Ndoa ya Diamond, Zuchu imepita njia za mastaa hawa

Muktasari:
- Bila kujali ni kipi kinaendelea katika jambo hilo, tunakuleta mastaa wa muziki na filamu duniani ambao nao walifunga ndoa kimya kimya au kwa faragha na hata sherehe zao kuhudhuriwa na watu wachache tena sana kwa masharti fulani.
MASTAA wa muziki wa kizazi kipya nchini, Diamond Platnumz na Zuchu inadaiwa kufunga ndoa kimya kimya mbele ya watu wachache, jambo lililoibua mjadala na kuacha maswali kwa wengi kwa jinsi walivyoliwasilisha kwa mashabiki wao.
Bila kujali ni kipi kinaendelea katika jambo hilo, tunakuleta mastaa wa muziki na filamu duniani ambao nao walifunga ndoa kimya kimya au kwa faragha na hata sherehe zao kuhudhuriwa na watu wachache tena sana kwa masharti fulani.
Kelly Rowland & Weatherspoon
Mwimbaji huyo wa Destiny’s Child, alifahamiana na Weatherspoon tangu miaka ya 1990 na kuwa marafiki hadi 2013 walipochumbiana na mwaka uliofuatia hapo Mei 9,2014 walifunga ndoa iliyohudhuriwa na watu wachache huko Costa Rica.
“Nadhani tunataka tukifunga ndoa iwe sisi na mchungaji wetu pekee. Namaanisha, ni sisi wawili tu ambao tutakuwa kwenye hiyo ndoa,” alisema Kelly Rowland mwaka 2013 wakati akiongea na Jarida la People.
Miongoni mwa waliohudhuria ndoa yao ni pamoja na Jay Z na mkewe, Beyonce, Solange na Tina Knowles, huku ikidaiwa wawili hao waliamua kufunga ndoa isiyo na mambo mengi kwa sababu tayari Kelly Rowland alikuwa na ujauzito wa miezi sita.
Kanye West na Kim Kardashian
Mastaa hawa ambao uhusiano wao ulianza Aprili 2012, walisafiri kutoka Marekani hadi Florence, Italia na walifunga ndoa yenye wageni wachache, Mei 24, 2015 ikiwa ni mwaka mmoja tangu Kim kuvishwa pete ya almasi yenye ukubwa wa karati 15.
Waalikwa katika shughuli hii hawakuruhusiwa kuingia na simu na baadaye mastaa hao walikataa ofa ya Dola 11 milioni kutoka kwa majarida makubwa yaliyotaka picha zao kwa sababu za kibiashara.
Rafiki wa karibu wa Kanye West wakati hao, Jay Z hakuhudhuria harusi hiyo pamoja na mkewe, sababu inadaiwa ni Beyonce hakuwa tayari kuonekana katika reality show ya Kim, Keeping Up With The Kardashians, pia hajawahi kutaka kuwa karibu naye.
Jennifer Lopez na Ben Affleck
Ikiwa ni takribani miaka 18 tangu walipoachana, Julai 16, 2022, Jennifer Lopez na Ben Affleck walifunga ndoa kimya kimya huko Las Vegas, ikiwa ni ndoa ya nne kwa Lopez baada ya hapo awali kuolewa na Ojani Noa (1998), Cris Judd (2001) na Marc Anthony (2004).
Pengine waliamua kufanya jambo kimya kimya kutokana na yale yaliyowatokea hapo awali na uhusiano wao uliandamwa sana na vyombo vya habari hadi kuahirisha harusi yao iliyopangwa kufanyika Septemba 14, 2003 huko Santa Barbara. Wawili hao waliocheza pamoja filamu kama Gigli (2003) na Jersey Girl (2004), baada ya kufunga ndoa hiyo walinunua jumba lao la kifahari huko Beverly Hills kwa dau la Dola 60 milioni lakini baada ya kuachana Mei mwaka uliopita walitangaza kuuza jumba hilo.
Jay Z na Beyonce Knowles
Novemba 2006, Beyonce, mshindi wa Grammy 35 akiongea na Jarida la Cosmopolitan alisema katika maisha yake hajawahi kujiona kama Bibi harusi ingawa aliwahi kufikiri kuhusu aina ya harusi anayoitaka ambayo sio kubwa sana.
Kufikia Aprili 4, 2008, Jay Z na Beyonce wakafunga ndoa huko New York, huku ikiwa na wageni takribani 40, baadhi ya mastaa waliohudhuria ni Kelly Rowland na Michelle Williams, pamoja na marafiki zao, Gwyneth Paltrow na Chris Martin. Katika tukio hilo, simu zote za wageni zilikusanywa kabla ya shughuli kuanza ili kuhakikisha hakuna anayepiga picha wala kuchukua video. Mwaka 2011 ndipo Beyonce alifichua picha ya kwanza ya vazi lake la harusi katika video ya Live at Roseland.
Alicia Keys na Swizz Beats
Mkali huyu wa kibao, No One (2007), alifunga ndoa na Swizz Beatz, Julai 31, 2010 katika sherehe ya faragha iliyofanyika karibu na bahari ya Mediterania ikiwa ni miaka miwili tangu kuachana na mpenzi wake wa muda mrefu, Kerry Brothers Jr.
Hii ilikuwa ni ndoa ya pili kwa Swizz Beatz baada hapo awali kumuoa mwanamuziki Mashonda mnamo 2004 ingawa uhusiano wao ulianza 1998, na hadi wanaachana walikuwa na mtoto mmoja, Kasseem Dean aliyezaliwa Desemba 2006.
Mashonda aliwahi kumtuhumu Alicia Keys kuivunja ndoa yake na walifikia hatua ya kuwa paka na chui, pengine hili lilichangia kwa sehemu ndoa ya Alicia Keys na Swizz Beats ambaye ni mtayarishaji muziki mwenye mafanikio kufungwa kwa usiri.
Usher na Jennifer Goicoechea
Ikiwa ni siku chache kabla ya Usher Raymond IV kutumbuiza katika onyesho lake la Super Bowl, Februari 8, 2024, staa huyo na mpenzi wake, Jennifer ‘Jenn’ Goicoechea walipata cheti cha ndoa huko Las Vegas.
Siku nne baadaye, vyanzo vingi vilithibitisha wawili hao waliokuwa pamoja tangu mwaka 2019 walifunga ndoa wikiendi hiyo wakiwa tayari wamejaliwa watoto wawili, Sovereign Bo (2020) na Sire Castrello (2021).
Hata hivyo, mshindi huyo wa Grammy mara nane huku akiuza rekodi zaidi milioni 150 duniani kote, kabla ya kumuoa Jennifer, alikuwa katika ndoa na Tameka Foster na kupata watoto wawili, Usher V na Naviyd Ely.