Patrick ana jambo lake kwa Kanumba

Saturday July 30 2022
Patrick PIC
By Charity James

MMSANII anayefanya vizuri kwenye tamthilia ya Pazia, Othman Njaidi ‘Patrick’ amefunguka kuwa ana jambo kubwa la kufanya kwenye tasnia ya filamu ili kumuenzi marehemu Steven Kanumba.

Patrick, aliyeibuliwa mwishoni mwa enzi za uhai wa Kanumba akiwa na Jennifer Kanumba kwa pamoja wamesema wana mpango wa kuandaa kitu kikubwa na bora ambacho kitaweza kurudisha ubora wa tasnia hiyo.

“Tangu kufariki dunia kwa Kanumba ambaye ametufanyia mambo makubwa enzi za uhai wake kwa kuibua vipaji vyetu, hakuna jambo kubwa tulilolifanya, mpango wangu nikishirikiania na Jennifer ni kufanya kazi kubwa ambayo itaibua hisia za wadau wa filamu,” alisema Patrick na kuongeza;

“Mimi kwa upande wangu tangu nimeingia kwenye tasnia ya filamu chini ya marehemu Kanumba nimekuwa nikijiendeleza kwa kuonekana kwenye tamthilia mbalimbali, naamini uzoefu wangu utakuwa chachu ya kuandaa kazi bora.”

Patrick alisema ana imani na uwezo wa Jennifer pamoja na kutokuonekana kwa muda mrefu kwenye filamu lakini anaamini ni moja ya wasanii wenye kipaji kikubwa hawezi kusahau muda ukifika watafanya kitu kitakachoamsha hisia za wengi.

“Sanaa ni kipaji na Kanumba aliacha vijana wa kazi hatuwezi kukurupuka na kufanya kitu cha ovyo tunataka kufanya kitu kikubwa na bora cha kuweza kutupa hadi tuzo kubwa.”

Advertisement
Advertisement