wa kwanza, Salome.

Kwa ujumla Rayvanny na Diamond tayari wameshirikiana katika nyimbo zaidi ya 11, ni wazi wamegundua wakitoa kazi pamoja zinafanya vizuri kama ilivyokuwa kwa Xavi na Iniesta wakicheza pamoja.

Tayari wawili hao wameshirikiana kwenye nyimbo kama Salome, Iyena, Mwanza, Tetema, Timua Vumbi, Amaboko, Woza, Nitongoze na Yaya, huku wakikutana kwenye ngoma mbili zilizoshirikisha wasanii wote wa WCB Wasafi, Zilipendwa na Quarantine, hivyo kufanya jumla ya nyimbo 11.

Katika nyimbo hizo tisa, Diamond amemshirikisha Rayvanny katika nyimbo mbili, Salome na Iyena, huku Rayvanny akimshirikisha Diamond kwenye nyimbo saba ambazo ni; Mwanza, Tetema, Woza, Timua Vumbi, Amaboko, Nitongoze na Yaya.

Hivyo kwa kipindi cha miaka sita hakuna wasanii Bongo walioshirikiana zaidi ya hawa, huku Rayvanny akiwa ndiye msanii pekee aliyemshirikisha Diamond kwenye nyimbo nyingi kwa muda wote.

Ila hiyo ni tofauti kabisa na wasanii wengine, mfano Harmonize na Rich Mavoko hadi wanaachana na WCB Wasafi, Diamond hakuwahi kuwashirikisha bali wao ndio waliomshirikisha katika ngoma zao.

Harmonize alimshirikisha Diamond katika nyimbo mbili, ‘Bado’ na ‘Kwangwaru’, huku Rich Mavoko ikiwa ni moja, ‘Kokoro’, na wawili hawa hawajaweza kufanya kazi na Diamond nje ya WCB Wasafi kama ilivyo kwa Rayvanny.

Hivyo Rayvanny anaendelea kubaki kuwa msanii pekee aliyeshirikishwa zaidi na Diamond, ndani ya WCB Wasafi kwa muda wote Diamond kawashirikisha wasanii watatu tu katika nyimbo zake ambao ni Rayvanny, Zuchu na Mbosso.

Lava Lava, Queen Darleen, Harmonize na Rich Mavoko hawajawahi kupata nafasi hiyo, Darleen ndiye mwenye bahati mbaya zaidi maana hata kumshirikisha Diamond katika wimbo wake wowote ule hajafanikiwa!.

Utakumbuka nyimbo ambazo Rayvanny amemshirikisha Diamond, video zake zimekuwa zikipata idadi kubwa ya watazamaji YouTube, mfano ‘Tetema’ ina ‘views’ milioni 76, ‘Mwanza’ milioni 63, ‘Amaboko’ milioni 17 na ‘Nitongoze’ milioni 9.1. 

Ukimtoa Rayvanny, msanii mwingine wa Bongofleva ambaye ameshirikiana zaidi na Diamond ni Mbosso ambaye wamekutana katika nyimbo saba, huku nne zikiwa zao wawili pamoja. Wawili hao wametoa nyimbo kama; Baikoko, Karibu na Yataniua ambazo zote za Mbosso, huku Diamond akimshirikisha Mbosso katika wimbo wake mmoja, Oka, ukichanganya na ngoma za lebo ambazo ni; Zilipendwa, Jibebe na Quarantine, jumla ni saba.

Kwa jumla ndani ya WCB Wasafi mtiririko wa kushirikiana na Diamond upo hivi; Rayvanny (11), Mbosso (7), Lava Lava (6), Zuchu (5), Harmonize (3), Rich Mavoko (2) na Queen Darleen (2). Nje ya WCB Wasafi walioshirikiana zaidi na Diamond ni Nay wa Mitego, Shetta na Linex ambao kila mmoja ametoa nyimbo mbili na Diamond. Ikumbukwe Staa wa Nigeria, Mr. Flavour ndiye msanii wa kimataifa ambaye amefanya kolabo nyingi zaidi na Diamond zikiwa ni tatu, wawili wao wameshirikiana kwenye nyimbo kama ‘Nana’, ‘Time to Party’ na ‘Berna Reloaded’, huku Patoranking (Nigeria), Morgan Heritage (Jamaica) wakifanya kolabo mbili na Diamond.