Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nani atusahaulishe kuhusu Ray C

Muktasari:

  • Rehema Chalamila alikuwa anajua kuimba sauti yake ilikuwa laini, kama mashine ya kupooza moyo. Nadhani sauti ya Ray C ni moja ya sauti ambazo wahenga walizisikiliza, wakazichambua na ndipo wakapa msemo wa ‘sauti za kumtoa nyoka pangoni’.

KILA nikimtazama msanii mpya wa Bongo Fleva aliyesajiliwa kwenye lebo ya Nandy, Yasirun Yassin Shaban maarufu Yammy nashindwa kujizuia kumkumbuka Ray C. Sauti yake na mikogo ni kama Ray C anakuja kwa mbali na kupotea. Na kila nikimuona Yammy nashindwa kujizuia kujiaminisha kwamba hakuna msanii wa kike Tanzania aliyewahi kuwa ‘full package’ kumzidi Ray C.

Rehema Chalamila alikuwa anajua kuimba sauti yake ilikuwa laini, kama mashine ya kupooza moyo. Nadhani sauti ya Ray C ni moja ya sauti ambazo wahenga walizisikiliza, wakazichambua na ndipo wakapa msemo wa ‘sauti za kumtoa nyoka pangoni’.

Alikuwa na sauti nzuri kiasi kwamba ilikuwa ukisikiliza ngoma yake ya ‘Niwe na Wewe Milele’ unaweza kudhani ni pisi ya kihindi kutoka India imeamua kuimba Bongofleva. Si unajua sauti za Wahindi huwa haziishi masikioni, zinapenya mpaka moyoni, hivyo ndivyo alivyokuwa Rehema.

Ray C alikuwa na damu ya kutoa hit song. Nitajie wimbo mmoja tu wa Ray C alioutoa tangu anaanza muziki mpaka anapotea kwenye gemu ambao haukuwahi kuhiti nami nitakuonyesha mechi ya Yanga waliyocheza wakiwa wamevaa jezi nyekundu; HAKUNA. Niwe Nawe Milele, Wanifuatia Nini, Unanimaliza, Sogea Sogea, Nihurumie, Umenikataa, Watanionaje, Mapenzi Yangu, Nipe Mimi… zote za Ray C hizo. Na sio ngoma zake tu, Bi Mkubwa alikuwa mtu m-badi mpaka kwenye ngoma za kushirikishwa.

Nakumbuka mwaka fulani alipotoa ‘Nataka Niwe Nawe Milele’, kila mtoto alikuwa anaimba hiyo ngoma kwa kutumia mistari ya kutengeneza mwenyewe. Na niamini mimi, hakuna kipimo kikubwa cha umaarufu na kupendwa kwa wimbo kama wimbo kupendwa na watoto na kuimbwa na watoto.

Ray C alikuwa bonge moja la performer. Unadhani kwa nini anaitwa Kiuno Bila Mfupa? Ni kwa sababu kweli kiuno chake hakikuwa na mfupa. Nakukumbusha tu, asilimia 90 ya ngoma za Ray C ni ngoma za kutulia sio za kucheza, lakini kwa sababu Ray C ni performer alikuwa anatafuta sehemu ya kucheza tu na kupagawisha mashabiki wake. Angalia video za ngoma zake utaniamini. Pia, Ray C alikuwa bonge moja la mtoto wa kike. Pisi ya kwenda. Jicho legelege, bodi kinanda mpaka muda mwingine nawaza usikute zile nyimbo za Wasafi za kusifia wanawake huwa wanamuimbia Ray C.

Lavalava anaimbaga ‘mtoto mjojo, sijui nini na nini, jicho kama anasikia usingizi, blaa blaaa, kiuno kama nyungunyungu’... hizo ni sifa anazotakiwa kupewa Ray C kabisa. Na kama hujui moja ya kigezo cha kuwa msanii ni kuwa pisi kali kama ni msanii wa kike, na kuwa HB kama wa kiume na kama hutaki sikulazimishi, lakini nina uhakika umeshawahi kusikia neno ‘mwonekano wa kisanii’.

Na ukimchukua meneja yeyote wa wasanii wa muziki na filamu ukamwambia achague msanii mmoja kati ya hawa wawili; kwanza anayeimba sana, lakini mwonekano wa kawaida, na wa pili anayeimba sana na mwonekano mzuri, lazima atachagua wa pili.

Nawaza kwa msanii ambaye ni ‘full package’ kama alivyokuwa Rehema. Msanii ambaye anajua kuimba, ana damu ya hit song, ni performer mzuri na pia ni pisi kali ingekuwaje kama angekuwa anafanya muziki katika kipindi hiki cha mitandao ya kijamii? Nina uhakika Ray C angekuwa habari kubwa zaidi.

Ninachojaribu kusema ni kwamba naamini mpaka leo hakuna msanii wa kike Tanzania anayemzidi Ray C kwa kuwa ‘full package’. Yaani ni ngumu sana kupata mtu wa kutusahaulisha Rehema Chalamila.