Ukweli Konde Boy, Kajala kurudiana

Muktasari:
- Mashabiki wa nyota hao wameshindwa kuelewa iwapo wawili hao wamerudiana kweli au wanazuga kwani hakuna ambaye amekuwa tayari kuweka wazi jambo hilo, ingawa katika 'birthday party' hiyo ya mwaka mmoja wa kuzaliwa wa mtoto huyu Amara, walionekana wakiwa katika mahaba mazito.
PAMOJA na kuonyesha kila dalili ya kurudiana kwa mastaa wa Bongo Fleva, Harmonize a.k.a Konde Boy na wa filamu, Kajala Masanja, katika sherehe ya kuzaliwa mtoto wa Marioo na Paula iliyofanyika juzi, jijini Dar es Salaam, wawili hao wamewaacha wengi njiapanda kwa kutokujua yaliyomo yamo au la!
Mashabiki wa nyota hao wameshindwa kuelewa iwapo wawili hao wamerudiana kweli au wanazuga kwani hakuna ambaye amekuwa tayari kuweka wazi jambo hilo, ingawa katika 'birthday party' hiyo ya mwaka mmoja wa kuzaliwa wa mtoto huyu Amara, walionekana wakiwa katika mahaba mazito.
Mwanaspoti lililokuwa katika sherehe hiyo, lilibahatika kuongea na wawili hao kwa nyakati tofauti kujua undani wa suala hilo na kila mmoja alisema yake;
Kwa upande wa Kajala huku akiwa anacheka, alikana kuhusu kurudiana na Harmonize na kukiri wamemaliza tofauti zao na wanaishi kama marafiki.
"Sikia nikwambie mwenzangu, haya mambo hayazungumziki hadharani (kicheko) ila sijarudiana na Harmonize, lakini tumesameheana kwa kuishi kama marafiki na aombaye msamaha husamehewa hata vitabu vya dini vinasema kuhusu neno kusamehe.

Hivyo potelea pwete vitu vingi vya ajabu vilitokea huko nyuma kati yangu na Harmonize, ila sikufikiria wala kuwaza kama anaweza akawa mkarimu tena kwangu na kwa familia yangu," alisema Kajala.
Kuhusu kuonekana wakipigana mabusu, kukumbatiana na kukaa pamoja meza moja kukiwa na stori pia amempa Harmonize masharti ya usiri wa penzi lao, alisema;
"Kwa mazingira tuliyokutana kwenye sherehe ya mjukuu wangu Amara, ni siku ya furaha sana na kufika tu kwake Harmonize ni furaha kwani wapo tuliowaalika na hawakuja na kwa namna yoyote lazima mtu urudishe moyo nyuma na kuacha mambo mengine yaendelee na kujikuta mnarudisha uhusiano wenu.
Hata kama tukiwa tumerudiana kuna mambo ambayo hatutakiwi kuyafanya kama ilivyokuwa mwanzo, kutakuwa na mabadiliko sana ila kwa sasa tuishi humu, kwa hiyo ishu ya kurudiana au kutorudiana kama ipo tutaitangaza sisi wenyewe hizo au hao wanaosema ni mashabiki zetu tu wanaopenda iwe hivyo.

"Kwa upande wa suala la kumpa masharti Harmonize ya kufanya siri kurudiana kwetu, sidhani kama kuna mapenzi ya siri hata iweje yatagundulika na kwa Harmonize mnavyomjua mngeshajua kitambo wala asingekuwa analialia kila kukicha," alisema Kajala huku akiwa anacheka.

Kwa upande wa Harmonize kuhusu kurudiana na Kajala, alisema;
"Hakuna swali linaloniumiza kama hili la umerudiana na Kajala, sababu Kajala ni mwanamke ninayempenda sana na natamani kurudiana naye ila kwa sasa bado hatujarudiana, tunaishi tu kama marafiki wa karibu.
"Kwanza kuongea tu na Kajala na familia yake ni jambo kubwa sana kwangu zaidi ya hilo swali la kurudiana ninaloulizwa kila wakati na watu," alisema Harmonize.

Kuhusu kurudiana kisirisiri tangu mwaka jana na masharti aliyopewa na Kajala la kutotangaza, alisema;
"Dah, jamani onyo tena? Hivi kuna mapenzi ya siri kweli hasa kwa sisi wasanii maarufu? Mie naomba watu waelewe sisi ni washikaji kama yakitokea ya mambo ya kurudiana mie nitasema tu jamani, ila ukweli upo hivyo."
Uhusiano wa wawili hao ulivunjika baada ya video ya Harmonize kuvuja akiwa anamtongoza mtoto wa Kajala, Paula, kabla ya hivi karibuni kuonekana wakiwa karibu kimahaba, ingawa wamekuwa wakikanusha ikiwamo Kajala kuliambia Mwanaspoti hataki kusikia tena habari za Harmonize katika maisha yake .