Mfaume: Nimepigwa Russia ila nilichofanyiwa sio kabisa

Sunday April 11 2021
mfaume pic
By Imani Makongoro

Bondia Mfaume Mfaume amerejea nchini leo Aprili 11 na kubainisha kilichomsibu nchini Russia hadi kuchapwa kwa TKO na mwenyeji, Rizvan Elikhanov hivi karibuni.

Ingawa awali kocha wa bondia huyo, Ramadhan Uadi (Rama Jaha) alieleza bondia wake alipewa pambano kwa kustukizwa na hakuwa na maandalizi, Mfaume amesema mazingira ya pambano hilo yalimtoa mchezoni mapema.

"Sikujua mpinzani wangu ana kilogramu ngapi, japo alionekana kuwa na uzani mkubwa zaidi, lakini kwenye fomu yake iliandikwa ana kilogramu 72 na mimi 71, hatukupima pamoja kama taratibu za ngumi zinavyotaka, yeye alipimia kwingine na sikushuhudia," amedai Mfaume.

Bondia huyo amesema kingine kilichomvuruga ni yeye kulipwa asilimia 20 ikiwa ni kinyume na malipo waliyokubaliana awali huku akiambiwa asilimia 80 imekatwa.

"Yote yametokea tayari nikiwa kule, ningejua mapema nisingelikubali pambano hili, kwani nilichokutana nacho Russia sio kabisa na sitokubali kupoteza haki yangu nitapeleka malalamiko yangu kwenye Kamisheni," amedai bondia huyo.


Advertisement

Amesema katika Milioni 10 ambazo walikubaliana kwenye mkataba amepewa Milioni mbili pekee.

"Hivi Milioni 2 au hata tatu, nikicheza hapa nyumbani naipata tena zaidi ya hiyo, cha ajabu mtu niliyekwenda naye Russia baada ya pambano ananiambia pesa yangu imekatwa asilimia 80 eti kwa sababu nimepoteza pambano.

"Sheria za ngumi kote duniai zinajulikana, bondia analipwa kile kilichoandikwa kwenye mkataba, yeye anakuja kuniambia pesa imekatwa asilimia 80, imekatwa na nani hasemi, huku si kutafutiana matatizo tu watu twende jela.

"Halafu nilipomsachi tukiwa kule alikuwa na pesa nyingi zaidi ya zile ambazo alipaswa kulipwa, nikamuuliza hizi pesa umetoa wapi na wakati hakuwa nazo awali hajibu,".

"Mabondia tupo kwa ajili ya kudhurumiwa, ila mimi sitokubali kwenye hili, haki yangu, sikutaka tu kufanya vurugu kule sababu kuna watu wapo kwa ajili ya kuwatafutioa sababu wenzao ili waende jela, lakini haki yangu nitalipwa tu," anasema.

Bondia huyo anasema kingine ambacho amekutana nacho nchini humo ni siku ya pambano lake, alipelekwa ulingoni tofauti na muda.

"Tulipelekwa kula chakula cha mchana saa tisa, tukijua tuna muda wa kutosha wa kupumzika kabla ya kupanda ulingoni usiku, lakini kabla hatujanawa hata mikono baada ya kumaliza kula, tukaambiwa tunapaswa kwenda ukumbini kwenye pambano.

"Fikiria umetoka kula na kushiba, halafu hapo hapo unaambiwa ukacheze tena tofauti na ratiba tuliyoifahamu, walitufanyia vitu vingi vilivyotutoa mchezoni," amedai Mfaume nahodha wa kambi ya Nakos ya Mabibo, Dar es Salaam.

Akizungumzia kipigo cha TKO, Mfaume alisema mbali na kuumia bega, lakini asilimia kubwa kilisababishwa na kutolewa mchezoni mapema.

Promota Jay Msangi ambaye Mfaume ndiye alimtaja kuwa ndiye alitafuta pambano hilo alisema promota ndiye amemkata pesa Mfaume na bondia mwingine, Maono Ally.

"Walionyesha hawakwenda kucheza bali kuchukua pesa tu, hiyo ndiyo sababu," alisema Msangi.

Advertisement