Rayvanny awafunika Mondi, Harmonize aweka rekodi mpya

Muktasari:

  • Wasanii hao ambao awali walikuwa kwenye lebo moja ya muziki inayosimamiwa na Diamond ya Wasafi Classic Baby (WCB) walikuwa kwenye vipengele tofauti vinavyoshindaniwa kwenye tuzo hizo huku Mondi na Harmonize wakiondoka na tuzo moja kila mmoja.

Msanii wa Bongo Flava na mmiliki wa lebo ya Next Level Music, Rayvanny usiku wa Aprili 14, mwaka huu aliweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza nchini kutwaa tuzo tano za East Africa Arts Entertainment Awards (EAEA) zilizofanyika Nairobi, Kenya na kuwafunika Diamond Platnumz na Hamornize.

Wasanii hao ambao awali walikuwa kwenye lebo moja ya muziki inayosimamiwa na Diamond ya Wasafi Classic Baby (WCB) walikuwa kwenye vipengele tofauti vinavyoshindaniwa kwenye tuzo hizo huku Mondi na Harmonize wakiondoka na tuzo moja kila mmoja.

Rayvanny ameweka rekodi hiyo ikiwa tangu aondoke WCB na kuanzisha lebo yake na aliingia kwenye gemu ya muziki mwaka 2016 baada ya kusainiwa na Diamond.

Huu pia ni ushindi wake mkubwa katika muziki na akiwa nje ya WCB na vipengele alivyoshinda ni Msanii Bora wa Kiume - East Africa,

Album/EP bora - East Africa, Mwandishi bora - East Africa, Best lovers’, choice single - East Africa na Best inspirational single - East Africa.

Wasanii wengine waliopata tuzo hizo kutoka Tanzania na kushinda tuzo moja moja mbali na Diamond aliyeshinda ya Overall Hit-Maker Artist Of The Year (East Africa) na Harmonize "Single Again" aliyeshinda ya Overall Hit Single Of The Year (East Africa), wengine ni S2kizzy - Overall Hit-Maker Producer Of The Year (East Africa), Jux Ft Diamond Platnumz "Enjoy" - Eaea Collaboration Of The Year (East Africa) , Lizer Classic - Best Sound Engineer (East Africa), Mr LG - Best Breakthrough Beat/Hit-Maker (East Africa), Wcb Wasafi - Record Label Of The Year (East Africa.

Akizungumzia tuzo hizo baada ya kuwasili Uwanja wa ndege wa kimataifa ya Julias Nyerere, alilishukuru Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa kufanikisha ushindi huo na kukiri musiki wa Tanzania umebadilika na kukua.

"Nalisifu sana baraza la sanaa kwa bidii, tumebadilisha muziki wa Tanzania kuwa bora zaidi barani Afrika, sifa ni kwetu wote,” alisema Rayvanny aliyewahi pia kushinda tuzo za Tanzania Music Awards (TMA) 2022, Zikomo Awards (Zambia) 2022, Afrimma (Marekani) 2022, DIAFA Awards (Dubai) 2022 n.k.

Rayvanny pia ni mshindi wa tuzo ya BET (Marekani) 2017 kama ‘Viewer’s Choice Best New International Act’ akiwa ni msanii wa pili Afrika Mashiriki baada ya Eddy Kenzo wa Uganda 2015.

HONGERA SIO WA PAULA

Baada ya kuachia wimbo mpya 'Hongera' uliobeba maudhui na ujumbe kwa mwanamke aliye na ujauzito, kumekuwa na uvumi unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii, yakuwa staastaa huyo 'Chui’ amekanusha madai hayo hajamwimbia Paula bali ni kwa wanawake wote wajawazito.

Siku chache baada mtoto wa  mwigizaji mkongwe wa filamu  Bongo Kajala, Paula aliposti picha kwenye akaunti ya Instagram akiwa mjamzito na kuandika wanatarajia mtoto pamoja na mpenzi wake mwanamuziki Marioo, ndipo imeibuka habari za Rayvanny ameingia studio na kuwatungia wimbo wa hongera wawili hao.

Rayvanny ambaye aliwahi kuwa mpenzi wa Paula, kwenye huo wimbo  japo hakutaja moja kwa moja jina la Paula kwenye utunzi wake, wengi wanahisi ni ujumbe kwa wapenzi wapya, Marioo na Paula ambao wametangaza kutarajia mtoto hivi karibuni.