Mbona Shilole angemuiga Diamond angezungumza kimombo haraka tu

ZUWENA Mohammed ‘Shilole’, ulimi wake husababisha kizaazaa sana kila anapojitahidi kuzungumza Kiingereza. Huboronga kweli, lakini mwenyewe hakomi. Jitihada zake zikawashitua British Council ambao waliona lipo jambo la kufanya ili kulinda hadhi ya lugha yao.
British Council ni kituo cha kimataifa cha Uingereza kinachohusika na uhusiano wa kitamaduni na fursa za elimu. British Council pia hutoa mafunzo ya Kiingereza, hivyo walipoona Shilole ‘anapuyanga’ sana kwenye kuzungumza ung’eng’e, waliona ni aibu kwa lugha yao, ukizingatia wao wapo hapahapa.
Sasa basi, waliamua kumsaka ili wamweke sawa asiendelee kuitia madoa ya ‘broken’ lugha hiyo ya Malkia Elizabeth II. Baada ya kufanikiwa kumpata, wamemwingiza darasani. Hivyo kwa sasa Shilole ni mwanafunzi wa British Council, anafundwa ili akitoka huko asirudie tena broken zake.
Hivi karibuni nilimsikiliza Shilole alipokuwa akihojiwa kwenye kipindi cha CCTV Camera, Redio Times FM. Alisema tangu ajiunge na British Council, Kiingereza chake kimeanza kunyooka. Alisema hapo kabla hata kutamka neno ‘subscribe’ alikuwa hawezi, ila kwa sasa anaweza.
Binafsi nampongeza Shilole kwa hatua hiyo ambayo amepiga. Ni matumaini kwamba akimaliza kufundwa British Council, hataendelea tena kumwaibisha Malkia Elizabeth II. Bila shaka kujua kuzungumza Kiingereza vizuri kumtamsaidia kufungua milango zaidi ya mafanikio, hasa ile ambayo hakuweza kuifungua kwa sababu ya lugha gongana.
Pamoja na pongezi, ni vizuri kumweleza Shilole kuwa amechelewa sana. Ipo njia ambayo ingemsaidia sana kuimudu lugha ya Kiingereza haraka. Ni njia hiyo aliyoitumia supastaa Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Hivi sasa Diamond ni mahiri kwenye utafunaji wa ‘yai’. Huhojiwa mpaka na vyombo vya habari vya kimataifa na minara ya lugha husoma vizuri. Hata pale chenga hutokea, basi huwa chache.
ENGLISH COURSE YA DIAMOND
Mtaalamu wa Kiingereza, Sarah Li Cain, raia wa Canada, ameshaandika vitabu kadhaa, hutoa machapisho mitandaoni, vilevile huzunguka nchi mbalimbali kufundisha Kiingereza. Kitaaluma Sarah ni mwalimu. Ameshaandika makala nyingi kuelezea mbinu mbalimbali za kuzungumza Kiingereza kwa ufasaha.
Hapa nimechagua andiko lake “How to Speak English With Confidence in 9 Easy Steps”. Tafsiri yake ni jinsi ya kuzungumza Kiingereza kwa kujiamini katika hatua tisa rahisi. Katika hizo hatua tisa, nimependa kuizungumza ya tatu inayosema: “Make Friends with English Speaking Expats.” Kwamba tengeneza urafiki na watu wenye umahiri wa kuzungumza Kiingereza.
Ukitaka kujua ‘English Course’ ya Diamond ndiyo hiyo namba tatu; kujenga urafiki na mafundi wa kuzungumza Kiingereza. Uzuri Diamond marafiki aliowatengeneza hawakuwa wa juujuu, bali ni wale ambao hata giza lilipoingia, alichangia nao shuka. Marafiki ambao alitumia muda wake mwingi pamoja naye.
Ndiyo, Diamond amekuwa hodari sana wa kuchagua wapenzi ambao ni mafundi wa kutafuna yai, tena yai lenyewe ni lenye kitunguu. Soma hii orodha; Wema Sepetu, Jokate Mwegelo, Penniel Mungilwa ‘Penny’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’. Unakuwa na wapenzi hao kwa nyakati tofauti halafu usijue Kiingereza si ni kurogwa huko?
Wema anafahamika kwa kutema ung’eng’e. Hawezi kuzungumza sentensi mbili bila Kiingereza. Jokate si mzungumzaji sana wa Kiingereza, ila ni hodari sana. Jokate ni msomi sana huyu mrembo. Penny, kwake ndipo mayai hutagiwa. Zari kwao Uganda mayai ndiyo hukaangwa. Lugha anazozifahamu vyema ni Kiingereza na Kiganda, lakini huzungumza zaidi Kiingereza.
Kama Shilole naye angekuwa na orodha ya wapenzi wenye ufundi mzuri wa Kiingereza, bila shaka angekuwa anakizungumza sana. Maana Diamond hivi sasa ni fundi, ukimwita kwa ajili ya mahojiano ya Kiingereza hana shida. Ulimi unanyooka vema tu.
Shilole labda kwa sababu amekuwa na Nuhu Mziwanda, ambaye naye minara ya Kiingereza haisomi na sasa tayari ameshaolewa na Ashraf Uchebe ambaye ni wazi hiyo lugha kwake bado inaleta usumbufu. Maana kama angekuwa na ufundi mdogo tu wa lugha ya Malkia, asingeshindwa kumfundisha mkewe kutamka neno ‘subscribe’, mpaka aende British Council.
HOJA IELEWEKE VEMA
Haina maana ya kumshauri Shilole aachane na Uchebe ili amsake mwenye utaalamu wa kuzungumza Kiingereza.
Badala yake ni kumfahamisha kwamba, Diamond naye alikuwa mtupu kabisa wa kuziunganisha herufi ili kuyapatia sawia maneno ya Muingereza.
Hivi sasa Diamond si mweupe tena. Wapo watu wengi ambao wamehitimu mpaka vyuo vikuu lakini ukiwasikiliza wanavyotema yai, unajua kabisa ni yai ambalo halijaungwa kitunguu. Wakati Diamond yai lake kwa sasa siyo tu lina kitunguu, bali lina nyongeza ya karoti, pilipili hoho na nyanya maji.
Hivyo, Shilole kama naye angepitia English Course kama ya Diamond, pengine hivi sasa angekuwa na yai zuri tu. Asingekuwa na matatizo ya uzungumzaji mpaka kuwashitua British Council ambao, wameamua kumpeleka darasani ili asiendelee kuiwekea masizi lugha yao kwa broken zake.
Mafanikio ya Diamond kwenye kuzungumza Kiingereza kupitia wapenzi wake ndiyo vijana huita kukanyaga ganda la ndizi. Unateleza tu! Wema, Jokate, Penny na Zari wamemtelezesha Diamond kutoka kutoweza kuzungumza Kiingereza hadi kuwa fundi kabisa.
Mei 2012, Diamond alipata mwaliko wa kufanya shoo ya uzinduzi wa shindano ya Big Brother Africa (BBA), msimu wa Star Game eviction.
Baada ya kumaliza kuwajibika vizuri jukwaani, alifanya mahojiano kidogo na aliyekuwa mshereheshaji wa BBA msimu huo, Ikponmwosa Osakioduwa ‘IK’. Mahojiano yalifanyika kwa Kiingereza.
Diamond aliporejea nchini, alihojiwa kwenye kipindi cha XXL, Clouds FM, na swali mojawapo aliloulizwa lilihusu uwezo wake wa kuzungumza Kiingereza kwenye shoo ya Big Brother. Diamond alijibu: “Haya ni matokeo ya Wema Sepetu English Course.’ Wema hana shule inayofundisha Kiingereza, alimaanisha ukufunzi wa hapa na pale alioupata kwa Wema ulimjenga sana.
Diamond pia amepata kumshukuru Penny kwa kumwezesha kunogesha Kiingereza chake. Sasa kama Wema na Penny ambao ni Waswahili wenzake aliwamwagia sifa kwa kumsaidia kukijua Kiingereza, jiulize kuhusu Zari ambaye Kiswahili hakijui vizuri, kwa hiyo mawasiliano yao yalitumia zaidi Kiingereza.
NI VIJIMAMBO TU
Unashangaa Diamond kujua Kiingereza kupitia wanawake zake? Na unastaajabu ninaposema Shilole naye angemuiga Diamond angekuwa ameshajua Kiingereza? Mjini kuna vijimambo vya kutosha. Kuna watu huanzisha uhusiano wa kimapenzi na wenye nyumba ili tu wasilipe kodi.
Ukishangaa ya Diamond kujua Kiingereza kwa ‘lifti’ ya wapenzi wake, utastaajabu Dar es Salaam jinsi akina dada wa mjini wanapojilegeza kwa madereva wa bodaboda, bajaji, taksi na kadhalika ili tu wapate usafiri kwa urahisi. Wakitaka kwenda kwenye kicheni pati wanatuma sms tu kisha wanateleza. Mdada anajua kwamba kila akitaka kuzunguka mjini atampigia simu ‘bebi’ wake ampeleke.
Wigo ni mpana sana. Wapo wanaume huingia mapenzini na akina mama lishe ili wasiwe na shida ya chakula. Vilevile wapo wadada huchangamka na wenye vibanda vya kuuza chipsi, kwa matarajio ya kula viepe, mishikaki, kuku na soseji bila presha.
Hivyo, Diamond apokee pongezi nyingi kwa matumizi bora ya rasilimali watu. wapenzi wake hakuwa nao tu kwa faida ya kimapenzi, bali pia wamemnoa kwa Kiingereza. Ni sawa na dada anayetoka na dereva wa bodaboda, faida haiishii tu kwenye mapenzi, bali na usafiri anapata.
Shilole apokee ushauri. Yeye hawezi kufanya kama Diamond, maana sasa ni mke wa mtu. Hata hivyo, anayo njia ya kutengeneza marafiki wa kawaida wenye kukijua Kiingereza vizuri ili wawe wanazungumza na kumnoa zaidi. Akimaliza British Council, kama hatakuwa anazungumza mara kwa mara, atasahau tu. Lugha inataka uizungumze kila wakati unapolala na kuamka ili uimudu. Marafiki wa kuzungumza nao ni muhimu.