Maswali albamu mpya ya Rayvanny, The Big One
Muktasari:
- Albamu hiyo iliyotayarishwa na S2kizzy, Beat Killer na Laizer, inakuja baada ya kutoa Sound From Africa (2021) pamoja na Extended Play (EP) nne, Flowers (2020), New Chui (2021), Flowers II (2022) na Unplugged Session (2022).
STAA wa Bongofleva, Rayvanny ameachia albamu ya pili, The Big One (2024) yenye nyimbo 18 ikiwa ni ya kwanza chini ya lebo yake ya Next Level Music (NLM) na tangu ameondoka WCB Wasafi iliyomtoa kimuziki.
Albamu hiyo iliyotayarishwa na S2kizzy, Beat Killer na Laizer, inakuja baada ya kutoa Sound From Africa (2021) pamoja na Extended Play (EP) nne, Flowers (2020), New Chui (2021), Flowers II (2022) na Unplugged Session (2022).
Utakumbuka Rayvanny alitoka kimuziki na wimbo wake, Kwetu (2016) na kuja kuweka rekodi kama msanii wa kwanza Tanzania kushinda tuzo ya BET 2017 na wa kwanza Afrika kutumbuiza katika tuzo za MTV EMAs 2021.
Ndiye msanii wa kwanza Afrika Mashariki kusikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 100 Boomplay Music, pia akiwa msanii wa tatu kutazamwa (views) zaidi ya mara bilioni 1 YouTube baada ya Diamond Platnumz na Harmonize.
Albamu hii mpya ya Rayvanny imeshirikisha wasanii wengi wakali wa Bongofleva, yupo Alikiba, Diamond, Harmonize, Marioo, Jay Melody, Phina, Yammi na Darassa, huku wa kimataifa wakiwa ni King Promise, Khalil Harisson n.k.
Hata hivyo, mradi huu uliokuja kwa kushtukiza unaacha maswali hasa upande wa wasanii walioshirikishwa na wasioshirikishwa, swali la kwanza ni kwanini Diamond ameshirikishwa katika nyimbo mbili?.
Wimbo wake, Nitongoze (2022) ambao amemshirikisha Diamond, sidhani kama ilikuwa na ulazima wa kujumuishwa katika albamu hii maana umetoka siku nyingi na ulifanya vizuri hadi kushinda tuzo ya muziki Tanzania (TMA) kama Wimbo Bora wa Kushirikiana.
Kufanya vizuri huko inamaana uliwafikia watu wengi, sasa ni miaka miwili imepita tangu utoke, kwanini uwekwe katika albamu ya 2024?, hivyo kolabo yake mpya na Diamond ‘Nesa Nesa’ ilitosha kabisa katika albamu hiyo.
Pia utakumbuka Rayvanny alishafanya kitu kama hicho katika albamu yake, Sound From Africa (2021) na kolabo yake na Diamond, Tetema (2019) ilijumuishwa licha ya kutoka zaidi ya miaka miwili nyuma.
Ikumbukwe kwa jumla Rayvanny na Diamond wameshatoa nyimbo 10 pamoja ambazo ni Salome (2016), Iyena (2018), Mwanza (2018), Tetema (2019), Timua Vumbi (2019), Amaboko (2020), Woza (2020), Nitongoze (2022), Yaya (2023) na Nesa Nesa (2024).
Rayvanny anafanya tofauti na utaratibu, mara nyingi nyimbo chache ambazo tayari zimeshatoka ambazo hujumuishwa katika albamu ni zile zilizoachiwa ndani ya mwaka huo ambao albamu pia inatoka, na hizo chache hutolewa kama utangulizi.
Mfano Marioo katika albamu yake ya kwanza, The Kid You Know (2022), nyimbo ambazo tayari zilikuwa zimetoka ambazo zilikuja kuwekwa katika albamu hiyo ni Naogopa (2022) na Mi Amor (2022) ambazo zilitoka mwaka huo huo.
Swali la pili, kwanini katika albamu hii Rayvanny hajamshirikisha msanii pekee wa lebo yake, Mac Voice ambaye ile nguvu yake kimuziki kwa sasa sio kama ambavyo alianza, anaonekana kupoa kwa kiasi fulani.
Ikiwa ni albamu ya kwanza kutoka chini ya NLM, basi Rayvanny alipaswa kumshika mkono Mac Voice ambaye alimtambulisha Septemba 2021 kupitia EP yake, My Voice (2021) huku yeye akisikika katika nyimbo mbili.
Tunafahamu Rayvanny ana mashabiki wengi nje ya nchi na kazi zake zimekuwa zikifanya vizuri katika chati mbalimbali kubwa duniani, hivyo kama angempa nafasi Mac Voice katika albamu yake ni wazi angemuongezea kitu katika safari yake.
Utakumbuka Rayvanny amewahi kushika namba moja chati za Billboard Mexico Airplay kupitia wimbo, Mama Tetema (2021), ikiwa ni mara ya pili kuingia chati hizo baada ya hapo awali kutamba Billboard Top Triller Global Chart akiwa na Dj Cuppy wa Nigeria.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya Rayvanny hajafikiria au kutaka kumpeleka Mac Voice huko na hatujui mipango yao ni ipi pengine tutamsikia katika albamu ya Mac Voice ambayo alishatangaza ujio wake.
Utakumbuka Rayvanny na Mac Voice tayari wameshirikiana katika nyimbo tano, Tamu (2021), Bora Peke Yangu (2021), Pombe (2021), Muongeze (2022) na Mwambieni (2023).
Rayvanny anaungana na mastaa kibao Bongo waliotoa albamu mwaka huu akiwemo Roma (Nipeni Maua Yangu), Jay Melody (Therapy), Young Lunya (Mbuzi), Stamina (Msanii Bora wa Hip Hop), Marioo (The God Son) n.k.
Upande wa EP kuna Anjella (The Black Queen), Rayvanny (ZiiBeats Vol.2), Bwana Misosi (Mbona Kimya), Alikiba (Starter) n.k, huku Zuchu akitangaza kutoa albamu yake ya kwanza, Peace and Money (2024) hapo Desemba 20.
Rayvanny aliyeanzia muziki Tip Top Connection kisha WCB Wasafi, anakuja na albamu akiwa na kumbukumbu ya kuweka rekodi kama msanii wa kwanza Afrika Mashariki kwa albamu yake (Sound From Africa) kusikilizwa zaidi ya milioni 100 ndani ya wiki moja.