Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mke aelezea ugonjwa, kifo cha King Kikii

Muktasari:

  • King Kikii alifariki dunia usiku wa kuamkia Ijumaa Novemba 15, 2024 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

KUTOKANA na kifo cha mwanamuziki mkongwe wa Muziki wa Dansi Tanzania, Boniface Kikumbi ‘King Kikii’, mkewe, Constansia Kalanda amefunguka namna mume wake alivyougua hadi kufariki dunia.

King Kikii alifariki dunia usiku wa kuamkia Ijumaa Novemba 15, 2024 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

“Mzee King Kikii alifanyiwa oparesheni ya pingili za shingo, hapo ndipo ugonjwa wake ulipoanzia na kusababisha kukaa kimya kwa zaidi ya miaka sita,” alisema Constansia na kuendelea.

“Oktoba 30 mwaka huu, alilazwa katika Hospitali ya Muhimbili, baada ya muda tukaona arudi nyumbani. Tulivyorudi nyumbani alikaa vizuri lakini sio kwamba alikuwa vizuri sana. Alhamisi (Novemba 14 mwaka huu) tuliamka tukamuogesha, akasema anataka kulala, lakini cha ajabu tukaona mtu anakula sana kitu ambacho hapo awali hakuwa mlaji.

“Wakati hayo yakijiri binti yake Jesca alikuwa hapa na kaka yake Joseph, kwa hiyo siku nzima walishinda naye, ilipofika jioni nikaingia ndani nikamuuliza mbona kama una joto sana? Akasema hapana, akataka nimgeuze, nikaita kijana akamgeuza, lakini kutokana na joto Jesca na kaka yake Joseph wakasema ngoja tumpe dawa, wakampa, lakini akawa hataki kuimeza.

“Mimi ni mtu mzima, nikamwambia tema, akatema nikaipokea lakini watoto wakasema lazima anywe dawa, kwa hiyo wakaisaga tukampa kwenye kijiko ila hali yake ilikuwa mbaya, homa ilikuwa joto 38, haishuki, basi nikachukua kitambaa nikamkanda.

“Tulikuwa na mchungaji, maana mimi nilikuwa sibagui wachungaji na mashekhe walikuwa wanakuja kumwombea.

“Mchungaji alivyomaliza nikamwambia basi muache mchungaji aondoke akasema hapana, akasisitiza “asiondoke asiondoke”, tukaheshimu sauti yake, tukawa tumekaa na watatoto.

“Saa 5 usiku, mimi nikawa nimelala naye pale kitandani japo watoto wakawa hawataki nikae pale kutokana na mimi kuwa na tatizo la presha, sikutaka watoto wajue ile hali anayopitia baba yao, lakini walinitoa wakaniambia nikapumzike ndani, nikawaridhisha nikaenda ndani.

“Nikiwa huko nikawa nasali, ghafla nikasikia sauti kama mtu kalia mara moja, kaka yake Jesca ambaye ni Joseph akaniambia nitulie tu wanampeleka baba hospitali, lakini nilipoingia ndani kwa baba yao nikakuta wametoa godoro, nikawauliza mbona mnampeleka na godoro?”

“Jesca alishindwa kujikaza, akaanza kulia, hadi kufikia hapo nikajua nini kinaendelea, lakini mapema tu nilijua tu leo (juzi) kama akilala ni Mungu tu.”

Kuhusu idadi ya watoto alioawaacha King Kikii, Constansia anabainisha kwa anavyofahamu wapo watatu na wawili amezaa naye na mmoja alimkuta.

“Idadi ya watoto sijajua ila kama mnavyojua wanamuziki,  hiyo ni siri yake mwenyewe marehemu,  kuhusu wake, najua ana mke mmoja wa ndoa ambaye ni mimi na nimezaa naye watoto wawili ambao ni Jesca na Zitah, ambaye ni mtoto wetu wa mwisho na Joseph ni mtoto wake wa kwanza niliyemkuta naye, mengine ni maelezo ya ndani ya familia,” alisema Constansia huku akifichua Bendi ya La Capital iliyokuwa chini ya King Kikii ilikufa baada ya mwenyewe kuanza kuumwa.

Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu aitwaye Joseph, mwili wa King Kikii unatarajiwa kupumzishwa katika nyumba yake ya milele kesho Jumatatu, Novemba 18, 2024, jijini Dar es Salaam.