Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MC ELIUD: Bila Sh3 Milioni humpati ng’o!

Muktasari:

  • Miongoni mwa hao ni Eliud Samwel, kijana aliyetokea katika Jiji la Mbeya mpaka Dar es Salaam mwaka 2021, akiwa hana mafanikio wala ajira ambayo inamuingizia kipato na kumpa jina.

MOJA kati ya kazi za sanaa zinazofanywa na watu wengi kwa sasa ni uchekeshaji, ambao kikawaida unaweza ukauchukulia poa, lakini wapo vijana wanaoishi, kuwa umaarufu na kutimiza malengo yao kupitia kazi hiyo.

Miongoni mwa hao ni Eliud Samwel, kijana aliyetokea katika Jiji la Mbeya mpaka Dar es Salaam mwaka 2021, akiwa hana mafanikio wala ajira ambayo inamuingizia kipato na kumpa jina.

Lakini hakuogopa wala kusita bali alijaribu sanaa hii ili kuona kama inaweza kuwa upande wake.


ILIANZA HIVI

Eliud anasema hakuwa na mpango wa kufanya kazi ya kuchekesha na alikuwa na mipango ya kufanya kazi nyingine tu, kama watu wengine wanaofanya kazi ambazo wamezisomea au hawajazisomea.

Mwaka 2020 ndipo alipoanza kutengeneza video ndogo ndogo na kuziposti kwenye ukurasa wake wa Instagram ambapo alikuwa anaongelea mambo ya zamani lakini kwa njia ya kuchekesha.

“Mwaka 2021 siku moja mapema nilipokea simu ya rafiki yangu akiniambia nikashiriki mashindano ya Cheka Tu, ambapo niliomba niwe wa kwanza kuingia ili nishiriki na kuondoka tu.

“Sikuwachekesha majaji, hivyo sikuwa na matumaini ya kushinda kwani ilikuwa ukishinda unaenda Dar es Salaam, ambako ndiko kulikuwa na mashindano makubwa yanayojumuisha watu wote na kambi kwa ujumla,” alisema Eliud.


ALIVYOKUJA DAR

“Wakati mashindano yamefikia mwisho majaji walisema wanataka watu wawili na tulikuwa watatu muda huo, hivyo nilimwambia jirani yangu kuwa yeye aende mimi nibaki.

“Baada ya kusema hivyo moyo wangu ulikuwa na amani na nikaamua kukubali mwenzangu aende akapambanie ndoto zake na mimi nitarudi kwenye maisha ya kawaida, lakini miongoni mwa majaji alisema hapana navunja taratibu na mtaenda wote, hapo ndipo nilipokuja mjini.”

SH50 TU

“Wakati niko mdogo kazi yangu kubwa ilikuwa kutania wenzangu kwahiyo kama mtu ana ugomvi anauleta kwetu mimi na rafiki yangu alikuwa anaitwa Francis,

“Tulikuwa tnalipwa Shilingi hamsini tu ili tumtanie mtu na tukianza mpaka analia, tulikuwa na uwezo wa kucheka viatu vya mtu mpaka akakosa raha.”


ELIMU SASA

“Nilikuja mjini kusoma kwa mara ya kwanza nikiwa naishi kwa dada yangu ambaye ndiye wa kwanza kuzaliwa, nilisoma Chuo cha Utumishi pale Posta nikisomea Teknolojia ya Mawasiliano (IT),”

“Niliamua kusomea kozi hiyo kwa sababu kuna ndugu alinishauri kuwa, kama nitapata elimu hiyo basi ningeweza kufanya kazi Bandarini na malipo yake ni makubwa,

“Lakini cha kusikitisha nilikutana na hesabu hapo ndipo nilipoona kazi ya kusoma kwangu ni ngumu kwani hilo somo na mimi sikuwahi kuliweza tangu elimu ya awali.”


SHOW YA KWANZA

“Show yangu ya kwanza ilikuwa ngumu kwani nilikuwa na changamoto ya kushindwa kupangilia maudhui yangu jambo ambalo lilinihatarishia kubaki kwenye mashindano.

“Lakini rafiki yangu Koi Mzungu aliniita na kunishauri nini cha kufanya ili niweze kufanya vizuri kwa sababu nilikuwa na hadithi nyingi za kuchekesha.”


UGUMU UKO HAPA

“Hizi kazi sio rahisi ila Mungu anasaidia tunazifanya, hakuna jambo gumu kama kumchekesha mtu ambaye ana mawazo usiyoyajua yanahusiana na nini.

“Wapo wanaopanda jukwaani na wasichekeshe, hiyo inakuogopesha wewe unayefuatia na kuna muda wa kumtania mtu kwahiyo ukikosea tu unaweza ukawakasirisha watazamaji (wateja) wote.”


MALIPO YA KWANZA

“Show ya kwanza kuifanya nililipwa Sh300,000 kama sijakosea na niliiona nyingi nikasema nimeongea dakika 10 nimepata mshahara wa mtu wa mwezi mzima.”


KAZI NA FAMILIA

“Mara nyingi watu wananiuliza kwa nini nahusisha familia yetu wakati nachekesha, ila hawaelewi kwamba kwetu vitu vingi vinavyotokea nimegundua ndio vinavyowachekesha watu na kuwakumbusha mambo ya zamani.

“Kuna vitu baba yangu au mama alikuwa anavifanya, nikiwasimulia watu wanacheka sana, mfano kwetu tumezaliwa wanane lakini mimi ndio mtoto pekee tangu msingi ya dunia kuumbwa niliyempandisha mama yangu ndege kwa mara ya kwanza, hilo tu linawafanya watu wacheke na kukumbuka wazazi wao wakati mwingine,

“Kwetu kuna vitu wadogo zangu wanafanya vinanichekesha na wazazi kwa ujumla hilo linanifanya niwataje sana kila mara kwani vinawafurahisha watu wengi.”


SIJAWAHI KUJIPANGA

“Sijawahi kujipanga juu ya kile nitakachokwenda kukisema ila baada ya muda mfupi najikuta nimepata wazo na Mungu huwa ndiye pekee anayenisaidia.

“Wengine wanaandika na kujiandaa hata siku tatu kabla ili waweze kusimama na kupata mtiririko mzuri, jambo ambalo linanitofautisha na wengine.”


KUIGIZA KULIANZA HIVI

“Kwa mara ya kwanza nimeigiza tamthilia ya Jua Kali, wakati hapo awali sikufahamu kama ninaweza kufanya hivyo ijapokuwa nilikuwa shabiki sana wa mchezo huo,

“Nilipokea simu ya Lamata (Leah Mwainyekule) ambaye ndiye bosi wa tamthilia hiyo ya Jua Kali, kuwa anahitaji nifanye naye kazi, jambo ambalo sikuwahi kulitarajia kwenye maisha yangu ila nilikubali na ninaifurahia sana.” 


COMEDY INALIPA SANA

“Nalipwa mpaka Sh3 milioni kwa shoo moja tu. Na sio wakati wote utawachekesha watu kama ilivyozoeleka jukwaani, ila sasa naitwa hadi kwenye mikutano mikubwa ya watu wa heshima.

“Yaani baada ya majukumu yao ya semina basi huwa naitwa kwenda kuwapunguzia mawazo, lakini hii ni kazi inayolipa kuliko hata kuigiza kwani ndani ya muda mfupi napata pesa nyingi kuliko kuigiza au chochote.”                                      

U-MC KAMA UTANI

“Kazi ya u-MC niliianza kama utani tu, mtu mmoja aliniomba ni mwongozee harusi yake na ilifana hata sikujua nilifanyaje lakini watu walicheka sana.

“Nikajikuta napata kazi hizo mara kadhaa nikiwa bado mkoani hivyo niliona bora hii kazi maana kuchekesha sikuwa nafahamu kama nitaweza.”


KUANDAA SHOO YAKO NDIO MCHONGO

“Maisha ya kazi yamenifundisha vingi lakini kubwa zaidi ni namna ya kuandaa shoo yangu mwenyewe, na hiyo ndio inayolipa zaidi.

“Ukialikwa unalipwa pesa ndogo wakati mwingine kwa sababu kazi zetu huwezi kualikwa peke yako kwani hatutumii muda mrefu jukwaani zikizidi basi ni dakika 10 tu.”  


MAVAZI

“Mavazi yangu yana utofauti mkubwa na yanawachekesha watu wengi lakini ni nguo nzuri tu za heshima na kama ile ya kitenge nimeishona kwa Sh15,000 na ile suti ya njano Sh170,000 na kikofia nilikipata kwa Sh20,000.

“Lakini mara nyingi nanunua za mtumba pale Karume halafu nazinyoosha vizuri na hakuna anayejua kama mimi nimetoa mavazi maeneo hayo.”


KAZI YA HESHIMA

“Hii sio kazi ya kawaida, wengi wetu tunaofanya sanaa ya uchekeshaji tuna elimu na huenda baadaye wakatoka viongozi wakubwa kwenye hii tasnia kwa sababu tuna nguvu ya ushawishi,

“Kumchekesha mtu mkubwa sio suala jepesi na sisi ndio watu pekee ambao tunaweza kuwasilisha jambo gumu kwa njia nyepesi na watu wakaelewa, lakini hata mionekano yetu ni ya heshima tunapokuwa katika kazi zetu.”

HAKUNA CHANGAMOTO

“Mambo yote niliyopitia kwangu sio changamoto kwani naamini Mungu ananifundisha kitu hivyo siwezi kusema kama kuna shida yoyote ambayo imeniumiza.”

SAFARI YA KWANZA YA NDEGE

“Kwa mara ya kwanza kupanda ndege nikiwa naenda kwetu Mbeya kusalimia, nilipata tabu, sikuongea na mtu na pia nilihisi kupatwa na ugonjwa wa homa, ila kilichonichanganya zaidi ni maelekezo waliyopewa wazungu yalikuwa mafupi mpaka nikasema kuna siri hatujaambiwa sisi weusi.”

USHAURI WA MAMA

“Mama hanaga ushauri mwingi zaidi ya kuniambia niombe Mungu tu, maana hafahamu sana juu ya mambo haya ya uchekeshaji hivyo hawezi kusema sana.”

UHUSIANO

“Nina uhusiano tena ni siriaz kabisa na watu wengi wanadhani nachekesha muda wote ila mimi ni mkali, ndio sababu ya kutokumuweka wazi mwanamke wangu. 

MAFANIKIO

“Nimeweza kununua usafiri wangu mwenyewe lakini nyumbani pia kuna mabadiliko sio kama hapo awali, lakini sasa naweza kufanya kila ninachokitaka, bila kusahau rangi yangu ya ngozi imebadilika sana sikuwa na weusi huu.”