Mzimu wa penzi la Whitney na Bobby unavyomtesa Harmonize

Saturday April 02 2022
harmonize pic
By Peter Akaro

MWAKA 2008 aliyekuwa mume wa Whitney Houston, Bobby Brown katika waraka wake uitwao; The Truth, The Whole Truth and Nothing But, alidai kuwa Whitney aliamua kufunga ndoa naye ili kujisafisha baada ya kuandamwa na kashfa ya kuwa na uhusiano wa jinsia moja na msaidizi wake, Robyn Crawford.

Whitney, mwimbaji wa RnB, Pop na Soul aliyekulia kwenye kanisa la New Hope Baptist huko Newark, Marekani, kwa miaka yote alikanusha jambo hilo, pia mama yake, Cissy Houston ambaye ni mwimbaji wa Injili alijitokeza kumtetea.

Hata hivyo, Robyn Crawford katika kitabu chake, A Song for You: My Life with Whitney Houston anakiri kuwa uhusiano wake na Whitney ulianza mwaka 1982 kabla ya mwimbaji huyo kusainiwa na lebo ya Arista Records.

harmonize pic 1

Brown na Whitney walikutana mwaka 1989 katika tuzo za Soul Train Music Awards, walifunga ndoa Julai 18, 1992 na kujaliwa mtoto mmoja, Bobbi Kristina Brown aliyezaliwa Machi 4, 1993 na kufariki Julai 26, 2015 baada ya kupoteza fahamu kwa miezi sita kutokana na matumizi ya dawa za kulevya na zile kupunguza mfadhaiko.

“Nafikiri tulifunga ndoa kwa sababu zote mbaya, sasa natambua Whitney alikuwa na agenda ya kusafisha sura yake, wakati yangu ilikuwa ni kutaka kupendwa na kupata watoto, Whitney aliamini kuolewa kungemuondolea kashfa hiyo,” alisema Brown.

Advertisement

Brown ambaye ni mwanamuziki wa miondoko ya New Jack Swing, naye alikuwa akitupiwa lawama kuwa ndiye alimuingiza Whitney katika matumizi ya dawa za kali za kulevya. Hata hivyo, alikanusha hilo na kueleza alimuona Whitney akitumia dawa za kulevya kwa mara ya kwanza siku ya harusi yao ingawa naye aliwahi kukamatwa kwa matumizi ya dawa hizo.

Ikumbukwe Whitney Houston aliyetamba pia na filamu kama The Bodyguard (1992), Waiting to Exhale (1995) na The Preacher’s Wife (1996), alifariki Februari 11, 2012 katika mji wa Los Angeles nchini Marekani akiwa na umri wa miaka 48. Mwili wake ulikutwa kwenye sinki la kuogea katika chumba cha Hoteli ya Beverly Hills, huku matumizi ya kupindukia ya dawa za kulevya yakitajwa kusababisha kifo chake.

Kwa ufupi Brown na Whitney wanatoa picha ya mambo mawili, mosi; wanawakilisha kundi kubwa la watu maarufu katika muziki ambao kwa nje muda mwingine huonekana kama wana furaha lakini ndani mambo huwa kinyume, jambo lanalokuja kubainika baada ya utengano.

Pili; wanatoa funzo kuwa watu wengi katika tasnia hiyo huingia katika uhusiano au ndoa kwa lengo lingine tofauti na mapenzi kama inavyoonekana kwa nje. Biashara, kusaka umaarufu, kujisafisha dhidi aina fulani ya tuhuma na mengineo vinatajwa kuchochea hilo kwa kiwango chake.

Staa wa Bongofleva kutoka Konde Music Worldwide, Harmonize anaweza kuingia katika mambo hayo mawili kwa kile kinachoendelea sasa katika uhusiano wake na ule aliopitia katika ndoa yake na mrembo wa Kizungu kutoka Italia, Sarah ambaye walioana Septemba 7, 2019 baada miaka mitatu ya uchumba.

Mapema wiki hii, Harmonize ameeleza kuwa watu wanaweza kumuona mwenye furaha lakini sivyo, yote kisa mapenzi!. Anatamani kuiona familia yake inarejea katika himaya yake, familia hii inadaiwa ni Kajala na binti yake, Paula ambao alikuwa akiishi nao kabla ya mvurugano ulitokea baina yao hadi kufikishana polisi.

Kauli ya Harmonize inakuja baada ya kuachana na mrembo toka Australia, Briana ambaye alimtambulisha kwa mashabiki wake Novemba 15, 2021 wakati akiendelea na ziara yake ya kimuziki nchini Marekani.

Novemba 27, 2021 Briana aliwasili Tanzania akiwa na Harmonize wakitokea Dubai, lakini kufika usiku wa Machi 30, 2022 Briana alithibitisha kuachana na Harmonize ikiwa ni takribani miezi mitano ya penzi lao katika uso wa dunia, huu ni uhusiano wa pili wa Harmonize uliodumu kwa kipindi kifupi zaidi.

Ikumbukwe kabla ya Briana, Harmonize alikuwa na uhusiano na Kajala ambao ulianza Februari 2021, na kufika Aprili 2021 ikiwa na mwezi mmoja tu wa penzi lao, wakaburuzana kituo cha polisi ambako Kajala alikuwa akituhumiwa kusambaza picha za utupu za Harmonize akishirikiana na binti yake, Paula ambaye alikuja kuingia katika uhusiano na hasimu wa Harmonize wa kimuziki, Rayvanny.

Kwa mujibu wa Harmonize akiongea na wanahabari, Novemba 19, 2021 kwenye Uwanja wa Ndege Dar es Salaam (JKIA), alisema inafikia hatua anaogopa kuingia katika uhusiano na wanawake nchini maana anaona watumiwa na mahasimu wake kummaliza. Na hilo ndilo hasa lililomsukuma kuwa na Briana, uhusiano ambao haukufua dafu.

Hapa Harmonize anavaa viatu vya Brown na kumuona Kajala kama Whitney aliyeingia katika penzi lake kwa lengo jingine tofauti na mapenzi, hiyo ni baada Kajala kuwa upande wa Rayvanny ambaye ameingia katika uhusiano na binti yake, Paula.

Ikumbukwe tangu ameondoka WCB, Harmonize na Ravanny wamekuwa hawaelewani, hivyo akahisi kuwa Kajala huenda alitumika na watu toka timu ya Rayvanny kwenda kwake kwa lengo la kumchafua na kumshusha kimuziki. Hiyo ni baada ya kusambaa kwa video za aibu zinazodaiwa kuwa zake na nyingine akimtongoza Paula. Kusambaa kwa video hizo ndipo Harmonize akawapeleaka polisi Kajala, Paula na Rayvanny.

Utakumbuka kabla ya Kajala, Harmonize alikuwa na Sarah ambaye baadhi ya watu walidai ndiye aliyekuwa akimpa kiburi cha fedha na ndiye aliyefanikisha mpango wa kujitoa WCB ambako anadai alilazimika kulipa Sh600 milioni. Ikumbukwe hawa walifunga ndoa wakati tetesi za Harmonize kuachana na lebo hiyo zikiwa ndio zinachomoza.

Jambo hilo lilikanushwa na Harmonize na tunaweza kulipima kwa muda ambao ndoa yao ilidumu. Walioana Septemba 2019 na kuachana Desemba 2020 ukiwa ni mwaka mmoja tu wa ndoa na hapo tayari Harmonize alikuwa kashatoka WCB. Sarah ndiye alitangaza kumuacha Harmonize kwa madai ya kuzaa nje ya ndoa yao, madai ambayo Harmonize alithibitisha ni kweli.

Lakini hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa mapenzi yao kukumbwa na madai ya usaliti, Agosti 2018 iliibuka kashfa mbaya zaidi kuwa Sarah alichepuka na mlinzi wa Diamond kwa wakati huo, Mwarabu Fighter, licha ya Sarah kukanusha vikali hilo, Mwarabu alijikuta akifutwa kazi WCB.

Hiyo ni sawa na ndoa ya Brown na Whitney ambayo nayo iliandamwa na madai ya usaliti, lakini katika mahojiano na Oprah Winfrey, Whitney alikanusha madai ya kuisaliti ndoa yake.

“Sijawahi kudanganya na kuchepuka, sijawahi kufanya jambo hilo,” alisema Whitney ambaye kupitia wimbo wake, I Will Always Love You, anashikilia rekodi ya wimbo uliouza zaidi duniani kwa muda wote (Best-selling singles of all time)

Ikiwa ni kweli Harmonize alifunga ndoa hiyo na Sarah ili kumsaidia kufanikisha mpango wa kujitoa WCB, basi Sarah naye anavaa viatu vya Whitney na kumtazama Harmonize kama Brown aliyekuja kwake kimikakati zaidi. Ikumbukwe wakati Brown anamuoa Whitney mwaka 1992 alikuwa na umri miaka 23 wakati Whitney akiwa na miaka 29, kwa tofauti hiyo umri, inaamini sio tu mapenzi yalimpeleka Brown kwa Whitney bali kula matunda ya umaarufu wa Whitney ambao alinufaika nao kwa kipindi cha miaka 15 ya ndoa yao.

Advertisement