Miaka 20 Juma Nature katika muziki bila tuzo

ALIKUJA na mtindo wa uandishi kutoka uswazi, ameshirikishwa sana na wasanii hasa upande wa ‘chorus’ katika utumishi wake wa miaka zaidi ya 20 ndani ya Bongo Fleva na ametengeneza himaya yake ya kuheshimika.

Juma Nature kutokea TMK ametoa albamu tano ambazo ni Nini Chanzo (2001), Ugali (2003), Ubinadamu Kazi (2005), Zote Historia (2006) na Tugawane Umaskini (2009). Fahamu zaidi;


1. Wimbo uliomtoa Nature ni ‘Kighetogheto’ uliotayarishwa na P-Funk Majini ndani ya Bongo Records lakini huu ni wa pili, wa kwanza (original version) Nature aliurekodi, Sound Crafters kwa Prodyuza Enrico Figueiro.


2. Nature ndiye msanii wa kwanza Bongo kuujaza ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, ni katika uzinduzi wa albamu yake, Ugali yenye ngoma kali kama Ugali, Inaniuma Sana na Staki Demu.


3. Alikuwa anatembea kwa mguu toka Temeke hadi Kijitonyama kuifuata Bongo Records, baadhi ya watu hawakuamini uwezo wake hadi kumwambia P Funk Majani kuwa Nature ni MC Cartoon. Ila sasa historia imeandikwa.


4. ndiye aliyemuingiza Mkubwa Fella kwenye muziki na kuanza kusimamia wasanii kama Meneja wao, Nature alimwomba Fella amsimamie kimuziki na ndipo kazi ya umeneja ikaanza.


5. Prodyuza P Funk alikutana na Madojo na Domo Kaya akiwa kwenye ziara ya albamu ya Nature, Ugali na Nature ndiye aliyewapeleka wasanii hao kwa Bongo Records walipoanzia kuwika.


6. Mkubwa Fella alipata wazo la kuanzisha kundi la TMK Wanaume baada ya wasanii wengi kutaka kumshirikisha Nature katika nyimbo zao maana sauti ya Nature ilikuwa bidhaa inayouzika kirahisi wakati huo.


7. P Funk mwenyewe ndiye aliyemchukua Nature na kumpeleka Bongo Records baada ya kuona uwezo wake kwenye nyimbo alizoshirikishwa na Joint Mobb (Mtani Jirani) na Mabaga Fresh (Mtulize).


8. Kabla ya kutoka kimuziki Nature alifanya shughuli mtaani kama kupasua mawe, kuuza chuma chakavu na kusukuma mikokoteni, hiyo ni sawa Diamond Platnumz aliyeuza mitumba na mafuta katika Petro stesheni.


9. Licha ya kushinda tuzo ya Channel O Music Video Awards 2007, Nature hajawahi kushinda tuzo Bongo, zile za Tanzania Music Awards (TMA), hiyo ni sawa na wakali wengine kama TID, Dully Sykes na Mr. Blue.


10. Nature ndiye msanii wa kwanza Bongo kumilikia gari aina ya Mercedes Benz, ni baada ya kutoa albamu ya Ugali, hiyo ni sawa na Sugu ambaye ndiye msanii wa kwanza kumiliki gari aina ya Honda Accord Inspire baada ya kuachia albamu yake, Nje ya Bongo.