MUSIC FACTS: Rama Dee alivyoibeba albamu ya Professor Jay

Muktasari:
- Mkali huyu alisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Iringa ili kurekodi nyimbo zake ‘Sarah’ na ‘Kikao cha Family’ zilizofanya vizuri, na hadi sasa ametoa albamu na kushinda tuzo ya muziki Tanzania (TMA) 2013 kama Msanii Bora wa RnB. Fahamu zaidi.
NI wazi kuwa sauti yake, melodi, uandishi na swaggs zake katika uimbaji ni kati ya mambo yanayofanya Rama Dee kuwepo katika orodha ya waimbaji wakali wa RnB Bongo kwa muda wote.
Mkali huyu alisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Iringa ili kurekodi nyimbo zake ‘Sarah’ na ‘Kikao cha Family’ zilizofanya vizuri, na hadi sasa ametoa albamu na kushinda tuzo ya muziki Tanzania (TMA) 2013 kama Msanii Bora wa RnB. Fahamu zaidi.
1. Rama Dee ambaye amekuwa akifanya vizuri katika chorus za nyimbo nyingi za Hip Hop, chorus yake ya kwanza aliifanya na kundi la Mapacha (Maujanja Saplayaz) kupitia wimbo wao, 50/50.
2. Joh Makini ndiye rapa ambaye Rama Ree amefanya naye kolabo nyingi zaidi, Rama Dee alimjua Joh Makini kupitia kundi la Mapacha, na kupitia Joh Makini ndipo akawajua Nikki wa Pili na G Nako.
Hadi sasa Rama Dee na Joh Makini kutoka kundi la Weusi wameshirikiana katika nyimbo kama Sina Time, Furuha Yetu, Tomorrow n.k.
3. Kama asingekuwa mwanamuziki, basi Rama Dee angekuwa mcheza soka, hiyo ni sawa na Rich Mavoko, Alikiba, Young Killer, Tundaman na Ruby aliyewahi kuichezea Young Twiga Stars.
4. Wasanii wa Hip Hop Bongo ambao Rama Ree anawakubali ni Joh Makini, Bonta, Fid Q, G Nako na Nikki wa Pili ambaye kupitia wimbo, Good Boy walioshirikiana ndipo rapa huyo akawa maarufu zaidi Bongo.
5. Rama Dee alijiunga katika harakati za Antivirus na kushiriki katika albamu, Antivirus Vol. 3, lengo lake lilikuwa ni kupunguza ukali wa waneno kutoka katika nyimbo zilizokuwa zinatolewa na vuguvugu hilo ambalo lilitaka mabadiliko katika mfumo wa muziki nchini.
6. Kwa mujibu wa Soggy Doggy, wasanii wake bora wa RnB Bongo kwa muda wote ni Rama Dee na Nuruelly na Belle 9, kumbuka Soggy ana sikio la muziki sana, alishafanya Bongo Records akiwa kama msaidizi wa P-Funk Majani.
Ikumbukwe Soggy na Bizman ndio wametengeneza mdundo wa wimbo Bushoke ‘Mume Bwege’ na kurekodi ndani ya Bongo Records, pia amehusika katika wimbo wa Afande Sele, Darubini Kali.
7. Rama Dee ndiye alitakiwa kusikika kwenye chorus ya wimbo wa Nikki Mbishi ‘Punchline’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Sauti ya Jogoo (2011) ila ikashindikana na nafasi hiyo akapewa Grace Matata.
8. Sauti ya Rama Dee ndio inasikika mwanzoni mwa wimbo wa Professor Jay, J.O.S.E.P.H (2006), Rama Dee na wenzake ndio waliimba chorus ya wimbo huo uliobeba jina la albamu ya tatu Jay ingawa hawajatajwa kushirikishwa.
9. Rama na Lady Jaydee kwa mara ya kwanza walikutana Marekani na kujadiliana kuhusu wimbo wao ‘Suluhu’ na waliporejea nchini ndipo wakaumalizia wimbo huo ambao unapongeza utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
10. Lady Jaydee ndiye mwanamuziki wa kike ambaye amefanya kolabo nyingi zaidi na Rama Dee, ukiachilia ngoma za hapo awali, wameshirikiana katika albamu yao, Love Sentence (2023) yenye nyimbo 10 ikiwa ni albamu ya tisa kwa Jide tangu ametoka mwaka 2000.