Rayvanny akosa Grammy, lakini dunia imemtambua

Muktasari:
- Ikumbukwe Rayavnny ndiye msanii pekee Tanzania aliyeshinda tuzo ya BET (2017), moja ya tuzo kubwa Marekani akiwa ni msanii wa pili Afrika Mashariki baada ya Eddy Kenzo (2015) wa Uganda.
Miongoni mwa wanamuziki kutokea Afrika waliohudhuria hafla ya utolewaji wa tuzo za 66 za Grammy 2024 huko Los Angeles nchini Marekani, ni pamoja na staa wa Bongofleva, Rayvanny ila haijawa bahati kwake.
Tuzo hizo zimetolewa usiku wa kuamkia leo Februari 5 katika ukumbi wa Crypto.com Arena, huku zikiacha majonzi kwa wasanii wa Nigeria ambao wamepoteza vipengele vyote walivyokuwa wakiwania msimu huu.
Ieleweke kwamba Rayvanny alikuwa anashiriki na sio kuwania tuzo za Grammy, yaani anashiriki kupitia mgongo wa albamu ya Maluma, Don Juan (2023) ambayo ilikuwa inawania kipengele cha 'Best Latin Pop Album' 2024.
Sababu ya kushiriki huko, albamu hiyo ndio ina wimbo wa Maluma 'Mama Tetema' ambao amemshirikisha Rayvanny. Ikumbukwe wimbo huo ndio umesampo wimbo wa Rayvanny, Tetema (2019) akimshikirikisha Diamond Platnumz.
Hata hivyo, albamu hiyo ya Maluma haijashinda na badala yake ushindi umeenda kwa Gaby Moreno kupitia albamu yake X Mi (Vo.1), hivyo kiu ya Rayvanny kupanda jukwaa la Grammy 2024 kuchukua tuzo ikaishia hapo.
Lakini kama albamu hiyo ingeshinda tuzo bado Rayvanny asingepewa tuzo, ni Maluma peke yake ndiye angepata, huku Rayvanny akipatiwa cheti na waandaji wa Grammy (Recording Academy) cha kutambulika kwa kushiriki katika kazi hiyo.
Ikumbukwe Rayavnny ndiye msanii pekee Tanzania aliyeshinda tuzo ya BET (2017), moja ya tuzo kubwa Marekani akiwa ni msanii wa pili Afrika Mashariki baada ya Eddy Kenzo (2015) wa Uganda.
Staa wa Amapiano kutoka nchini Afrika Kusini, Tyla ndiye msanii pekee wa Afrika aliyeshinda Grammy 2024. Ni katika kipengele cha Best African Music Performance akiwabwaga Asake, Burna Boy, Davido na Ayra Starr wote kutokea Nigeria.
Maumivu makubwa yamekuwa kwa mashabiki wa Burna Boy na Davido ambao hawajapata ushindi wowote licha ya kuchaguliwa kuwania vipengele vingi katika tuzo hizo kubwa zaidi duniani tangu mwaka 1959.
Burna Boy alikuwa anawania vipengele vya Best Global Music Album (I Told Them...), Best African Music Performance (City Boys), Best Global Music Performance (Alone) na Best Melodic Rap Performance (Sittin' on Top of the World).
Kwa upande wake Davido aliwania vipengele vya Best Global Music Album (Timeless), Best Global Music Performance (Feel, Unavailable) na Best African Music Performance.
Ikumbukwe msanii wa mwisho Afrika kushinda Grammy ni Burna Boy kupitia albamu yake ya tano 'Twice as Tall' (2020) aliyoshinda kama Albamu Bora ya Muziki Duniani 2021 na kuandika rekodi kama msanii wa kwanza wa kiume Nigeria kushinda Grammy kupitia kazi yake mwenyewe.