Nyota hawa wameupiga mwingi sana mwaka 2021

Sunday September 26 2021
Ntota 1
By Peter Akaro

Zimesalia siku chache kutimia robo ya tatu ya mwaka 2021, mengi yametokea kwenye kiwanda cha muziki wa Bongofleva, wasanii wameachia albamu, Extended Playlist (EP) na nyimbo, pia kufanya shoo kali.

Hii ni orodha iliyopangwa kwa mtiririko wa alphabeti ikionyesha baadhi ya wasanii wa Bongofleva ambao wamefanya vizuri zaidi upande huo hadi sasa robo ya tatu ya mwaka 2021 inapoelekea kukamilika.


1. Alikiba

Huu ndio mwaka ambao Alikiba katoa nyimbo nyingi, alianza na ‘Infidèle’ kisha ‘Ndombolo’ akiwa na wasanii wote wa Kings Music, huu ndio wimbo wa kwanza wa Bongofleva kushika nafasi ya kwanza TikTok, video zake zaidi ya 5,000 zilipandishwa kwenye mtandao huo.

Kizuri zaidi ni kolabo za kimataifa, kamshirikisha Rudeboy wa Nigeria katika ngoma yake ‘Salute’, kisha Mayorkun wa Nigeria pia aliyesikika kwenye ngoma ‘Jealous’, pia kuna ‘Songi Songi Remix’ akiwa na Maud Elka toka DR Congo, ambao unabamba kwa sasa.

Advertisement


2. Diamond Platnumz

Ilikuwa imetimia miezi saba bila Diamond kuachia ngoma mpya, Juni 25, 2021 ndipo aliachia ngoma yake ya kwanza kwa mwaka huu ‘Kamata’ iliyofanya vizuri, sasa anatamba na ngoma nyingine inayokwenda kwa jina ‘Naanzaje’.

Hata hivyo, ngoma yake yenye mahadhi ya Amapiano ‘IYO’ akiwashiirikisha Focalistic, Mpara A Jazz na Ntosh Gazi kutoka Afrika Kusini, imefanya vizuri sana kwa sababu ndio muziki unaovuma kwa sasa kwenye Bongofleva.


3. Harmonize

Licha ya ngoma zake binafsi kufanya vizuri, pia zile alizoshirikishwa na wasanii wa lebo yake, Konde Music Worldwide zimebamba, mfano ngoma ‘Kama’ ya Anjella ambayo ni ya pili kufanya pamoja mwaka huu baada ya kuachia, ‘All Night’.

Nyota 3

Mwimbaji huyu anayetamba na ngoma za Amapiano kama ‘Sandakalawe’, ‘Mang’dakiwe’ na ‘Teacher’, kwa sasa anaendelea na ziara yake nchini Marekani ambayo itachukua zaidi ya mwezi mmoja, haya ni matokeo ya nyimbo zake kufanya vizuri hasa kimataifa.

4. Mabantu

Hawa si wasanii wa kwenye mitandao sana ila muziki wao una nguvu zaidi mtaani na pia unapewa nafasi kubwa kwenye redio na runinga, wana njia zao tofauti za kuburudisha, huchoki kuwasikiliza.

Kundi hili linaloundwa na wasanii wawili, Mei 2021 waliachia EP yao ‘No Stress’ yenye nyimbo tano. Kizuri zaidi nyimbo zote zimefanya vizuri, tofauti na wasanii wengine wanapotoa EP au albamu.


5. Marioo

Anajipambanua kama msanii aliyeleta muziki wa ‘Swahili Amapiano’ baada ya kuachia ngoma yake ‘Mama Amina’ Novemba 2020, na sasa anafanya vizuri na ngoma mpya ‘Beer Tamu’ yenye mahadhi hayo pia, akishirikiana na Tyler na Visca.

Marioo, ambaye wikiendi iliyopita alitumbuiza kwenye tamasha la Simba Day na kufanya vizuri, toka mwaka huu kuanza ametamba na ngoma kama ‘For You’ na ‘Wow’ ambazo hadi sasa bado zipo kwenye chati.


6. Mbosso

Albamu yake ya kwanza ‘Definition of Love’ iliyotoka Machi 2021 ikiwa na ngoma 12, ni ya kwanza pia kuitoa akiwa chini ya WCB ambayo haijajumuisha nyimbo alizozitoa hapo awali. Hapa zote ni mpya.

Albamu hii ina ngoma kama ‘Baikoko’, ‘Kadada’, ‘Mtaalam’, ‘Your Love’, ‘Kamseleleko’ na ‘Karibu’ ambazo zote zimefanya vizuri kwenye chati za vyombo vya habari na mitandao mikubwa ya kuuza na kusikiliza muziki.


7. Nandy

Aliufungua mwaka kwa kuachia kolabo za kimataifa, alianza na ngoma ‘Number One’ akimshirikisha Joeboy wa Nigeria, ikafuata ‘Leo Leo’ akiwa na Koffi Olomide wa DR Congo, pia Juni 2021 akatoa na EP ‘Taste’ ikiwa na nyimbo nne.

Nyota 2

Kubwa zaidi ni mwendelezo wa tamasha lake ‘Nandy Festival’ ambalo limetoa burudani katika Mikoa kadhaa hapa nchini ikiwamo Kigoma, Mwanza, Arusha, Zanzibar, Dar es Salaam na Dodoma ambapo akiwa huko alipigiwa simu na Rais Samia Suluhu Hassan na kupongezwa kwa kazi hiyo nzuri.


8. Rayvanny

Kafanikiwa kuanzisha lebo yake, Next Level Music (NLM), kubwa zaidi Februari 2021 aliachia albamu yake ya kwanza ‘Sound From Africa’ ikiwa na nyimbo 23 na ndio albamu pekee hadi sasa iliyotoka mwaka huu yenye idadi kubwa ya nyimbo.

Albamu hiyo imeweka rekodi Afrika Mashariki kwa kufikisha wasikilizaji zaidi ya milioni 100 ndani ya wiki moja pekee tangu itoke. Ikijumuisha wasikilizaji kutoka kwenye mitandao ya Audiomack, iTunes, Spotify, YouTube, Boomplay na Apple Music.


9. Weusi

Albamu yao ya kwanza kama kundi ‘Air Weusi’ ambayo ilitoka Machi 2021 ikiwa na nyimbo 14 imefanya vizuri. Mpaka sasa hili ndio kundi pekee kutoka kwenye Bongofleva ambalo limetoa albamu kwa mwaka huu.

Ngoma kutoka kwenye albamu hiyo ambazo zilimefanya vizuri kwenye chati za redio na runinga ni ‘Mbupu’, ‘Tout Le Monde’ na ‘Penzi la Bando’ ambayo wamemshirikisha malkia wa taarabu nchini, Khadija Kopa.


10. Zuchu

Wimbo wake ‘Sukari’ uliotoka Januari 2021 umefanya vizuri sana, tayari video yake imetazamwa mara milioni 53 YouTube na ndio pekee iliyotazamwa zaidi Afrika Mashariki toka mwaka huu kuanza.

Akiwa bado anafanya vizuri na ngoma yake ‘Nyumba Ndogo’, Zuchu alikwenda kufanya shoo nyumbani kwao Zanzibar ‘Home Coming’ na kupata mapokezi makubwa, pia naye alipigiwa simu na Rais Samia Suluhu Hassan na kupongezwa kwa hatua hiyo nzuri katika muziki wake.

Advertisement