Prime
Ni ukurasa mpya wa Hamisa Mobetto katika mapenzi

KWA mara ya kwanza Mwanamitindo maarafu Bongo, Hamisa Mobetto anajiachia hadharani na penzi lake jipya ikiwa ni takribani miaka mitano tangu kuachana na Diamond Platnumz ambaye walikuwa na uhusiano wa siri.
Raia wa Togo, Kevin Sowax ndiye ameushikilia moyo wa Hamisa kwa wakati huu, wawili hao wamekuwa pamoja Tanzania kwa zaidi ya wiki moja sasa na wikiendi iliyomalizika walikuwa wakifurahia harufu nzuri ya karafuu visiwani Zanzibar.
Utakumbuka kabla ya Kevin, Hamisa alihusishwa kuwa na uhusiano na Rapa wa Marekani, Rick Ross baada ya kuonekana kuwa na ukaribu katika mitandao ya kijamii na baadaye kukutana Dubai kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, ilikuja kubainika ukaribu wa wawili hao ulikuwa wa kibiashara zaidi baada ya kuonekana pamoja katika tangazo la moja ya kampuni ya mawasiliano ya simu, huku baadaye Rick Ross ukiacha kumfuata (unfollow) Hamisa katika mtandao wa Instagram.
Katika historia yake, Hamisa ambaye ni mama wa watoto wawili sio mtu wa kuweka sana hadharani mahusiano yake, ni vigumu kupata picha nyingi zake akiwa na wazazi wenziye, Majizzo na Diamond, hii ni kutokana na usiri au mtindo wake wa maisha kipindi yupo nao.
Lakini sasa mambo yamebadilika na yanaenda mbio, Hamisa ameweka wazi kila kitu kuhusu Kevin na hata kumtambulisha kwa mama yake mzazi, ni Hamisa ambaye hakuzoeleka kwa miaka zaidi ya 10 ya umaarufu wake katika kiwanda cha mitindo, filamu na muziki.
“Namuomba Mungu wa mwisho awe ni wewe Kevin,” aliandika Instagram Hamisa ambaye ni Miss XXL, After School Bash 2010 na mshindi wa pili wa Miss Dar Indian Ocean 2011.
Kutokana na hilo, Hamisa anakuwa mzazi mwenzie na Diamond wa pili kuonyesha wazi mahusiano yake baada ya Zari The Bosslady ambaye anadai tayari amefunga ndoa na mpenzi wake kutokea nyumbani kwao Uganda, Shakib Chams.
Ikumbukwe Hamisa ndiye alimwondoa Zari katika maisha ya Diamond baada ya kuwa na uhusiano wa siri na staa huyo wa Bongo Fleva kutoka WCB Wasafi hadi kujaliwa mtoto wakati anajua alikuwa na Zari kwa wakati huo.
Zari akampisha Hamisa kwa Diamond lakini wawili hao wakashindwa kuendelea, familia ya Diamond haikuwa upande wa Hamisa na hadi sasa haziivi, hivyo ukawa mwisho wa penzi lao na kubakia kama wazazi.
Ndipo Diamond akaanzisha uhusiano na Tanasha Donna kutoka Kenya ila hawakudumu, kisirani cha Tanasha na migogoro ya kifamilia vinatajwa kuwatenganisha wakiwa tayari na mtoto mmoja na hadi sasa Tanasha hajaweka wazi yupo na nani.
Ikiwa Hamisa na Kevin watafunga ndoa itakuwa ya kwanza kwa Mwanamitindo huyo ambaye ni mama wa Fantasy (2015) aliyejaliwa na Majizzo, na Dylan (2017) aliyejaliwa na Diamond.
“Tangu wakati nilipokuona nilijua wewe ndio mwenyewe, kadiri navyoendelea kukujua, hisia zangu zinaendelea kukua, nashukuru kuwa na wewe maishani mwangu, nafurahi juu ya nyakati zetu zijazo.” alisema Kevin kuhusu Hamisa.
Kauli ya Kevin ilikuja mara baada ya kumzawadia Hamisa gari jipya aina Range Rover na kuteka mazungumzo mtandaoni, muda mfupi baadaye walionekana wakiwa pamoja huko Guangzhou, China.
Kevin alipowasili Tanzania aliongozana na Hamisa hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutoa Sh1 milioni ili kusaidia watoto wadogo wanaopambana na ugonjwa wa saratani, fedha hizo zitasadia vipimo kwa watoto watano.
Huenda wawili hao wanamaanisha kuwa pamoja kwa muda mrefu, sio Hamisa wala Kevin, kila mmoja anaonekana kuwa na furaha na mwenzake kwenye mitandao ya kijamii ila bado ni mapema kumaliza maneno.
Ikumbukwe Hamisa alipata umaarufu kupitia mashindano ya urembo na baadaye kuingia kwenye mitindo, alifanya vizuri zaidi na kushinda tuzo kama Abryanz Style Fashion (Uganda), Starqt Awards (Afrika Kusini), Scream Awards (Nigeria), Young C.E.O Round Table (Tanzania) n.k.
Akiwa kama video vixen, Hamisa ametokea kwenye video za nyimbo kama My Baby (2013) wa Quick Rocka, Salome (2016) wake Diamond na Dodo (2020) wa Alikiba, huku akicheza filamu kama Endless Love, Vocha n.k.
Katika muziki Hamisa ametoa EP moja, Yours Truly (2022) yenye nyimbo sita, ameshirikiana na wasanii kama Diamond, Christian Bella, Seneta Kilaka, Whozu, Otile Brown (Kenya), pia kuna Korede Bello na Singah (Nigeria). Ana lebo yake, Mobetto Music na chapa yake ya mavazi, Mobetto Styles.