Msanii maarufu kutoka India aahidi uwekezaji Tanzania

Monday November 08 2021
Dutt PIC
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Muigizaji maarufu kutoka nchini India, Sanjay Dutt yupo nchini Tanzania toka Jumamosi ya Novemba 6, 2021 na kueleza dhamira yake ya kuwekeza nchini hapa.

Dutt ni kati ya wasanii waliojizolea umarufu duniani tangu mwaka 1980 alipotia miguu katika tasnia hiyo ambapo amewahi kutesa na filamu mbalimbali ikiwemo Jeete Hain Shaan Se, Mardon Wali Baat , Ilaaka,  Hum Bhi Insaan Hain, Kanoon Apna Apna  na pia kuwahi kupata  tuzo  kama muigizaji Bora  mwaka 1991 na mwaka 19993.

Dutt amepata fursa ya kufanya mkutano na waandishi wa habari mara baada ya kupokelewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa uwanja wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Dutt amesema Tanzania ni moja ya nchi anazozipenda na anaona fursa nyingi ndani yake na kueleza kuwa atakuja kufanya uwekezaji siku moja.

"Tanzania ipo ndani ya moyo wangu, nitakuja kuwekeza hapa siku moja, kwa kuwa ni nchi nzuri na salama, kwa uwekezaji" amesema.

Naye Waziri Bashungwa alimkaribisha msanii huyo na kueleza ujiio wake utakuwa na manufaa mengi kwa watanzania sio tu katika masuala ya biashara bali na kwenye tasnia ya filamu na masuala ya kutangaza utalii kwa ujumla.

Advertisement

Waziri huyo amesema katika kipindi ambacho Dutt atakuwa nchini  hapa atapata wasaa wa kukutana  na wasanii wa filamu kuzungumza nao njia alizopitia hadi kufikia mafanikio aliyo nayo leo.

Wakati Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dk Kilagho Kilonzo amesema kupitia ugeni huo wasanii wa filamu wanapaswa kuiona thamani yao kuwa sio watu wadogo kama wanavyofikiria kwani msanii mkubwa kama huyo kuja nchini ameona kuna kitu kwa wasanii wa Tanzania.

Mmoja wa wasanii wa filamu, Halima Yahaya maarufu Davina amesema anafurahi kukutana na msanii ambaye alikuwa akimtazama tangu akiwa mdogo na hajafikiria kama naye angekuwa msanii na kushauri wasanii kumtumia vizuri katika kuendeleza kazi zao na kuitangaza tasnia hiyo nje ya nchi.

Advertisement