Misiba ya watu mashuhuri 2020

Tuesday December 29 2020
kwa heri 1
By Kelvin Kagambo

KUSEMA kwaheri haijawahi kuwa rahisi hususan kwa watu mashuhuri waliokuwa wanatembea na mioyo ya mashabiki. Hata hivyo, asili ya maisha inatulazimisha kusema kwaheri kwa watu tunaowapenda kama ambavyo tumelazimika kusema kwaheri kwa watu maarufu waliotangulia mbele ya haki ndani ya mwaka huu.

Lakini, uzuri ni kwamba, mastaa wanapotangulia mbele za haki mashabiki wanabaki na fursa ya kushereherekea mazuri yaliyofanywa nao na kutukuza urithi wa matokeo makubwa yaliyoachwa na sanaa waliyokuwa wanaifanya mastaa husika. Na kwa sababu hiyo, tukiwa tunaelekea kufunga mwaka, Mwanaspoti tunawakumbuka na kuwaenzi watu maarufu au wanaohusiana na watu hao waliofariki mwaka huu.

JENGUA

Wapenzi wa filamu na tamthilia Tanzania hawataisahau Desemba 15, siku ambayo walimpoteza muigizaji nguli wa filamu na tamthilia, Mohamed Fungafunga maarufu Jengua.

Jengua alipoteza maisha akiwa Mkuranga mkoani Pwani kwa mwanaye wa kike alikokuwa akiuguzwa, na mwili wake ulisafirishwa kuletwa Dar es Salaam kwa ajili ya kuzikwa kwenye makaburi ya Mburahati Mianzini, huku presa ikitajwa kuwa chanzo cha kifo chake.

Gazeti hizi lilipata nafasi ya kuzungumza na wasanii na watu maarufu wengi waliofika kwenye mazishi hayo. Na wengi walikiri kwamba mzee Jengua alikuwa ni mwigizaji wa aina yake na huenda itapita miaka mingi mpaka tasnia hii kupata mtu ambaye atakuwa akicheza nafasi za baba mkatili, mkali, mwenye roho mbaya na akavaa uhusika kwa kiwango cha juu kama ilivyokuwa kwa Jengua.

Advertisement

Jengua aliumaliza mwendo huku historia ya sanaa ya maigizo ikimtambua kama mmoja wa wasanii wachache wa Tanzania waliodumu kwenye sanaa hiyo kwa zaidi ya miaka 40 wakiwa pia na ustaa wao uleule.

MABERA

Dah! Wakati mwili wa mtaalamu wa kucharaza gitaa la solo, Saidi Mabera unapelekwa kwenye makazi yake ya milele, ungetamani kusikia palepale kikipigwa kibwagizo maarufu cha Mabe, Mabe, Mabe, Maberaaaa; ili kutoa heshima ya mwisho kwake.

kwa heri pc2

Mabera alifariki Septemba 28 nyumbani kwake Goba jijini Dar es Salaam huku mwanaye, Mabera Junior akilithibitisha gazeti hili kwamba chanzo cha umauti wa wake ilikuwa ni presha.

Historia ya muziki itamkumbuka Mabera kama shujaa aliyetumia mikono kwa ajili ya kuwaburudisha wapenda muziki kwa zaidi ya miaka 50. Na hata ndani ya bendi aliyokuwa akitumikia ya Msondo Ngoma alikuwa ndiye msanii mkongwe zaidi aliyebaki, wengine wote walishatangulia mbele za haki.

MC ZIPOMPAPOMPA

Wapenzi wa Bongo Movie watamkumbuka mwanamama huyu kwa ule uhusika wake aliokuwa anaigiza kwenye tamthilia ya Slay Queen wa Madam Tety. Lakini kwa upande wa wasanii, wengi wameeleza kuwa Mc Zipompapoma alikuwa ni kama mama kwao.

kwa heri pic 3

Zipompapompa ambaye jina lake kamili ni Gladness Chiduo alifariki dunia Novemba 10 jijini Dar es Salaam na kuzikwa mkoani humo ambapo msiba wake ulihudhuriwa na wadau wengi wa tasnia mbili - uigizaji pamoja na washereheshaji.

MENEJA WA RUBY

Hamish Donovan ndilo jina analofahamika sana. Jamaa aliwahi kuwa meneja wa msanii mwanamuziki Ruby, lakini pia aliwahi kuwa moja ya sehemu ya waandaji wa Tamasha la Wasafi Festival.

Mbali na hivyo pia Hamish alikuwa anajihusisha sana na kuleta wanamuziki wa nje ya Bongo kwa ajili ya kuja kupiga shoo hapa nchini, lakini ndani ya mwaka huu ndiyo amekamilisha kibali chake cha kuwepo duniani.

Hamish alizikwa Desemba 12 na inaripotiwa kuwa kifo chake kilitokana na ajali ya gari aliyoipata jijini Dar es Salaam.

MKE WA BABU TALE

Moja ya misiba ya watu mashuhuri Bongo iliyogusa mioyo ya watu wengi Tanzania ilikuwa ni kifo cha mke wa meneja wa Dimond, Hamis Taletale maarufu Babu Tale.

Mke wa Babu Tale aliyefahamika kwa jina la Shammy alifariki dunia Juni 28 akiwa hospitali ambao alikuwa amelazwa na kumuachia Babu Tale jukumu la kulea watoto watatu

Shammy alizikwa Morogoro na mazishi yake yalihudhuriwa na watu wengi mashuhuri.

Enzi za uhai wake Shammy alikuwa akijihusisha na shughuli za kusaidia jamii kupitia taasisi yake ya Nasimama nao.

MNGEREZA

Godfrey Mngereza amefariki dunia wiki hii akiwa Dodoma ambapo taarifa zinaeleza kuwa alikwenda kikazi.

kwa heri 4 pic

Mngereza alikuwa ni katibu mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na anatajwa kuwa mmoja wa viongozi waliokuwa na uhusiano mzuri na wasanii wa Bongo, licha ya kwamba baraza hilo linafahamika pia kwa kuwafungia kazi.

MAMA WA MC PILI

Mchekeshaji Emmanuel Mathias maarufu Mc Pilipili alipata pigo dabo baada ya kumpoteza mama yake mzazi pamoja na mama yake mdogo mwezi huu katika ajali ya pikipiki.

Mbaya zaidi msiba huo ulitokea siku ambayo mdogo wake na Mc Pilipili alikuwa anaoa. Mwili wa mama huyo ulisafirishwa kwenda Dodoma kwa ajili ya mazishi.

Na enzi za uhai wake mama huyo alikuwa akionekana kupitia Instgram ya Mc Pilipili kwani yeye na mtoto wake walikuwa karibu kupita maelezo.

Advertisement