Ni Wema na Diamond tu!

Wema Sepetu na Diamond.
Muktasari:
- Kitendo cha Diamond kuzoa tuzo saba kiliufanya usiku huo kuwa mwanana kwake na mpenzi wake Wema ambaye alishindwa kuvumilia na kusema kuwa Diamond ndiye mume wake mtarajiwa.
USIKU wa kuamkia jana Jumapili ndani ya Mlimani City jijini Dar ulikuwa ni maalumu kwa Tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) lakini kwa kiasi kikubwa, usiku huo ulitawaliwa na mastaa wawili Wema Isaac Sepetu ‘Beatiful Onyinye’ na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Mwanaspoti linakupa undani.
Kitendo cha Diamond kuzoa tuzo saba kiliufanya usiku huo kuwa mwanana kwake na mpenzi wake Wema ambaye alishindwa kuvumilia na kusema kuwa Diamond ndiye mume wake mtarajiwa.
Wema aliyasema hayo baada ya Diamond kupokea tuzo ya saba ya Mtumbuizaji Bora wa Kiume wa Muziki, tuzo iliyokuwa ya mwisho kutolewa katika Ukumbi wa Mlimani City.
“Nina furaha sana na ninajivunia kuwa mke mtarajiwa wa mwanamuziki anayefanya vizuri, kitendo cha kupata tuzo saba ni ishara kwamba kazi zake zinakubalika,” alisema Wema.
Awali Wema alimkabidhi Diamond Tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kiume-Kizazi Kipya na kushindwa kutaja jina la mshindi moja kwa moja.
Kabla ya kukabidhi tuzo hiyo, mshereheshaji wa shughuli hiyo, Mjuni Silvester ‘Mpoki’ aliusifu uwezo wa Wema wa kuzungumza Lugha ya Kiingereza kwa ufasaha.
Wema ambaye ni Miss Tanzania wa mwaka 2006 aliangaza huku na kule na akasema “Baby where are you (mpenzi uko wapi),” kisha akamtaja mshindi kuwa ni Nasibu (Diamond).
Diamond alipanda jukwaani na kukumbatia Wema, kisha alichukua tuzo yake na baada ya picha mwigizaji huyo aliondoka jukwaani.
Lakini Diamond alimsihi asiondoke. Diamond alitoa shukrani zake kwa Watanzania kwa kumpigia kura na kisha akaushukuru na usingizi wake ambao ni Wema kwa kusema unamfanya aweze kufanya kazi bora.
“Lakini pia ninamshukuru mpenzi wangu kwa kunipa utulivu na usingizi mnono ambao unaniwezesha kuamka na nguvu mpya na kufanya kazi kwa ari na moyo ninamshukuru sana,” alisema Diamond huku akigeuka nyuma kumsaka Wema ambaye alishashuka jukwaani.
Historia ya usiku wa Wema na Diamond iliendelea kuandikwa baada ya watu wa karibu na wawili hao kupewa jukumu la kutoa tuzo akiwamo Martin Kadinda aliyetoa Tuzo ya Mtunzi Bora wa Mwaka-Kizazi Kipya.
“Naomba nimtangaze kwenu rasmi Mtunzi Bora wa Mwaka-Kizazi Kipya ambaye pia ni shemeji yangu… Diamond Platnumz,” alisema Kadinda.
Kama vile haitoshi kamera zote zilizokuwa ndani ya Ukumbi wa Mlimani City zilikuwa zikiwaandama wawili hao na wenyewe hawakuonesha kujali.
Wageni waalikwa waliohudhuria hafla ya ugawaji wa tuzo hizo walifurahia ‘pair’ (pea) ya wapenzi hao, huku wengi wao wakitaka kujua tarehe ya ndoa ya wawili hao.
Katika kuonesha kuwa wanawakubali Wema na Diamond, wageni hao waliwashangilia kila walipopanda jukwaani kwa ajili ya kupokea tuzo.
Mmoja wa waalikwa, Japhet Athanas alisema: “Kwa kweli naipenda pea hii, halafu kijana anaonekana kung’ara zaidi akiwa na Wema sijui kwa nini hamuoi, anahangaika tu?” alisema huku wageni wengine wakimuunga mkono.
Tuzo alizozoa Diamond ni Wimbo Bora Afro Pop (Number One), Mwimbaji Bora wa Kiume-Kizazi Kipya, Mtunzi Bora wa Kiume-Kizazi Kipya na Mtunzi Bora wa Mwaka. Nyingine ni Wimbo Bora wa Mwaka (Number One), Video Bora ya Mwaka (Number One) na Mtumbuizaji Bora.