Mr Blue: Kwa sasa mambo yamebadilika

MKALI wa muziki wa HipHop, Khery Sameer 'Mr Blue' amesema miaka ya nyuma wasanii walikuwa wanaimba muziki kutokana na mikasa wanayokutana nayo tofauti na sasa.

Mr Blue ameliambia Mwanaspoti kuwa kuna utofauti mkubwa wa muziki wa kizazi chake na muziki wa sasa huku akitaja mashairi kuwa ya sasa hayana ujumbe wa maana na wa kuelimisha au kuzungumzia maisha ya uhalisia.

“Mimi naweza kukutajia baadhi ya mashairi ambayo ni maisha yangu halisi kama wimbo wangu wa Baki na mimi ushauri wa ilikuwa Jumapili mchana nilikutana na msichana nikiwa kwenye harakati za kuchana," alisema Mr Blue na kuongeza;

“Shairi hilo ni uhalisia mke wangu nilikutana naye Jumapili mchana nakumbuka ilikuwa birthday ya dada yake walikuwa billcanass na mimi nilikuwa hapo kwenye mihangaiko yangu ya kazi.”

Alisema muziki wa sasa huwezi kukuta kitu kama hicho kwani  wasanii wanaimba kutokana na namna wanavyojisikia muziki wa aina hiyo ndio uliopo na ndio maana haudumu.

Mr Blue alisema aliamua kuimba hivyo ili kutoa ujumbe kuwa mke mzuri sio lazima apatikane kanisani popote anaweza kupatikana kama yeye alivyompata mzazi mwenzake ambaye amekiri kuwa walianza kama marafiki hadi sasa ni mke na mume.