Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pembe maisha yake ni funzo tosha

Muktasari:

Kitu ambacho hawezi na hajawahi kufanya ni kufeki. Anaishi maisha yake asilia na katika kuthibitisha hilo, Mwanaspoti lilimwibukia kwake maeneo ya Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam na kupiga naye stori mbili tatu kuhusu sanaa yake na maisha kwa jumla.

ANA stori. Ukikutana naye utagundua ni mstaarabu, lakini sifa yake kubwa ni kusikiliza mawazo ya mwingine.

Si mwingine ni msanii wa maigizo ya vichekesho nchini, Yusuf Kaimu ‘Pembe’. Mzee wa Kirungu.

Kitu ambacho hawezi na hajawahi kufanya ni kufeki. Anaishi maisha yake asilia na katika kuthibitisha hilo, Mwanaspoti lilimwibukia kwake maeneo ya Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam na kupiga naye stori mbili tatu kuhusu sanaa yake na maisha kwa jumla.

ALIVYOPATA MKE

Mzee Pembe mbali na kuigiza, hata mapenzi anayajua na kwenye hilo hataki masihara kabisa kwani hata kwa namna alivyompata mkewe Mariamu kipindi hiko ni wazi alikuwa siriazi na mapenzi.

“Katika mapenzi hakuna masihara, nakumbuka nilipomwona mwaka 1976 na alinivutia sana machoni mwangu, akaingia moyoni. Sikutaka kuchelewa nikamwambia kaka angu akaenda kutoa posa kwa sababu sikutaka kumkosa.

“Taratibu nyingine zikafanyika, nikamwoa mwaka huo huo na ndiye ninayeishi naye mpaka sasa na bado tunapenda. Ninapofika katika sekta hiyo naiheshimu kwani ndio iliyonifanya niitwe baba, ndio inatufanya binadamu tuwepo wengi duniani,” anasema Pembe ambaye anasema kwenye penzi lao alishawahi kupitia majaribu ya shetani na kujikuta akichepuka kitendo kilichomkasirisha mkewe Mariamu lakini aliomba msamaha na mpaka sasa wako freshi.

“Mtelezo huo haukuniacha salama kwani nilifanikiwa kupata watoto watatu, nashukuru Mungu mke wangu ameamua kuwakaribisha kwa moyo mkunjufu nyumbani,” anasema.

WATOTO 10, WAJUKUU 10

Mungu amemjalia watoto 10, saba amezaa na mkewe Mariamu anayeishi naye na watatu kutoka kwa mwanamke mwingine. Kati ya hao wawili Salum na Adam wanacheza soka la mtaani, lakini anaamini ipo siku wataonekana vipaji vyao na watoto wengine wana vipaji vya kuigiza kama yeye.

KIWANJA SH5,000

Ukiona kinang’aa ujue kimeundwa na siri ya kata anaijua mtungi. Pembe anafichua nyumba aliyojenga anakoishi hadi sasa kiwanja alinunua kwa Sh5000 tu alizozidunduliza kwa miezi minne mwaka 1987, kabla ya kuanza kusaka nyingine kwa ajili ya ujenzi.

“Sanaa zamani licha ya kubeba ujumbe uliokuwa ukiigusa jamii ya Watanzania, lakini haikulipa sana kama sasa na ndio maana maendeleo yetu yalikuwa taratibu sana,” anasema na kumshukuru Mungu amepata pakulaza kichwa chake kwani haikuwa rahisi kukamalisha nyumba yake.

PESA YAKE YA KWANZA KUBWA

Mwaka 1981 akiwa mfanyakazi wa Shirika la Maendeleo (DDC), anakumbuka alipata Sh480 (mia nne na themanini) na hiyo ndio ilikuwa pesa yake kubwa ya kwanza kushika kwani kipindi hiko ilikuwa ni nyingi.

“Kwanza nilimnunulia mke wangu zawadi ya vitenge na nyingine nikaitumia kwa matanuzi na matumizi muhimu ya hapa na pale,” anasema Pembe anayefichua kama kuna kitu hatakisahau kwenye maisha yake ya kuigiza vichekesho ni kituko alichofanya na Senga swahiba wake cha kunyenyua chuma na kashindwa wakati wakiigiza.

TABU MTINGITA BALAA

Wasanii wa vichekesho wamekuwa wengi nchini, hata kwa upande wa wanawake kwa sasa ni tofauti na zamani lakini kama kuna msanii wa vichekesho anakubali kazi zake zaidi kwa upande wa wanawake ni Tabu Mtingita, kwani ana kipaji halisi na tayari wameshacheza pamoja baadhi ya vichekesho.

“Mara ya kwanza kuongea naye kwenye simu, nilijikuta nacheka hadi nkashindwa kumkatalia kufanya naye kazi, anajua kujieleza na kuigiza mambo yanayogusa wengi.” “Hakuna mtu mgumu kana Senga, si mtu wa kukubali jambo kirahisi ila nilishangaa Tabu anasema amemkubalia kufanya naye kazi. Tabu anaifanya sanaa hii iwe ya mvuto,” anasema na kuongeza zamani alikuwa akiimba kwaya na kikundi cha kwaya ya Chama cha TANU, akiimba sauti ya tatu kabla haijavunjika baada ya TANU kufutwa na maisha kuendelea mbele.

URAFIKI NA SENGA

Ukiwaona pamoja kwenye runinga lazima ushike mbavu lakini kama hujui wawili hawa wamekuwa pamoja kwa muda mrefu na mwaka 2006 waliamua kujiondoa kwenye Kundi la Kaole kutokana na matatizo ya kimasilahi na wasanii wengi waliondoka kila mmoja akiangalia mishe nyingine huku wao wakifanya kazi pamoja na silaha yao anasema ni uaminifu ndio maana wanaendelea.

ALIKOLITOA RUNGU LAKE

Mara nyingi Pembe akiigiza humkosi na rungu lake. Hata hivyo kama hujui tu rungu hilo ni kati ya mawili aliyoyanunua mwaka 1995 kwa Sh600 mjini Kondoa, mkoani Dodoma akiwa na nia ya kuunga mkono sanaa ya uchongaji.

Hata hivyo anasimulia alijikuta akiendelea kulitumia kwenye sanaa kutokana na mashabiki.

“Kuna siku nilipanda nalo kwenye jukwaa tukifanya shoo. Watu walishangilia walipoliona na hiyo ndio ikawa sababu ya kuamua kulitumia kama nembo yangu kwa mashabiki.”

JINA LA PEMBE

Pembe ni jina ambalo limezoeleka kwa mashabiki zake, lakini mwenyewe anadai aliyempa jina hilo ni marehemu Amri Athuman ‘King Majuto’.

“Awali sikuwa naitwa Pembe ni baada ya mzee wangu Majuto kuniona kazi yangu na kuniambia nibadili jina ndio maana namkumbuka mpaka leo,” anasema na kuongeza Mzee Majuto ni kati ya wasanii wakongwe walioacha alama kubwa ya kazi zinazoishi na zenye mafunzo kwa vijana wa sasa kufanya sanaa ipate heshima kubwa.

MADILI KIBAO

Kumbe jamaa anapiga pesa. Hii ni kutokana na kukubalika kwa mashabiki na yeye pamoja na Senga wamekuwa wakipata dili kibao hadi mikoani.

“Mfano tu hapa tumeshakula pesa ya watu kwa ajili ya Pasaka. Tunasubiri tu muda ufike tukafanye kazi mkoani. Hata hapa Dar es Salaam kuna kazi kama za siku ya kuzaliwa, harusi na nyinginezo na bei zetu inategemea na mtu anayetualika na makubaliano.”

FUNDI WA SOKA

Pembe ana watoto wanaocheza soka la mitaani, ni wazi vipaji hivyo wamerithi kwake kwani awali alikuwa akicheza soka hasa namba saba na 11. Hata hivyo, kutokana na masihara yake aliyokuwa akifanya baada ya mechi na kuchekesha watu, wenzake walimshauri ahamie kwenye uigizaji na aachane na soka na huo ndio ukawa mwanzo wa safari yake.

SINGELI  KIMATAIFA

Muziki unaovuma kwa sasa nchini ni Singeli na Pembe anakubaliana na hilo akidai kila kitu kina wakati wake na Singeli imefikia wakati wake tofauti na zamani ulionekana wa kienyeji sana na haukukubalika.

“Singeli imefika dunia nzima kwa sababu ya mambo ya sayansi kwani mwanzo haikuwa hivyo. Itazidi kukua na kufika mbali zaidi.”