Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nani kumrithi Brigitte Miss Tanzania?

Muktasari:

Warembo hao ambao wamekaa kambini si chini ya mwezi mmoja huku kila mmoja akiwa na shauku ya kutwaa taji hilo linaloshikiliwa na Brigitte Alfred na leo Jumamosi ndiyo itakuwa siku ya hukumu yao.

MASHINDANO ya Redds Miss Tanzania yanafanyika leo Jumamosi kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam na warembo 30 watawania gari jipya na fedha taslim Sh 8 milioni kutoka kwa wadhamini wakuu, Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL).

Warembo hao ambao wamekaa kambini si chini ya mwezi mmoja huku kila mmoja akiwa na shauku ya kutwaa taji hilo linaloshikiliwa na Brigitte Alfred na leo Jumamosi ndiyo itakuwa siku ya hukumu yao.

Mpaka sasa warembo watano wamekwishafuzu nusu fainali ya mashindano hayo ambayo yatapambwa na wasanii Lady Jaydee, Sarakasi Mama Afrika na msanii wa kizazi kipya kutoka Uganda, Mike Ross.

Mrembo atakayeshika nafasi ya pili kwa mujibu wa Meneja wa Redds, Victoria Kimaro atapata Sh 6.2 milioni, wa tatu Sh 4 milioni, wa nne Sh 3 milioni na wa tano Sh 2 milioni washiriki wengine kuanzia wa sita hadi 15 watapata Sh 1.2 milioni na waliobaki watapozwa kwa Sh 700,000 kila mmoja. Thamani ya fedha taslimu itakuwa ni Sh 46.1 milioni.

Brigitte aliyekuwa Miss Sinza alilitwaa taji hilo mwaka jana na kukabidhiwa gari aina ya Noah, pamoja na kitita cha Sh 8 milioni.

Mwaka huu Sinza inawakilishwa na warembo wawili, Miss Sinza aliyevaa ‘viatu’ vya Brigitte, Prisca Clement na mshindi wa tatu, Sarah Martin. Tayari Prisca ameingia nusu fainali (top 15) baada ya kushinda taji la vipaji.

Warembo wengine ambao wamefuata nyayo za Prisca ni Miss Tanzania Photogenic 2013, Happiness Watimanywa, Miss Tanzania Personality, Severina Lwinga, Miss Tanzania Top Model 2013, Narietha Boniface na Miss Tanzania Sports Woman, Clara Bayo. Warembo 25 wanakuwa na kazi ya kuwania nafasi 10 za nusu fainali ambao ni, Sabrina Juma, NiceJack Herman, Anastazia Donald, Lina Allan, Jacquiline Luvanda, Neema Mality, Diana Laizer, Sabra Islam, Janet Awetu, Elizabeth Pert, Lucy Charles, Esha Rashid na Salsha Esdory.

Wengine ni Mirima Manyanga, Lucy James, Svetlana Nyamweyo na Latifa Mohamed , Nancy Moshi, Glory Minja, Mary Chemponda , Lucy Tomeka, Philios George, Dorice Mollel, Alice Isaac na Carol Bayo.

Mshindi wa taji la mwaka huu atakuwa wa 21 katika historia ya mashindano ya urembo nchini yanayoratibiwa na Kampuni ya Lino Agency na ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia ya mwakani.

Kwa sasa Miss Tanzania anayemaliza muda wake Brigitte yupo Indonesia akijiandaa kuwania taji la Miss World katika mashindano yatakayofanyika Ijumaa ijayo. Mafanikio makubwa kwa Tanzania yalikuwa mwaka 2005, Nancy Sumary alipotwaa taji la mrembo bora wa Afrika (Miss World Africa). Mafanikio hayo yalipokelewa kwa mtazamo chanya na serikali na wadau wa mashindano ya urembo nchini.

Hii inatokana na ukweli kuwa warembo waliofuatia baada ya yeye walishindwa kufanya vyema kwa kumkaribia au zaidi ya yeye alivyofanya. Salha Israel aliyeshinda taji la Redds Miss Tanzania mwaka 2011 aliweza kuingia katika hatua ya 30 bora ya warembo waliofanya vizuri katika kipengele cha urembo wenye malengo maalumu.

Baada ya matokeo hayo, Tanzania ilirejea kidogo katika ramani ya mashindano ya dunia baada ya Lisa Jensen ambaye aliingia robo fainali ya taji la top model pamoja na warembo wengine 55. Lisa baadaye aliingia katika hatua ya 10 bora ya Multimedia Award.