Ray Vanny anashiriki Grammy, sio kuwania

HIVI karibuni waandaji wa tuzo za Grammy, Recording Academy wametangaza majina ya wasanii wanaowania tuzo hizo za 66 huku kukiwa hakuna jina la msanii hata mmoja kutokea Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla.
Hata hivyo, ghafla majina ya Rayvanny na S2kizzy yanaibuka yakihusishwa na tuzo hizo na wao wenyewe wakifurahia hatua hiyo lakini ukitazama kwenye vipengele vyote 94 huwaoni. Je, suala hilo lipo vipi?.
Ukweli ni Rayvanny na S2kizzy wanashiriki na sio kuwania tuzo za Grammy, wanashiriki kupitia mgongo wa albamu ya Maluma, Don Juan (2023) ambayo anawania kipengele cha ‘Best Latin Pop Album’ 2024.
Albamu hiyo ndio ina wimbo wa Maluma ‘Mama Tetema’ ambao amemshirikisha Rayvanny, huku S2kizzy akiwa ndiye Prodyuza wa wimbo huo ambao umesampo wimbo wa Rayvanny, Tetema (2019) akimshikirikisha Diamond Platnumz.
Ikiwa albamu hiyo itashinda tuzo ya Grammy, basi Rayvanny na S2kizzy watapatiwa cheti na waandaji wa Grammy (Recording Academy), cha kutambulika kwa kushiriki katika kazi hiyo na hata isiposhinda kuna aina nyingine ya cheti watapatiwa.
Utakumbuka Nandy aliwahi kupatiwa cheti hicho baada ya albamu, Pamoja (2021) yake Etana kutoka Jamaica kuwania Grammy kama ‘Best Regggae Album’, Nandy alishirikishwa katika wimbo uitwao Melanin.
Wapo wanaodai Diamond naye alipatiwa cheti hicho baada ya kushiriki albamu ya Alicia Keys, ALICIA (2020) ambayo ilishinda Grammy kama ‘Best Immersive Audio Album’ 2021, huku Diamond akisikika katika wimbo, Wasted Energy.
Ila ukweli hakupata kutokana tuzo katika kipengele hicho haiendi kwa msanii, bali kwa Mhandisi wa albamu (The Engineer), Mhandisi Mkuu (Mastering Engineer) na Mtayarishaji (Producer), wasanii walihusika watapokea iwapo tu walishiriki kama watayarishaji.
Kama wimbo wa Mama Tetema ndio ungekuwa amechaguliwa, basi moja kwa moja Rayvanny naye angetajwa kama msanii anayewania na kama ukishinda angepatiwa tuzo, huku S2kizzy na wengine walihusika kama watunzi wakipatiwa cheti.
Hata hivyo, bado ingekuwa ni kupitia mgongo wa Maluma kutokana kisheria wimbo huo sio wake bali ameshirikishwa na hapa ndipo wengi wanachanganya mambo kwa kudai wimbo wa Rayvanny upo Grammy. Hapana, ni wimbo alioshirikishwa upo katika albamu inayowania Grammy.
Wapo wasanii wa Afrika walioshinda Grammy kupitia nyimbo walizoshirikishwa, mathalani Tems alishinda Grammy kupitia wimbo, ‘Wait For U’ alioshirikishwa na Future ambao ulishinda Grammy katika kipengele cha ‘Melodic Rap Performance’ 2023.
Kitu kama hicho ndicho pia kilimpatia Wizkid tuzo yake ya kwanza na ya pekee ya Grammy hadi sasa, ni baada ya wimbo wa Beyonce Knowles, ‘Brown Skin Girl’ aliopewa shavu na kushinda Grammy kipengele cha ‘Music Video’ 2021.
Waimbaji wote walioshiriki katika wimbo huo walipewa tuzo akiwemo mtoto wa Beyonce, Blue Ivy Carter ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka tisa tu na hivyo kuandika rekodi kama mtu mdogo zaidi wa pili duniani kushinda Grammy.
Utakumbuka Leah Peasall ambaye sasa ana umri wa miaka 32 ndiye anashikilia rekodi ya kuwa mtoto mdogo zaidi duniani kushinda Grammy na mwaka 2002 alishinda akiwa na umri wa miaka minane.
Hadi sasa ni wasanii 14 kutokea Afrika waliofanikiwa kushinda Grammy ambao kwa jumla wameshinda tuzo 27, wasanii hao wanatokea nchi sita tofauti ambazo ni Benin, Afrika Kusini, Cameroon, Senegal, Nigeria na Mali.
Mwimbaji wa Benin Angelique Kidjo na kundi la Ladysmith Black Mambazo kutokea Afrika Kusini ndio vinara wa kushinda Grammy barani Afrika wakiwa wameshinda tuzo tano kwa kila mmoja.
Washindi wengine ni Soweto Gospel Choir - Afrika Kusini (3), Ali Farka Toure - Mali (3), Wouter Kellerman - Afrika Kusini (2), huko walioshida tuzo moja moja wakiwa ni Burna Boy, Sikiry Adepoju, Wizkid na Tems wote kutokea Nigeria.
Wengine ni Miriam Makeba na Black Coffee wote wa Afrika Kusini, Tinariwen wa Mali, Youssou N’dour wa Senegal na Richard Bona wa Cameroon.
Staa wa Marekani, Beyonce ambaye ni mke wa Jay-Z, ndiye msanii aliyeshinda tuzo nyingi zaidi za Grammy duniani akiwa nazo 32 kabatini kwake, aliandika rekodi hiyo Februari mwaka huu baada kuivunja rekodi ya George Solti wa Hungary mwenye tuzo 31.
Washindi wengine wenye tuzo nyingi ni Quincy Jones (28), Alison Krauss (27), Chick Corea (27), Pierre Boulez (26), Vladimir Horowitz (25), Stevie Wonder (25), John Williams (25), Jay-Z (24), Kanye West (24) n.k. Ikumbukwe tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa Februari 4, 2024 nchini Marekani, zinatajwa kuwa tuzo za juu zaidi katika muziki, zilianza kutolewa tangu Mei 4, 1959 wakati huo zikifahamika kama Gramophone Awards. Lengo lake kuu ni kutambua mafanikio katika tasnia ya muziki.