Mlela afuta kauli ya kutaka mishangazi

Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Mlela alisema kuoa ni kudra za Mungu, japo alishawahi kutamka kwamba ukifika muda wa kuoa basi angechukua lishangazi la maana lililomzidi umri akiamini lingemtuliza akili na kudumu katika ndoa yake kwa muda mrefu kuliko vichenchede, lakini kwa sasa ameahirisha mpango huo kwa kusema hana mpango wa ndoa tena.
STAA wa Bongo Movie, Yusuf Mlela ametangaza kufuta kauli aliyowahi kuitoa ya kutaka kuoa mwanamke aliyemzidi umri maarufu kwa sasa kama mshangazi na kusema kwa sasa wala hana mpango wowote wa kufunga ndoa, kwani anaweza hata asioe kabisa.
Akizungumza na Mwanaspoti mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Mlela alisema kuoa ni kudra za Mungu, japo alishawahi kutamka kwamba ukifika muda wa kuoa basi angechukua lishangazi la maana lililomzidi umri akiamini lingemtuliza akili na kudumu katika ndoa yake kwa muda mrefu kuliko vichenchede, lakini kwa sasa ameahirisha mpango huo kwa kusema hana mpango wa ndoa tena.
“Kusema kweli kwa sasa nimefuta wazo hilo la kuoa na inawezekana hata nisije kuoa kabisa,” alisema Mlela anayekimbiza kwenye fani hiyo uigizaji kuanzia kwenye filamu hadi tamthilia.
Mwigizaji huyo alisema katika malengo aliyojiwekea kwa mwaka 2024 ameona amefanikiwa baadhi ya asilimia zilizobaki anajipanga kumalizia mwakani, kwani kwa sasa ataongopa kama ataweza kutimiza alivyotaka.
“Katika kumalizia mwaka huu nimepanga kufurahia kwa kutoka na washikaji zangu kwenda kutalii mbuga za wanyama za Ngorongoro na Serengeti, kwani huu ndio muda wangu wa kupumzika kabla ya kuanza kuchakarika kutimiza malengo ninayoyahamishia 2025,” alisema Mlela.
Mlela katika maisha yake ya kisanii amecheza zaidi ya filamu 50 zikiwamo Red Cross, Angel, Red Mzula, Lonely Heart, Talaka Yangu, Promoter, Tough Life, Diversion of Love, Rubi, The Taxi Driver in Love, Continuos Love, Payback, War Against Men, War Against Women, Chumo, Pete ya Ajabu na The Romantic.
Nyingine ni; The Avenger, Sound of Death, Best Man, Mtumwa, Love is War, Time Goes Around, Black Sunday, Secretary, Money Desire, Last Minutes, Its Too Late, Divorce, April Fools, Why Did I Love, Lost, Miracle Love, Happy Couples na Round.